Sunday, September 13, 2015

MBUNGE KUTOA M 700 KUSAIDIA WAJASIRIAMALI

Na John Gagarini, Kibaha
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Silvestry Koka ameunga mkono mpango wa kukipatia kila kijiji hapa nchini shilingi milioni 50 za uwezeshaji wajasiriamali kwa kuahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 700 kwa Jimbo hilo kwenye mpango huo.
Alitoa ahadi hiyo  wakati wa uzinduzi wa kampeni kwenye Jimbo hilo zilizofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja Kibaha mbele ya Mgombea Mwenza wa CCM Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi na kusema kuwa mpango huo ni mzuri na unapaswa kuungwa mkono na wadau wa maendeleo.
Koka ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo anatetea kiti chake alisema kuwa tangu achaguliwe amekuwa akiwawezesha wajasiriamali wa Jimbo lote la Kibaha kwa kuwapatia fedha za kuwezesha vikundi vyao pamoja na mafunzo.
“Nimefurahishwa na mapango huo ambao ndiyo ilikuwa ajenda yangu ya kutaka wajasirimali waweze kuendeleza shughuli zao hivyo naipongeza serikali kwa kuona kuwa kuna haja ya kutoa fedha kwa ajili kuongeza pato la wananchi,” alisema Koka.
Alisema kuwa katika muda wake wa Ubunge miaka mitano iliyopita alitoa zaidi ya shilingi zaidi ya milioni 500 kwa wajasiriamali pamoja na kuwapatia elimu ya ujasirimali kupitia vikundi alivyohamasisha kuanzishwa.
“Nitatoa fedha hizo kwa kuiunga mkono serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini ambao wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao,” alisema Koka.
Naye Mgombea Mwenza Samia Suluhu alisema kuwa mpango huo utawezesha wajasiriamali kukuza mitaji yao na  serikali itasimamia ipasavyo fedha hizo ili zisiweze kutumika vibaya ili ziweze kuleta manufaa kwa wananchi.
Samia alisema kuwa wenyeviti wa Vijiji ambao watazinyemelea fedha hizo kwa manufaa yao binafsi wajiandae kwani wale watakaozitumia kinyume cha taratibu watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwashtaki. Pia fedha kwa akinamama na vijana asilimia 10 kwenye halmashauri atasimamia na kuhakikisha zinatolewa kama taratibu zinavyoonyesha.

Mwisho.  

Sunday, September 6, 2015

BAKWATA WAASA UCHAGUZI MKUU

Na John Gagarini, Kibaha
KAIMU Mufti Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Abubakari Zuberi amesema kuwa wanasiasa wanaokosa nafasi za uongozi wasiwe chanzo cha kuvunja amani ya nchi katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa maombi maalumu ya kuombea amani ya nchi yailiyoandaliwa na BAKWATA mkoa wa Pwani na kuwashirikisha viongozi na waumini wa kiislamu wa mkoa huo pamoja na waumini wa dini mbalimbali.
Mufti Zuberi alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi walioshindwa na watakaoshindwa kwenye kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa wanaonesha viashiria vya kutaka kuvunja amani iliyopo kutokana na kutokubali kushindwa.
“Kwa sasa tunaona viashiria mbalimbali vya kutaka kuvunja amani ya nchi     kutoka kwa baadhi ya wanasiasa hapa nchini na kutokana na hali hiyo tumeona ni vema tukafanya maombi haya kwa ajili ya kumwomba Mungu atunusuru na hali hiyo ili isije ikajitokeza,” alisema Mufti Zuberi.
Alisema kuwa Tanzania ni kama chumvi ya amani ambayo ikitumika vizuri itaongeza ladha lakini ikitumika vibaya itaharibu kila kitu hivyo ni vema Watanzania wakaendelea kuilinda amani iliyopo kwa sasa kwani baadhi ya majirani zetu wameathiriwa na vita na wanakimbilia kwetu.
“Tumwombe Mungu aendelee kutudumishia amani iliyopo kwa muda mrefu na tusikubali kuivunja amani yetu kwa tama ya baadhi ya watu wenye uroho wa madaraka kwani endapo amani itavunjika tutakuwa hatuna pa kukimbilia kwani majirani zetu wanakuja kwetu je sisi tutaenda wapi endapo amani itatoweka,” alisema Mufti Zuberi.
Kwa  upande wake mkuu wa Wilaya ya Kibaha Halima Kihemba ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani alisema kuwa tayari serikali imeweka mazingira ya uchaguzi kufanyika kwa njia ya amani na utulivu.
Kihemba alisema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuhakikisha amani inaendelea kudumu na kuwataka wawaelekeze waumini wao kufuta taratibu zilizopangwa katika kushiriki uchaguzi na wale wote waliojiandikisha watapiga kura na watakaokwenda kinyume cha sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Naye Kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa alisema kuwa tayari wametoa maagizo kwa Maimamu na Masheikh wa misikiti yote kufanya maombi maalumu kila Ijumaa kuiombea amani ya nchi ili uchaguzi uwe wa amani.
Mtupa alisema kuwa maombi hayo maalumu ya kumwomba Mungu kwa wale wenye nia mbaya ya kuleta vurugu washindwe na maombi hayo yatakuwa endelevu hadi uchaguzi mkuu utakapoisha ili hali ya amani iendelee kudumu.
Mwisho.

