Tuesday, January 6, 2026

KIDULI FC YAJIPANGA KUPINDUA MATOKEO ILI KUTWAA UBINGWA WA MKOA WA PWANI

TIMU ya Soka ya Kiduli Fc ya Kibaha licha ya kupoteza mchezo wa fainali ya kwanza dhidi ya Bagamoyo Sugar ya Bagamoyo kwa 1-0 imejipanga kupindua matokeo ili kutwaa ubingwa wa mkoa wa Pwani.

Kiduli inatarajia kucheza mchezo wa marudiano Januari 12 kwenye uwanja wa Mwendapole na mshindi wa jumla ndiye atakayekuwa bingwa wa ligi daraja la Tatu mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa timu hiyo Ally Masimike amesema wamepoteza mchezo huo kwa bahati mbaya.

Masimike amesema kuwa watarudi kwenye uwanja wa mazoezi na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wao wa kwanza.

"Lengo letu ni kupambana na kuhakikisha tunashinda ili kuwa mabingwa na kuuwakilisha Mkoa wetu kwenye michuano ya Mabingwa wa Mikoa,"amesema Masimike.

Bagamoyo Sugar iliifunga Kiduli Fc kwa goli 1-0 kwenye mchezo wa fainali ya kwanza kwenye uwanja wa Mwendapole Kibaha huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kupigwa kwenye uwanja huo huo ikiwa ni fainali ya pili ili kupata bingwa wa Mkoa.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Nasoro Mbilinyi amesema kuwa ligi hiyo ilikuwa ni kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20.


Mbilinyi amewataka wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kwenye fainali hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza.


Bingwa wa ligi hiyo atapata kombe na atawakilisha Mkoa wa Pwani kwenye mashindano ya ligi ya Mabingwa wa mikoa.

No comments:

Post a Comment