Na John Gagarini, Kibaha
WANAFUNZI 204 mkoani Pwani hawakufanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi kwa mwaka 2015
kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Katibu
Tawala wa mkoa huo Mgeni Baruan wakati wa kutangaza matokeo ya wanafunzi
waliofanya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2015 na kusema kuwa jumla ya
wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 22,191 sawa na asilimia 99.1.
Baruan alisema kuwa wanafunzi ambao hawakufanya mtihani kutokana na
sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro 185, vifo watano, ugonjwa wanane,
huku sababu nyingine wakiwa ni wawili.
“Ukiachilia mbali wanafunzi hao ambao hawakufanya mtihani na ufaulu wa wanafunzi kwa mkoa huo umefikia
asilimia 63.1 ikilinganishwa na mwaka 2014 sawa na asilimia 56.2.,” alisema
Baruan.
Alisema kuwa wanafunzi 14,010
wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016 kati ya wanafunzi baada
kufaulu mtihani wao wa kumaliza elimu ya Msingi ambapo wanafunzi wote
waliofaulu wamepata nafasi na hakuna aliyekosa nafasi.
“Kati ya idadi ya wanafunzi waliofanya
mtihani ni wavulana ni 10,024 na wasichana ni 12,167 huku ikionyesha kuwa mkoa
haukupata tuhuma za udanganyifu katika zoezi la ufanyaji mtihani,” alisema
Baruan.
“Mkoa umeshika nafasi ya 14 kitaifa
hata hivyo ufaulu huo hauridhishi kwani haujafikia kiwango cha asilimia 80 kwa
mujibu wa mwelekeo wa Matokeo Makubwa Sasa Big Results Now (BRN) hivyo
zinahitajika jitihada zaidi ili kufikia kiwango hicho,” alisema Baruan.
Kwa upande wake ofisa elimu mkoa
Yusuph Kipengele alisema kuwa agizo la Rais la Dk John Pombe Magufuli la
kuondolewa kwa ada na michango mbalimbali kuanzia shule ya msingi na sekondari
liko palepale.
Kipengele alisema kuwa baadhi ya
michango iliyoondolewa ikiwa ni pamoja na ada ni vitambulisho, mawadati,
majengo, vifaa vya michezo mlinzi haitakuwepo na mwalimu atakayechangisha
mchango wowote atakuwa anakiuka agizo la Rais.
Hata hivyo alisema kuwa jukumu la
wazazi ni kumnunulia vifaa vya shule mwanae ikiwa ni pamoja sare za shule,
madaftari, kalamu, chakula, nauli na vifaa vingine vidogovidogo ambavyo siyo
mzigo kwa mzazi yoyote.