  

     
 









Picha 1914 Kadhi wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa akizungumza kwenye maombi maalumu kuliombea taifa amani lilofanyika kwenye viwanja vya Bwawani Maili Moja Kibaha.

1918 Baadhi ya wakinamama waliohudhuria maombi maalumu ya kuliombea Taifa kuwa na amani katika uchaguzi mkuu wakiewasikiliza viongozi wao
1922 Mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba akihutubia kwenye maombi maalumu ya kuombea amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
1923 Sheikh Mtonda akiongea kwenye maombi maalumu kuliombea Taifa kuwa na amani kwenye kipindi cha uchaguzi.
1925 Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Pwani Said Lipambila akiwahutubia waumini wa Kiislamu waliohudhuria maombi maalumu kuiombea nchi kuwa na amani kipindi cha uchaguzi
1933 Kaimu Mufti mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Abubakari Zuberi akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria maombi maalumu kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani Kibaha
1936 Baadhi ya wamini wa dini ya Kiislamu wakiwasikiliza viongozi wao wakati wa maombi ya kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani maili Moja Kibaha
1940 baadhi ya waumini wakisikiliza viongozi wao wakati wa maombi maalumu ya kuliombea Taifa
1947 Kaimu Mufti Mkuu Abubakari Zuberi kulia akizungumza na Kadhi wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa wakati wa maombi maalumu ya kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja Kibaha


Wednesday, September 2, 2015

WATAKA MABADILIKO YA SHERIA ZA MIRATHI

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI kupitia vyombo vya kutunga sheria likiwemo Bunge vimetakiwa kubadilisha sheria za mirathi ili wanawake na watoto waweze kupata haki zao mara baba anapofariki dunia.
Hayo yalisemwa na baadhi ya madaktari na wauguzi wa Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, wakati wa mafunzo juu ya kukabiliana na kansa ya kizazi na matiti pamoja na unyanyasaji wa jinsia mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Wanawake Tanzania.
Moja ya washiriki wa mafunzo hayo Mganga wa Kituo cha Afya Mlandizi  Amilen Sam alisema kuwa familia nyingi mara baba anapofariki dunia wanawake wamekuwa hawapati mali yoyote licha ya kuwa wao walihusika katika upatikanaji wa mali hizo.
“Kutokana na sheria  nyingi za mirathi kupitwa na wakati vyombo vya kutunga sheria likiwemo Bunge lazima zibadili sheria hizo ambazo hazimpi nafasi ya kurithi mali ambazo mama kahusika kuzichuma na marehemu mume wake,” alisema Dk Sam.
Kwa upande wake Dk Pascalina Kamba wa Kituo cha Afya Disunyala alisema kuwa baadhi ya mila na desturi nazo ni chanzo cha tatizo hilo kutokana na kutoruhusu mwanamke kuongea lolote juu ya mali walizochuma na mume.
Dk Kamba alisema kutokana na sheria hizo kutungwa miaka ya nyuma ni dhahiri zimepitwa na wakati na hazipaswi kuendelezwa ili mwanamke na mtoto waweze kupata haki zao ikiwa ni matunda ya ndoa na si kuwanufaisha ndugu wa mume ambao hawajui mali hizo zimepatikana vipi.
Kwa upande wake mratibu kutoka mtandao huo wa maendeleo kwa wanawake Tanzania Gaudence Msuaya alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa nafasi walengwa kujadili unyanyasaji uliopo ndani ya jamii pia kuchukua hatua mara waonapo dalili mbaya zinazohusiana na magonjwa ya Kansa ya matiti na shingo ya uzazi.
Msuya alisema kuwa lengo lingine ni kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi hao ili watoe elimu hiyo kwa jamii pamoja na wteja wao wagonjwa ambao wanawapatia huduma ya matibabu kwenye maeneo yao ya kazi.
Mwisho.
  

