Tuesday, August 30, 2016

WAILILIA HALMASHAURI KUWAJENGEA SOKO BAADA YA SOKO KUTAKIWA KUVUNJWA

Na John Gagarini, Kibaha
USHIRIKA wa Wafanyabiashara wa Soko la mkoa la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwapatia eneo lingine la kufanyia biashara baada ya eneo wanalofanyia shughuli zao ambalo liko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa kuvunjwa baada ya miezi mitatu kuanzia mwezi Agosti.

Akizungumza mara baada ya mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika mjini Kibaha mwenyekiti wa ushirika huo Ally Gonzi alisema kuwa hadi sasa hawajui hatma yao mara zoezi hilo litakapofanyika.

Gonzi tunaiomba Halmashauri kutujengea soko au kama hawataweza kujenga ndani ya muda huo wa miezi mitatu ni vema wakaiomba wakala hao kutuongezea muda wa kuwa hapa hadi pale tutakapokuwa tumejengewa soko jipya.

“Tunamwomba Rais John Magufuli kutuangalia kwani hapa tuko zaidi ya miaka 30 na hadi sasa Halmashauri bado haijatujengea soko ambalo waliahidi kutujengea kutokana na eneo hilo kutokuwa la halmashauri,” alisema Gonzi.

Alisema kuwa kwa kipindi kirefu Halmashauri hiyo imekuwa ikiahidi kuwajengea soko la kisasa kwenye kitovu cha mji lakini hadi wanapewa barua za kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo na Tanroads hadi sasa hawajajengewa soko.

“Tunachoona kwa sasa kwa kuwa soko bado halijajengwa ni vema wakatuongezea muda hata wa miaka miwili kwani Halmashauri ilisema itakuwa imejenga soko ndani ya miezi 18 hivyo kwa kipindi hicho ni bora tungebaki hapa kwanza lakini vinginevyo hatujui tutakwenda wapi,” alisema Gonzi.

Aidha alisema kuwa mbali ya wao kutokuwa na mahali pa kufanyia biashara pia Halmashauri itakosa mapato kwnai soko hilo ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato pia wao walikuwa wakitegemea hapo kwa ajili ya kujipoatia kipato chao na familia zao.


Mwisho. 

UVUNJAJI SHERIA WASABABISHA MIGOGORO YA ARDHI

Na John Gagarini, Rufiji

IMEELEZWA kuwa kuwepo kwa migogoro ya ya wakulima na wafugaji  katika Halmashauri ya Rufiji mkoani Pwani kunatokana na  baadhi ya wafugaji kuvunja sheria na taratibu zilizowekwa na   kwenda kulisha mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya shughuli mbali mbali za kilimo.

Hayo yalisemwa na Mbunge  wa Jimbo la Rufiji Mkoani humo Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza na viongozi wa Halmashauri Mpya ya Rufiji ambapo ameahidi kulivalia njuga suala la migogoro ya ardhi inayotokana na jamii ya wafugaji na wakulima ambao wamekuwa wakigombania maeneo ya mashamba na kusababisha kutokea kwa mapigano ambayo wakati mwingine yanapelekea uvunjifu wa amani.

Mchengerwa alisema kuwa hawezi kuwavumilia wale wote ambao wataonekana wanakwenda kinyume cha sheria za nchi, na kuhakikisha kila mfugaji na mkulima anatengewa maeneo yao rasmi kwa ajili ya kufanyia shughuli zake ili kuepukana na migogoro na  mapigano ambayo yamekuwa yakijitokeza kutokana na kugombania ardhi.

“Nitaweka mikakati kabambe ambayo itaweza kuwawasaidia wananchi wakiwemo wafugaji na wakulima kwa kushirikina na viongozi wa halmashauri katika kuwatenge maeneo yao maalumu ambayo yataweza kusaidia kuepukana na migogoro hiyo ya ardhi,” alisema Mchengerwa.

Alisema kuwa anatambua kuwepo kwa changamoto kubwa na  migogoro kati ya wakulima na wafugaji, lakini dhamira yake kubwa anataka kuona wanachi wake wa jimbo la rufiji wanakaa kwa amani bila ya kuwepo kwa mapigano yoyote na kuhakikisha kwamba sula la amani na utulivu linakuwepo.

