Tuesday, February 14, 2023

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI LATATUA MIGOGORO YA MIRADÍ YA UJENZI



Na Mwandishi Wetu Dodoma

BARAZA la Taifa la ujenzi limeendesha mafunzo ya kusimamia mikataba ya ujenzi na utatuzi wa migogoro katika miradi ya ujenzi kwa wadau 155 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Hayo yasemwa Mtendaji Mkuu wa baraza la taifa la ujenzi Dkt.Matiko Mturi wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa baraza hilo katika serikali ya awamu ya sita.

Dkt Mturi amesema wameandaa rasimu ya mapendekezo ya gharama za msingi za ujenzi wa barabara kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na kuwakilisha katika kikao cha wadau wa ndani ya serikali ili kupata maoni na ushauri wao.

"Baraza limefanikiwa kuratibu ,kuandaa na kuwasilisha Wizara ya ujenzi na uchukuzi(sekta ya ujenzi) andiko dhana lenye mapendekezo ya kuboreshwa kwa mfumo wa sheria zinazosimamia ujenzi wa nyumba na majengo nchini,"amesema Mturi.

Amesema mwelekeo wa taasisi katika kutekeleza majukumu ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa sera ya ujenzi nchini,kuandaa na kutekeleza mpango mkakati wa maendeleo wa sekta ya ujenzi,kutoa miongozo mbalimbali ya kitaalam ya maeneo mbalimbali ya ujenzi.

Aidha amesema Taasisi inaendelea kutoa mafunzo kwa wadau wa ujenzi kuhusu maadili na utekelezaji wa miradi ya ujenzi, sanifu jenga na usimamizi wa mikataba ya ujenzi kwa wadau mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo yanayolenga kukuza na kujenga wataalam mahiri katika sekta ya ujenzi.

Monday, February 13, 2023

REDIO ZITANGAZE HABARI ZA VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

NAIBU Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinaendelea kutangaza na kuanda makala na vipindi vinavyolenga Maeneo ya Vijijini ambako kumekuwa na usikivu mkubwa wa Redio.

Methew amesema hayo Jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani ambapo kumefanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji Tanzania.

Amesema kuwa mchango wa vyombo vya habari ni mkubwa sana hasa Redio vimekuwa vikitoa taarifa nzuri hivyo kwa sasa Redio za FM zihakikishe zinakuwa na vipindi na makala nyingi zinazogusa Jamii na Utekelezaji wa Miradi ya serikali ya awamu ya sita.

"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt  Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha inasimamia na kuboresha upatikanaji wa habari serikalini na Taasisi zake kwa umakini na haraka hivyo vyombo vya habari vina haki ya kutumia fursa hiyo viweze kuitangaza nchi iliko toka na ilipo sasa ambapo kuna Utekelezaji wa miradi mingi inayowagusa Wananchi ikiwemo afya, Elimu,maji,nishati na miundonbinu,"amesema Methew.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amepongeza vyombo vya Habari hasa Redio za Dodoma kwa kuendelea kuitangaza Dodoma ambako ndio Makao Makuu ya nchi huku akiwataka wamiliki, wahariri na Waandishi wa habari katika siku mbili wapate fursa ya kuizunguka Dodoma kuona ujenzi unaoendelea kwenye mji wa kiserikali Mtumba kunaendelea ujenzi wa majengo ya wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambapo watakuwa wamefanya utalii wa ndani  ambako serikali imetoa fedha nyingi katika Ujenzi huo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Redio cha Wapo Fm Edina Malisa ameishauri mamlaka ya Mawasiliano TCRA kuhakikisha inakuwa inavitembelea vyombo vya habari na kujadiliana changamoto mbalimbali ambazo wanazipata ili kuweza kushirikiana na serikali ili kuweza kupatia ufumbuzi na kuendana na sheria na kanuni za vyombo vya habari.

Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji Tanzania umewashirikisha wamiliki wa vyombo vya habari, wakurugenzi, wahariri na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hapa nchini ambapo Mkutano huo ni wa siku mbili.

Friday, February 10, 2023

12 WAFA 63 WAJERUHIWA AJALINI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 63 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia Alhamisi Februari 9, 2023 Wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 12 (wanaume nane , wanawake wanne) na majeruhi 63 (wanaume 40 wanawake 23).

Senyamule amesema ajali hiyo imetokea usiku Kata ya Pandambili Kijiji cha Silwa wilayani Kongwa, barabara ya Dodoma - Morogoro.

"Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkoa wa Morogoro na majeruhi wawili wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,"amesema Senyamule.

Amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa  6 usiku na imehusisha lori la mizigo lenye namba za usajili T 677 DVX na basi la abiria  la Kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 415 DPP lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam.

Akizungumza na wakazi wa Pandambili eneo ambapo ajali ilipotokea Senyamule ametoa rai kwa jamii kutii sheria bila shuruti ili kuepuka ajali. 

"Serikali ilikuwa na nia njema ya kuruhusu vyombo vya usafiri kutembea usiku, lakini sasa baadhi ya madereva wanaanza kutozingatia Sheria za usalama barabarani, tutaendelea kuwachukulia hatua kali,"amesema Senyamule.a

Pia mewatembelea majeruhi katika Hospitali ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na kutoa pole na kuwatakia uponyaji wa haraka.

Naye Mkuu wa Operesheni na Mafunzo  wa Jeshi la Polisi Kamishna Awadh Haji ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi kutaka kulipita gari la mbele yake bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na lori hilo  lililokuwa limebeba saruji.