SHULE YAFUNGWA BAADA YA MWANAFUNZI KUFA KWA KIPINDUPINDU

Na John Gagarini, Kibaha

KUFUATIA kifo cha mwanafunzi wa wa darasa la tatu Shule ya Msingi Maendeleo wilayani Kibaha mkoani Pwani kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu serikali imeifunga shule hiyo kwa muda usiofahamika ili kuwanusuru wanafunzi na ugonjwa huo.

Aidha imepiga marufuku mikusanyiko yote sherehe, misiba, minada ya hadhara na wafanyabiashara ndogondogo wa vyakula kuuza biashara mashuleni, biashara za matunda na vyakula kwenye maeneo ya wazi ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.

Akitoa ufafanuzi juu ya ugonjwa huo kuthibitika kuingia katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na mkoa wa Pwani mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa mwanafunzi mwingine anaugua ugonjwa huo hali iliyosababisha serikali wilayani Kibaha kuifunga shule hiyo kwa muda ili kuchukua tahadhari na kuhofia ugonjwa huo usienee kwa wengine.

“Tunasikitika kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo na tumeona ili kunusuru wanafunzi wengine kuambukizwa tumeifunga shule hiyo na kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula kwenye maeneo ya wazi ikiwemo stendi ya Maili Moja ambapo biashara ya chakula hufanyika nyakati za usiku,” alisema Kihemba.

Kihemba alisema kuwa waliamua kuchukua hatua hizo za dharura ili kupunguza kuenea ugonjwa huo ambao na wafanyabiashara waache tabia ya baadhi ya wananchi ya kutiririsha maji machafu kwenye mitaro na mifereji ya barabarani.

“Nawaomba wananchi kuzingatia maagizo hayo na kuzingatia kanuni za usafi ili kuepuka ugonjwa huo ambao endapo hatua za haraka hazijachukuliwa husababisha kifo,” alisema Kihemba.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya hiyo amekemea vitendo cha baadhi ya wananchi kwenda kupatiwa matibabu kwenye hospitali za mitaani hali inayosababisha kushindwa kupona ama kugundulika kwa ugonjwa huo hatimaye kusababisha vifo.

“Kwa sasa tayari tumeshachukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuagiza madawa ya kutokomeza ugonjwa huo wa kipindupindu katika mamlaka husika na wanafunzi wa shule ya msingi maendeleo wamepatiwa dawa wote na wanafunzi wote wa shule hiyo wamepatiwa dawa,” alisema Kihemba.

Aidha alisema Idara ya afya mkoani humo imetenga maeneo ya kuwalaza baadhi ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo kwa ajili ya kuwapatia vipimo maalumu na kuwaanzishia  tiba mahususi ya ugonjwa huo.
  
“Kuanzia tarehe 24 Agosti mwaka huu wilaya ya Kibaha imepokea wagonjwa wenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu wapatao 11 katika kituo cha afya Mlandizi na Mkoani, ambapo wawili kati yao waligundulika kuwa na ugonjwa huo na mmoja ambae ni mwanafunzi alifariki dunia kabla ya matibabu.