“Natambua wananchi wengi wa Jimbo la Rufiji wanategemea sana shughuli za kilimo hivyo kwa sasa wameshaweka utaratibu wa kutenga maeneo ya wafugaji ili wasiweze kuingia katika mashamba ya wakulima na kupelekea vurugu za mara kwa mara kitu amabcho sio kizuri na kinarudisha nyuma maendeleo,” alisema Mchengerwa.

Naye Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Saidina Malenda mara baada ya kushinda katika uchaguzi huo  alisema  atahakikisha anasharikina bega kwa bega na viongozi wenzake kwa lengo la kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi wa Rufiji.

Malenda alisema kuwa anawashukuru madiwani wenzake kwa kuweza kumchagua kuwaongoza na kubainisha kwamba atafanya kazi bidii zote na kwa kushirikina katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo  bila ya kuwa na ubaguzi wa aina yoyote wa itikadi ya vyama  ili kuweza  kuwatumikia wananchi katika huduma mbali mbali wanazozihitaji.

Katika uchaguzi huo wa halmashauri mpya ya Wilaya ya Rufiji,uliofanyika utete nafasi ya Mwenyekiti ilikwenda kwa Saidani Malenda ambaye alipata kura 11 kati ya kura 19 zilizopigwa, ambapo nafasi ya Makamu mwenyekiti ilikwenda kwa Hawa Mtopa  ambaye aliyepata kura 10 katika ya kura 19 zilizopigwa.
     

MWISHO

PANGANI WALILIA ZAHANATI


Na John Gagarini, Kibaha

KATA ya Pangani wilayani Kibaha inatarajia kubadilisha ofisi za Mtaa wa Kidimu kuwa Zahanati ili kukabiliana na changamoto ya mtaa huo kutokuwa na zahanati hivyo kufanya huduma za matibabu kupatikana kwa ugumu.

Akizungumza na waandishi wa habari diwani wa kata hiyo Agustino Mdachi alisema kuwa gharama za kufuata matibabu kwa wakazi wa mtaa huo ni kubwa na kuwafanya wagonjwa kuwahatarini pale wanapokuwa wamepatwa au kuzidiwa na ugonjwa.

Mdachi alisema kuwa tegemeo kubwa ni hospitali ya wilaya ya Kibaha ya Mkoani ambayo iko umbali wa kilometa 18 na ile ya jirani ya Mpiji Magohe ambayo iko kata ya Mbezi wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo usafiri wa pikipiki ni shilingi 5,000.

“Mgonjwa anapotaka kwenda Mkoani humbidi kuwa na shilingi 50,000 hasa nyakati za usiku na mchana ni 40,000 au 30,000 gharama hizi kwa ajili ya kwenda kupata matibabu ni kubwa sana na kwa mwananchi wa kawaida kumudu ni ngumu sana,” alisema Mdachi.

Alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo wameamua kuibadili ofisi hiyo na kuwa zahanati ya mtaa ambapo wananchi watapa huduma karibu.

“Kwa sasa tuko kwenye mchakato kwa kuwaomba Halmashauri ya Mji kuturuhusu na kuleta wataalamu wa afya ili waangalie namna ya kulifanya jengo hilo kuwa zahanati na tunaamini ombi letu litakubaliwa,” alisema Mdachi.

Aidha alisema kuwa kutokana na ukubwa wa jengo hilo la serikali ya mtaa kuwa vyumba vingi wanaamini kuwa litafaa kwa ajili ya kuanzia huduma za kiafya wakati wanafanya mipango ya kujenga sehemu nyingine.

“Kwa kuwa ya kata ina ofisi nyingi tunaweza kutoa chuma kimoja kwa ajili ya ofisi ya mtaa ili kufanikisha zoezi hilo ambalo litawafanya wananchi wa mtaa na kata hiyo kupata huduma za afya karibu,” alisema Mdachi.

Aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujitolea katika masuala mbalimbali ya maenedeleo ikiwa ni pamoja na kufanikisha zoezi hilo la ujenzi wa zahanati hiyo.


Mwisho.

MADARASA YAUNGUA MOTO

Na John Gagarini, Kibaha

MADARASA matatu na ofisi ya Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Kongowe wilayani Kibaha mkoani Pwani zimeungua na moto ambao ulitokea juzi usiku na kusababisha hasara kubwa.