WATUMISHI HOUSING A YAJENGA NYUMBA KWA WATUMISHI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WATUMISHI Housing Investment (WHI) imeweza kujenga nyumba 983 kwa ajili ya watumishi wa umma katika mikoa mbalimbali nchini.

Aidha kupitia kampuni yake ya ujenzi imeshiriki katika ujenzi wa mji wa serikali Jijini Dodoma pomoja na majengo ya taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa chuo Cha utumishi wa umma katika mkoa wa Singida.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi mtendaji wa WHI Dkt Fred Msemwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa taasisi hiyo ambapo kumekuwa na ongezeko la kushuka kwa bei ya nyumba kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30.

Amesema kuwa wanategemea kuwa na miradi mipya ya ujenzi katika mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo ni Kawe, Dodoma, Gezaulole, mradi wa viwanda Arusha pamoja na nyumba za watumishi Halmashauri mpya.

"Yapo baadhi ya mafanikio ambayo taasisi imefanikiwa ikiwa ni pamoja na kupata vifaa vya upimaji wa ardhi vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kutoka serikalini kupitia mkopo wa benki ya dunia unaoratibiwa na benki kuu ya Tanzania,"amesema Msemwa.

Watumishi Housing Investment ni taasisi ya umma iliyo chini ya ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) iliyoanzishwa Mwaka 2014 na ilianzishwa na serikali kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSSSF), mfuko wa hifadhi ya jamii ( NSSF) pamoja na shirika la nyumba la Taifa na mfuko wa bima ya Afya (NHIF)

Wednesday, February 8, 2023

NSSF YAKUSANYA BILIONI 165.7

Na Mwandishi Wetu Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba amesema kuwa katika nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Desemba 2022 umekusanya shilingi bilioni 165.7 kutokana na mapato ya uwekezaji na vitega uchumi vya Mfuko. 

Hayo yamebainishwa leo Februari 8,2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mshomba amesema kiasi hicho cha mapato hakijajumuisha ongezeko la thamani ya vitega uchumi vya Mfuko huo na kuongeza kuwa katika kipindi husika thamani ya vitega uchumi vya Mfuko ilikua na kufikia shilingi trilioni 5.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7 ikilinganishwa na thamani ya shilingi trilioni 5.4 iliyofikiwa katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022.

"NSSF wana fursa za nyumba za makazi salama kupitia mfuko huo mwananchi anaweza kumiliki nyumba ya ndoto yake kwa kulipa gharama ya nyumba kwa mkupuo mmoja au kulipa kidogo kidogo wakati wakiendelea kuishi katika nyumba husika na nyumba hizo zipo Dungu, Mtoni Kijichi na Toangoma Jijini Dar es Salaam,"amesema Mshomba.

Amesema serikali imetekeleza mikakakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wakubwa ikiwa ni pamoja na kupitia maonesho ya filamu ya The Royal Tour.

"Miradi hiyo pekee imechangia takribani wanachama wapya 33,066 na kwa ujumla mkakati huo wa Serikali umechangia katika ongezeko la wanachama na michango inayokusanywa na Mfuko,"amesema Msomba.

Ameongeza kuwa kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali kuvutia uwekezaji na kufungua fursa mpya za biashara, wastani wa makusanyo ya michango kwa mwezi yameongezeka na kufikia shilingi bilioni 134 kutoka wastani wa shilingi bilioni 118 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022 ikiwa ni sawa na asilimia 14.

MAMLAKA YA USIMAMIZI BAHARI KUU KUJENGA KIWANDA KUCHAKATA SAMAKI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA ya kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu inatarajia Kujenga Kiwanda kikubwa cha kuchakata Samaki Mkoani Tanga ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 100 kwa siku ambacho kitagharimu Dola Milioni 10 na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo,Dk Emanuel Sweke wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya usimamizi wa Bahari Kuu. 

Sweke amesema kuwa katika kudhibiti uvuvi haramu  Mamlaka hiyo imeweza kuweka mifumo madhubuti ambayo inaendana na Teknolojia kwakufanya doria mbalimbali kwa ajili ya kukomesha uvuvi haramu.

"Kutokana na shughuli zake Mamlaka hiyo imeweza kuvunja rekodi ya kukusanya mapato mengi kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi kufikia shilingi bilioni 4.1 na wametoa jumla ya leseni za uvuvi 5336,"alisema Sweke.

Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu imeanzishwa rasmi Mwaka 2010 lengo lake likiwa ni kusimamia shughuli zote za uvuvi wa Bahari Kuu na ufuatiliaji.

WACHIMBA VISIMA VYA MAJI WATAKIWA KUWA NA VIBALI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BODI ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu imewataka wadau wa maji nchini kuzingatia na kufuata taratibu za uchimbaji wa visima vya maji ikiwemo kupata vibali halali ili kupata maji yenye ubora na kuondokana na malalamiko mengi ya maji yasiyo na viwango.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi ameeleza hayo  wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji chini ya bodi hiyo.

Mmasi amesema wadau wa maji wanapaswa kufahamu madhara ya kuchimba visima bila vibali na kupelekea changamoto ya ubora wa maji kwenye maeneo mengi jambo linaloweza kuleta madhara kiafya.

"Baadhi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kutumia maji yasiyo na madhara kuwa ni pamoja na kuhakikisha maji yanayopatikana baada ya kuchimbwa yanapelekwa maabara kuchunguzwa iwapo yanafaa kwa matumizi au la,"amesema Mmasi

Aidha amesema kuwa bodi hiyo imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto ya tatizo la maji katika mikoa ya Dar es salaam,Pwani na Morogoro kwa kuchimba visima vya maji