Alibainisha kuwa wagonjwa waliopokelewa walikuwa ni kutoka maeneo ya Maili Moja, Muheza, Tangini na Makuruge wilaya ya Kisarawe, Msigani na Mpiji Majohe wilaya ya Kinondoni, Visiga na Magindu Kibaha vijiji , Ruvu Darajani Bagamoyo ambapo kati yao watatu ndio waliogundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya kufanyiwa vipimo .

Mwisho

CCM MUFINDI WATAMBA KUSHINDA UCHAGUZI MKUU

Na John Gagarini, Mafinga
KUTOKANA na Utekelezaji wa Ilani kikamilifu chama cha mapinduzi kinatarajia kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao kwenye nafasi zote za Urais Ubunge na Udiwani
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kimeweka mikakati ya kupata ushindi wa kishindo kwa wagombea wake kwenye nafasi tatu za Urais Wabunge na Madiwani kutokana na utekelezaji wa ilani ya chama.
Hayo yalisemwa na mjini Mafinga na katibu wa CCM wilaya ya Mfundi Jimson Mhagama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa ushindi wa chama unatokana na ilani kutekelezwa kwa asilimia 95.
Mhagama alisema kuwa wilaya hiyo ina majimbo matatu ya Mufindi Kaskazini ambalo linaongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa, Mufindi Kusini linaongozwa na Menrad Kigora na Mafinga Mjini litakalowaniwa na Cosatu Chumi pamoja na kata 36 vyote vikiwa chini ya CCM  hivyo wana uhakika wa kuendelea kuyaongoza maeneo hayo.
“Sisi hatuna wasiwasi tunaendelea kuweka mikakati ya suhindi lakini ushindi wetu utatokana na utekelezaji wa ilani ya chama juu ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali za huduma za jamii ambazo zimeboreka kutokana na uongozi mzuri wa viongozi wa chama,” alisema Mhagama.
Alisema kuwa mfano kwenye huduma za jamii ujenzi wa baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami na changarawe zinazofanya kupitika kwa kipindi chote cha mwaka, uboreshaji wa huduma za afya kwenye Hospitali ya Mafinga na ujenzi wa zahanati kwenye vijiji, uanzishwaji wa vikundi vya ujasiriamali, huduma za taasisi za fedha na ujenzi wa shule za sekondari, uanzishwaji wa vyuo mbalimbali.
Aidha alisema kuwa CCM itaendelea kusimamia ilani yake kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanapatikana ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ambao wamekiamini chama kutokana na kuongoza kwa manufaa ya jamii.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa amemwagia sifa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa kutokana na uchapakazi wake kwenye wizara pamoja na kuhamasisha maendeleo kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini analoliongoza.
Akihutubia wakazi wa mji wa Mafinga wakati wa mkutano wake wa kampeni Lowassa alisema kuwa mbunge huyo ni mchapakazi na amefanya mabadiliko makubwa kwenye Jimbo hilo na kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii.
Lowassa alisema kuwa Mgimwa ni moja ya viongozi wazuri ambao wanawajibika vizuri katika maeneo ambayo wamepewa kuwajibika lakini angekuwa kwenye chama kama CHADEMA angefanya vizuri zaidi.
“Mgimwa namfahamu ni muwajibikaji mzuri katika maeneo ambayo anayaongoza lakini angekuwa upinzani angefanya vizuri zaidi kwani wapinzani wanafanya kazi sana na wana uwezo wa kuleta maendeleo,” alisema Lowassa.
Kwa upande wake katibu wa CCM wilaya ya Mufindi Jimson Mhagama akizungumzia juu ya kauli ya Lowassa alisema kuwa Mgimwa ni zao la CCM ambalo limeandaliwa kwani ndiyo kazi yao kutengeneza viongozi bora.
Mhagama alisema kuwa kiongozi bora anatoka CCM na kazi ya wapinzani ni kuchukua watu ambao uwezo wao umeshakuwa mdogo hivyo kushindwa kuwajibika hali ambayo haitawaletea maendeleo wananchi.
Aliwataka wananchi kuiunga mkono CCM na kuachana na vyama vya upinzani ambavyo havina sera za kuwaletea maendeleo wananchi badala yake ni kuwagawa na kuendeleza malumbano ambayo hayana faida kwa wananchi.
Naye mkazi wa Mafinga Edina Peter alisema kuwa wao wanataka kiongozi ambaye atawasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi na Mgimwa ni moja ya viongozi bora ambao wanajali maslahi ya wananchi.
Mwisho.
    
