Tuesday, February 20, 2024

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA KUENDELEA KUWEZESHWA

 


NA WELLU MTAKI, DODOMA

Serikali inaendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ikiwa ni pamoja na kuboresha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza kasi ya mapambano na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la dawa za kulevya nchini. 

Hayo yamesemwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera bunge na uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa Mwaka 2023

Amesema Serikali imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 Zaidi kilogramu milioni 1 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini huku Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo.

"Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini. Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo. Aidha, jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa" amesema Mhagama.

Aidha amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa zaidi kilogramu milioni 15 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.

"Kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11. Aidha, Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria" amesema Mhagama.

Pia ameeleza kuwa kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini ongezeko hilo ni sababu ya kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za  Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini ambapo sasa zitaitwa  klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya. 




KOKA ATOA FEDHA NA JEZI KWA WASHINDI KIBAHA VIJANA CUP





MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametoa fedha na vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 1.7 kwa ajili ya washindi wa Kombe la Kibaha Vijana Cup.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa Chama Cha Soka Kibaha (KIBAFA) ofisini kwake kwa niaba ya Mbunge huyo Katibu wa Mbunge Method Mselewa amesema fedha hizo na vifaa hivyo vitatolewa kwenye hatua ya fainali itakayochezwa Februari 21 kwenye uwanja wa Mwendapole.

Koka akizungumza kwa njia ya simu amesema kuwa ameamua kujitolea ili kuinua vipaji vya vijana wa Kibaha kwani michezo ni ajira kubwa kwa vijana na wengi wamenufaika kupitia soka na kuwa ni sehemu ya maendeleo.

Amesema kuwa ataendelea kusaidia michezo mbalimbali ili vijana wapate fursa kwenye timu kubwa ambapo chimbuko huanzia chini ambako ndiyo kwenye msingi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa KIBAFA David Mramba amesema kuwa wanamshukuru mbunge huyo kwa kuchochea sekta ya michezo kwenye Jimbo hilo na kuwafanya vijana kushiriki michezo.

Naye Mjumbe wa soka la wanawake kupitia chama hicho Jesca Sihha amesema kutolewa zawadi hizo ni chachu kwa wanasoka na kuomba na soka la wanawake nalo lipewe kipaumbele.

Monday, February 12, 2024

UJENZI MADARASA, USHIRIKIANO WAZAZI, WALIMU NA WADAU KICHOCHEO UFAULU MZURI BUNDIKANI


MTAA wa Uyaoni Kata ya Maili Moja Wilayani Kibaha umeishukuru serikali kwa kujenga madarasa saba yenye thamani ya shilingi milioni 140 kwenye Shule ya Sekondari ya Kata ya Maili Moja Bundikani kwa kipindi cha miaka mitatu na kuifanya iwe na miundombinu mizuri na kuongeza ufaulu.

Aidha serikali ilitoa fedha ambazo zimejenga vyoo matundu 18 pamoja ujenzi wa darasa moja ambalo kwa sasa liko hatua ya umaliziaji na mwaka huu imefuta daraja sifuri kwa kidato cha nne ambapo mtaa huo ni mlezi wa shule hiyo.

Mwenyekiti wa Mtaa huo Fadhil Kindamba amesema kuwa ufaulu mwaka huu wanafunzi 22 wamefaulu daraja la kwanza, 73 daraja la pili 144 daraja la tatu na 130 daraja la nne.

Kindamba amesema ufaulu huo umetokana ushirikiano uliopo baina ya walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu na kuboreshwa kwa miundombinu ya shule.

Katika hatua nyingine mtaa huo unatarajia kujenga vibanda viwili vya biashara kwa ajili ya kuvipangisha ili kujiongezea mapato na tayari wana matofali 500 kwa ajili ya kuanzia ujenzi utakaoanza hivi karibuni.

Amesema pia wanatarajia kuanzisha mnada ambapo tayari eneo limeshapatikana baada ya mwananchi mmoja kwenye mtaa huo kujitolea eneo kwa ajilo hiyo.

Tuesday, February 6, 2024

JINSI SERIKALI ILIVYOBORESHA SHULE YA SEKONDARI MWANALUGALI YAPELEKA MAMILIONI

MTAA wa Mwanalugali B Wilaya ya Kibaha umepokea kiasi cha shilingi milioni 452.6 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili madarasa saba na bwalo la chakula kwenye Shule ya Sekondari ya Mwanalugali.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mwenyekiti wa Mtaa huo ilipo shule hiyo Deodatus Rwekaza amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo ili wanafunzi wasome kwenye mazingira mazuri.