Akizungumza na Patapata mwenyekiti wa mtaa wa Kongowe Maimuna Jamhuri alisema kuwa moto huo ulitokea Agosti 28 majira ya saa nne usiku ambapo chanzo chake bado hakijafahamika mara moja.

Jamhuri alisema kuwa moto huo ulianzia kwenye ofisi hiyo ambayo ni ya mwalimu mkuu na kuenea kwenye madarasa pamoja na chumba cha kuhifadhia vitabu ambavyo navyo vimeteketea kwa moto huo ambao ulikuwa mkali.

“Moto huo ulizimwa na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi ambapo gari la zimamoto lilifika kwa kuchelewa kutokana na kuwa kwenye harakati za kuzima moto sehemu nyingine”, alisema Jamhuri.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kongowe Iddi Kanyalu alisema kuwa baada ya kutokea moto huo viongozi kadhaa walifika akiwemo mkurugenzi, Mwenyekiti na Injinia wa Halmashauri kwa ajili ya kuangalia athari za moto huo.

Kanyalu alisema kuwa kutokana na makisio ya harakaharaka zinahitajika zaidi ya milioni 50 kwa ajili ya kujenga upya madarasa hayo na ofisi kwani madarasa hayo yameharibika sana na hayafai kwa matumizi wala kufanyiwa ukarabati.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo leo kamati ya maenedeleo ya kata ina kaa kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo limewakumba wanafunzi 200 waliokuwa wanatumia madarasa hayo.

Naye mtendaji wa kata hiyo ya Kongowe Said Kayangu alisema kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Beatus Lingumbuka alitapa athari kidogo kichwani na mikononi kwani alikuwa kwenye harakati za kujaribu kuokoa baadhi ya vitu wenye ofisi yake.

Kayangu alisema kuwa kutokana na jitihada za wananchi wameweza kuokoa madawati kwenye madarasa hayo ambayo yalikuwa hatarini kuungua lakini hata hivyo waliweza kuyatoa na hakuna dawati hata moja lililoungua

Mwisho.


WAAMUZI KIBAHA WAPATA VIONGOZI WAPYA

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT) mkoa wa Pwani kimemchagua  Jeremia Komba kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kupata kura 15 huku mpinzani wake Kassim Safisha akipata kura tano.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika mjini Kibaha na kusimamiwa na mwamuzi mkongwe Hussein Magoti na kuwashiriki waamuzi ambao ni wanachama wa chama hicho cha waamuzi.

Komba alikuwa akichuana na mwamuzi mwenzake Kassim Safisha nakumshinda kwa tofauti ya kura tano hivyo kumfanya Komba kuwa bosi wa waamuzi wilaya ya Kibaha.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilikwenda kwa Sayenda Lubisa ambaye hata hivyo hakuwa na mpinzani na kujipatia kura 17 huku tatu zikiharibika.

Upande wa katibu mkuu Endrew Kayuni alikuwa mshindi kwa kupata kura 15 huku Mohamed Juaji akipata kura tano, nafasi ya katibu msaidizi ilikwenda kwa Hamis Mpangwa ambaye alijinyakulia kura 11 akimshinda Mohamed Msengi aliyepata kura tisa.

Nafasi ya mweka hazina ilikwenda kwa Kassim Naroho aliyepata kura 16 akimshinda Nickson Haule aliyepata kura nne, kwa upande wa mwakilishi wa mkutano mkuu ilikuwa na mgombea mmoja Hamad Seif ambaye alipata kura 19..

Kwa upande wa kamati ya utendaji nafasi tatu walioshinda ni Kasule Ambogo kura 18, Leah Petro kura 16, Gabriel Kinyogoli kura 15 na Sultan Singa kura nane ambapo mwenyekiti mpya Komba aliwataka waamuzi kuwa na mshikamano.

Komba alisema kuwa jambo kubwa ili waweze kufikia malengo ni kuwa nidhamu na kuzingatia sheria kwa kuzitafsiri wawapo uwanjani ili kuondoa malalamiko dhidi yao kwani baadhi wamekuwa wakienda kinyume na sheria za mchezo huo.