  

   

WODI YA WAZAZI MAFINGA YAHITAJI MAMILIONI YA FEDHA KWA AJILI YA VIFAA VYA UPASUAJI

Na John Gagarini, Mafinga
HOSPITALI ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa inahitaji kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa vya upasuaji kwenye wodi ya wazazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Mafinga Dk Innocent Mhagama alisema kuwa fedha hizo ni pamoja na ukarabati wa chumba cha upasuaji kwenye wodi hiyo.
Dk Mhagama alisema kuwa jengo hilo la wodi ya wazazi limekamilika na linatumika lakini halina huduma ya upasuaji kwa wanawake wajawazito.
Alisema kuwa wanafanya mipango mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha hizo ili kutoa huduma bora za idi ya hapo kwani matatizo yote yatakuwa yakitatuliwa ndani ya jengo hilo pasipo kumhamisha mgonjwa.
“Wodi hii iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 320 imekamilika tangu mwaka jana na inatoa huduma zote isipokuwa upasuaji ambapo kwa sasa tunatafuta fedha hizo ili kuwe na huduma hiyo,” alisema Dk Mhagama.   
 Alisema kuwa kukamilika kwa wodi hiyo kumepunguza tatizo la akinamama kutopata huduma bora lakini sasa huduma zimeboreka.
“Wodi ya awali ilikuwa na uwezo wa kuzalisha akinamama wawili au watatu lakini kwa sasa wanazalisha akinamama nane kwa wakati mmoja ambapo inauwezo wa kulaza akinamama 60 toka 20 kwa  wakati mmoja ambapo wanaojifungua kwa siku ni kati ya 18 na 20 na wanaofanyiwa operesheni kwa siku ni kati ya wanne hadi sita,” alisema Dk Mhagama.
Moja akinamama wanaotumia wodi hiyo Blandina Mpyanga alisem akuwa wanaishukuru serikali na wadau mbalimbali waliofanikisha ujenzi huo.
Mpyanga alisema kuwa kwa kipindi cha nyuma wakinamama wajawazito walikuwa wakilala wanne kwenye kitanda kimoja lakini kwa sasa kila mgonjwa na kitanda chake.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
KATIKA kukabiliana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito pamoja na kuozwa katika umri mdogo Jimbo la Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa imewekwa mikakati ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi kwa shule za sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari mbunge wa Jimbo hilo ambaye anatetea kiti hicho Mahmoud Mgimwa alisema kuwa ujenzi huo ni kwa ajili ya shule zote za kata na zingine ili kukabiliana na changamoto hizo.
Mgimwa ambaye ni Naibu waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa hadi sasa shule ya sekondari ya Isalavanu tayari imekamilika huku ile ya Kibengu ikiwa ujenzi unaendelea.
“Hii ni moja ya mikakati ambayo nimeiweka kama kipaumbele cha utekelezaji wa ilani ya chama ambapo nimechangia hosteli hizo bati 170 na vifaa mbalimbali katika kukamilisha ujenzi huo,” alisema Mgimwa.
Alisema kuwa endapo kila kata itakuwa na hosteli ni dhahiri tatizo la mimba na wanafunzi kuozwa wakiwa bado wanafunzi litapungua au kwisha kabisa.
“Unajua wanafunzi wa kike wanachangamoto kubwa kwani baadhi ya watu wamekuwa wakiwarubuni kutokana na mazingira wanayoishi hasa kutokana na umbali wa shule wanazosoma lakini wakijengewa mabweni itawasaidia,” alisema Mgimwa.
Mmoja ya wakazi wa Mji wa Mfainga Anna Karoli alisema kuwa mpango huo ni mzuri na utasaidia kuwanusuru wanafunzi wanaopewa mimba na kuozwa.
Karoli alisema wanafunzi wa kike wakikaa shule itawasaidia kujiepusha na vishawishi mbalimbali mara watokapo au kwenda shule.
Moja ya wanafunzi wa kike Anita Michael ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya JJ Mungai alisema kuwa mpango huo ni mzuri na utawasadia wanafunzi wa kike kukabiliana na changamoto hizo.
Anita alisema kuwa baadhi ya changamoto wanazozipata ni kurubuniwa na baadhi ya watu wakiwemo madereva wa bodaboda ambao wamekuwa wakiwadanganya kwa kuwapa lifti wakati wakwenda shule.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
WATUMISHI wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kuacha kujihusisha na mambo ya siasa ili kutozorotesha utoaji huduma kwenye sehemu zao za kazi.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaib Nnunduma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Mafinga na kusema kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Nnunduma alisema kuwa kama mtumishi anataka kujihusisha na sisa kuna taratibu ambazo anatakiwa afuate lakini si kufanya siasa akiwa kazini.
“Kufanya siasa ofisini ni kosa kisheria na mtumishi ambaye anafanya hivyo ni kinyume cha sheria za kazi hivyo hawapaswi kufanya hivyo kwani ni kukwamisha utendaji kazi,” alisema Nnunduma.
Alisema kuwa endapo mtumishi anabainika kujihusisha na siasa kazini sheria inambana na anaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
“Kila mtu kuna chama anachokipenda lakini huwezi kuonyesha itikadi zako za chama ofisini kwani kuna baadhi ya watu utawabagua kutokana na vyama vyao hivyo hilo ni kosa kisheria,” alisema Nnunduma.
Aidha alisema kuwa ataandaa mkutano na watumishi wote wa Halmashauri ili kuwajulisha kujiepusha na siasa kazini ambapo wakuu wa shule za sekondari alishaongea nao juu ya kujiepusha na siasa shuleni.
Mwisho.