Rwekaza amesema kuwa fedha kiasi cha shilingi milioni 240 kwa ajili ya bweni moja ilitolewa na limekamilika linatumika, bweni la pili ilitolewa fedha kiasi cha shilingi milioni 120 zimetolewa na ujenzi umefikia hatua ya kupaua.

"Fedha nyingine ni kiasi cha shilingi milioni 88 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba ambapo sita yamekamilika moja likiwa bado tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya elimu,"amesema Rwekaza.

Amesema kuwa fedha kiasi cha shilingi milioni 100 zometolewa kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la wanafunzi ambalo ujenzi wake umefikia hatua ya linta.

"Shule hii pia imechimbiwa kisima kirefu kutoka kwa wafadhili kutoka taasisi ya Ishik Education and Medical Foundation ya nchi ya Uturuki tunawashukuru sana kwa msaada huo ili kukabiliana na changamoto ya maji,"amesema Rwekaza.

Monday, February 5, 2024

NYUMBU YAITAMBIA AFRICAN LYON

Ofisa Michezo Mkoa wa Pwani katika aliyevaa tisheti ya bluu Grace Bureta akiwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA)  wakifuatilia mchezo wa First League Nyumbu 3-2 African Lyon Fc.

MWENDAPOLE B KUJENGA SHULE YA MSINGI


MTAA wa Mwendapole B Wilayani Kibaha uko kwenye hatua za mwisho katika kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi ili kuwapunguzia changamoto watoto wa mtaa huo kugongwa na magari wakivuka kwenda shule iliyoko mtaa jirani.

Aidha wanafunzi wanaotoka mtaa huo hutembea umbali wa kilometa mbili kwenda na kurudi hivyo kuwa na uhitaji wa shule ili kuwapunguzia umbali mrefu kwenda shule.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Mwenyekiti wa Mtaa huo Abubakary Matumla amesema kuwa mtaa huo una shule za msingi na sekondari za watu binafsi ambazo ni wazazi wachache wenye uwezo wa kuwapeleka watoto wao kusoma hapo.

"Tayari eneo limepatikana lina ukubwa wa hekari nne ambalo ni la mtu binafsi ambaye inabidi alipwe ndipo aliachie hivyo kuna makubaliano na Halmashauri ya Mji wampatie eneo lingine ili apishe hapo tuko hatua za mwisho za mabadilishano,"amesema Matumla.

Matumla amesema kuwa tayari wana tofali zaidi ya 4,000 kwa ajili ya ujenzi huo hivyo wanasubiri tu Halmashauri wampatie eneo lingine ili waanze ujenzi wa shule hiyo ambayo itawaondolea changamoto ya kugongwa au kusoma mbali.

"Wananchi wameshachanga fedha kiasi cha shilingi milioni 1.6 ambapo tunashirikiana na diwani ili kufanikisha kupata eneo hilo na matumaini ni makubwa,"amesema Matumla.

LATRA YACHUKUA HATUA KWA DALADALA ZINAZOKIUKA TARATIBU ZA USAFIRISHAJI/KUKATISHA RUTI

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Pwani imeyachukulia hatua za kisheria mabasi madogo Daladala 53 kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukatisha safari.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na ofisa leseni na usajili wa Mamlaka hiyo Geofrey Mashishi alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Mashishi amesema kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu kwa Daladala zinazofanya safari ndani ya Mkoa huo.

"Hatua hizo tumezichukuwa kwa wasafirishaji hao kwa sababu ya kukiuka masharti ya leseni zao kwa makosa mbalimbali mengine yakiwa ni kutotoa tiketi, kuzidisha nauli na mengine ambayo ni kinyume na taratibu za usafirishaji,"amesema Mashishi.

Amesema kuwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wasafirishaji wanaokiuka masharti ya leseni zao kunahitajika ushirikiano baina yao na wadau wakiwemo abiria.

"Sekta ya usafirishaji ina changamoto nyingi na tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kwashirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wasafirishaji wanafuata kanuni, sheria na taratibu za usafirishaji ili kuondoa malalamiko,"amesema Mashishi.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa abiria ili kujua haki zao na wasafirishaji kujua wajibu wao wanapotekeleza majukumu yao kupitia vyombo vya habari.

"Ukaguzi wa kufuatilia ni endelevu hivyo ni vema wasafirishaji wakazingatia masharti ya leseni zao ili kuondoa changamoto zisizo za lazima kwa wadau wa usafiri,"amesema Mashishi.