Mwisho.



 

ATISHIA KUWABAKA WANAFUNZI


Na John Gagarini, Chalinze

MWENYEKITI wa Halmashauri ya mji wa Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Said Zikatimu ameutaka uongozi wa Kitongoji Cha Msanga kata ya Talawanda uhakikisha inamkamata mtu ambaye anatishia kuwabaka wanafunzi wa shule ya Msingi Msanga.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Talawanda wakati wa ziara yake kuangalia shughuli za maendeleo kwenye kata ya Talawanda alisema kuwa mtu huyo hapaswi kuachwa kwani anahatarisha afya za wanafunzi hao.

Zikatimu alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wakike wa shule hiyo tayari wameshatoa taarifa dhidi ya mtu huyo ambaye huwa anawakimbiza kwa nia ya kuwafanyia kitendo hicho na endapo hatakamatwa anaweza kutekeleza azma yake hiyo mbaya.

“Mtu huyo inasemekena yuko Kijijini hapa amekuwa akificha sura yake ili asifahamike amekuwa akijificha kwenye vichaka na kuwakimbiza wanafunzi kwa nia ya kutaka kuwabaka hivyo lazima viongozi muweke mtego ili mumkamate mtu huyo ambaye ni hatari,” alisema Zikatimu.

Alisema kuwa serikali haiwezi kukaa kimya kwa mtu wa namna hiyo ambaye ni hatari kwa wanafunzi na kuwafanya watoto wa kike wasisome kwa amani hivyo lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kumdhibiti mapema.

“Lazima mfanye mpango wa kumkamata mtu huyo pia mnaweza kupiga kura ili kumbainisha mtu huyo ambaye baadhi ya watu wanamfahamu na wengine hawamfahamu ambapo kwa kutumia kura anaweza kufahamika kwa urahisi,” alisema Zikatimu.

Aidha alisema kuwa kamati za ulinzi na usalama ya Kijiji na Kitongoji zinapaswa kulishughulikia suala hilo na wananchi kutolifumbia macho kwani mtu huyo anaweza kufanya kweli endapo hatua hazitachukuliwa mapema.

Mwisho.

Thursday, August 11, 2016

MZEE WA BARAZA LA MAHAKAMA APANDISHWA KIZIMBANI KWA RUSHWA

Na John Gagarini, Kibaha

TAASISI ya Kuzuia na Kupamaba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Pwani imemfikisha mahakamani Mzee wa Baraza la Mahakama ya Mwanzo Maili Moja Kibaha Francis Ndawanje kwa tuhuma za kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi 100,000 ili kumsaidia mtuhumiwa kushinda kesi yake.

Mtuhumiwa alisomewa mashitaka kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha  mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Pwani  Herieth Mwailolo ambapo kwa upande wa chini ya mwendesha mashitaka kutoka TAKUKURU Mkoa Pwani Sabina Weston.

Akisoma maelezo juu shitaka hilo Weston aliiambia Mahakama kuwa mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kutenda makosa hayo mawili kati ya tarehe 3 na 4  Agosti mwaka huu ambapo.

Mahakama iliambiwa kuwa mtuhimwa aliomba rushwa Agosti 3 kwa Omary Hoza ili amsaidie mkewe Mariamu Hoza ambaye ana kesi namba 324 kwenye mahakama hiyo hivyo kumuomba rushwa ya shilingi 100,000.

Ikaelezwa kuwa mtuhumiwa alipokea rushwa siku iliyofuata Agosti 4 alipokea fedha hizo eneo la jirani na Kituo cha Polisi Tumbi jirani na barabara kuu ya Morogoro Maili Moja wilayani Kibaha.

Baada ya kusomwa mashtaka hayo mtuhumiwa alikana tuhuma hizo ambapo upande wa Taasisi hiyo ulisema kuwa hauna pingamizi na dhamana kwa mtuhumiwa ili mradi akamilishe masharti ya dhamana na yuko nje kwa dhamana ya shilingi 500,000 kwa wadhamini wawili kila mmoja.

Hakimu alisema kuwa wadhamini wanapaswa kuhakikisha mtuhumiwa anafika siku ya kesi hiyo ambayo imepangwa kufanyika Agosti 15 mwaka huu.

Mwisho.