MWANAFUNZI AJERUHIWA KWA KIPIGO CHA MWALIMU

Na John Gagarini, Mafinga
MWANAFUNZI wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya JJ Mungai Octavian Luoga (20) amejeruhiwa kichwani kwa kupigwa fimbo na mwalimu wake kwa tuhuma za kushindwa kuingia darasani.
Akizungumza jana mjini Mafinga na waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye Hospitali ya Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa alipotoka kupatiwa matibabu mwanafunzi huyo alisema kuwa mbali ya kupigwa na fimbo kichwani pia alipigwa makofi na mateke.
Luoga alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi Septemba  Mosi akiwa bwenini amepumzika kutokana na kuumwa na mishipa ya kichwa huku akiwa na wenzake wawili Wilson Due na Nsajigwa Moses ambao wote walikuwa wakiumwa jambo lililomfanya ashindwe kuingia darasani.
“Walimu wawili walikuja na kunitaka niende ofisini kwa ajili ya kupewa adhabu nikawaambia mimi naumwa ndiyo sababu ya kushindwa kuingia darasani mara wakaanza kunipiga nikawaambia nuamwa naomba mnisikilize wakakataa wakasema nimewajibu vibaya,” alisema Luoga.
Alisema kuwa kutokana na kipigo hicho ikabidi aende ofisini na kufika kule akaanza kupigwa makofi,mateke na fimbo maeneo mbalimbali ya mwili na mwalimu mkuu msaidizi Huruma Nyalusi akidai kuwa nawadharau walimu.
“Mwalimu alinipiga fimbo kichwani na damu zikaanza kunitoka hata hivyo hawakutaka kunipeleka hospitali ndipo wanafunzi wengine wakalazimisha nipelekwe ambapo tulienda polisi na baadaye hospitali kwa ajili ya matibabu nikashonwa nyuzi kadhaa,” alisema Luoga.
Aidha alisema kuwa walimu na wanafunzi wanafahamu matatizo yake na wiki moja iliyopita alilazwa kutokana na tatizo lake hilo hilo hali ambayo ilimfanya ashindwe kuingia darasani ambapo hata mahudhuria yake darasani ni mazuri lakini huwa anashindwa kuingia darasani kutokana na kuumwa kwake.
Baadhi ya wanafunzi walisema kuwa baadhi ya walimu wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kupiga wanafunzi kupita kiasi huku wakati mwingine wakiwapiga ngumi, makofi, vichwa mateke na kuwachapa fimbo zisizo na idadi.
Jitihahada za kumpata mwalimu Nyalusi aliyehusika na tukio hilo hazikuweza kufanikiwa kwani alikuwa akihojiwa kwenye kituo cha polisi cha Mafinga kuhusiana na tukio hilo baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kuandamana kwenda polisi kulalamika.
Hata hivyo  jitihada za kumpata mwalimu mkuu wa shule hiyo Mariano Mwanyingu hazikuweza kufanikiwa kwani hakuwepo shuleni hapo kwani aliondoka kabla ya tukio hilo kutokea na haifahamiki atarudi baada ya muda gani.
Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Mufindi Ambwene Mwanyasi alikiri kupokelewa kwa mwalimu huyo ambaye alihusika na tukio hilo kwa ajili ya kuhojiwa.
Mwisho.
MWANAFUNZI wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya JJ Mungai iliyopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa  Octavian Luoga (20) amejeruhiwa kichwani kwa kupigwa fimbo na mwalimu wake kwa tuhuma za kushindwa kuingia darasani.
Akizungumza jana mjini Mafinga na waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye Hospitali ya Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa alipotoka kupatiwa matibabu mwanafunzi huyo amesema kuwa mbali ya kupigwa na fimbo kichwani pia alipigwa makofi na mateke.
Luoga amesema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi Septemba  Mosi akiwa bwenini amepumzika kutokana na kuumwa na mishipa ya kichwa huku akiwa na wenzake wawili Wilson Due na Nsajigwa Moses ambao wote walikuwa wakiumwa jambo lililomfanya ashindwe kuingia darasani.
Amesema kuwa walimu wawili walikwenda na kumtaka aende ofisini kwa ajili ya kupewa adhabu kwani hakwenda darasani akawaambia anaumwa ndiyo sababu ya kushindwa kuingia darasani mara wakaanza kumpiga licha ya kuwaomba wamsikilize wakakataa wakasema amewajibu vibaya.
Amesema kuwa kutokana na kipigo hicho ikabidi aende ofisini na kufika kule akaanza kupigwa makofi,mateke na fimbo maeneo mbalimbali ya mwili na mwalimu mkuu msaidizi Huruma Nyalusi akidai kuwa nawadharau walimu.
Aidha amesema kuwa mwalimu alimpiga fimbo kichwani na damu zikaanza kumtoka hata hivyo hawakutaka kumpeleka hospitali ndipo wanafunzi wengine wakalazimisha apelekwe ambapo walienda polisi na baadaye hospitali kwa ajili ya matibabu nikashonwa nyuzi kadhaa.
Amesema kuwa walimu na wanafunzi wanafahamu matatizo yake na wiki moja iliyopita alilazwa kutokana na tatizo lake hilo hilo hali ambayo ilimfanya ashindwe kuingia darasani ambapo hata mahudhuria yake darasani ni mazuri lakini huwa anashindwa kuingia darasani kutokana na kuumwa kwake.
Baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa baadhi ya walimu wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kupiga wanafunzi kupita kiasi huku wakati mwingine wakiwapiga ngumi, makofi, vichwa mateke na kuwachapa fimbo zisizo na idadi.
Jitihahada za kumpata mwalimu Nyalusi aliyehusika na tukio hilo hazikuweza kufanikiwa kwani alikuwa akihojiwa kwenye kituo cha polisi cha Mafinga kuhusiana na tukio hilo baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kuandamana kwenda polisi kulalamika.
Hata hivyo  jitihada za kumpata mwalimu mkuu wa shule hiyo Mariano Mwanyingu hazikuweza kufanikiwa kwani hakuwepo shuleni hapo kwani aliondoka kabla ya tukio hilo kutokea na haifahamiki atarudi baada ya muda gani.
Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Mufindi Ambwene Mwanyasi alikiri kupokelewa kwa mwalimu huyo ambaye alihusika na tukio hilo kwa ajili ya kuhojiwa.