Friday, January 23, 2026

AJIPATIA KIPATO KUPITIA PANYA WEUPE

VIJANA Mkoani Pwani wameshauriwa kuchangamkia mradi wa ufugaji panya weupe ambao ni chanzo cha mapato ambapo mmoja huuzwa kati ya shilingi 3,000 hadi 5,000 kwa panya mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Mtaalamu wa Mifugo na Kilimo Rodney Mwasha amesema kuwa ufugaji wa panya hao hauna gharama kubwa.

Mwasha amesema kuwa panya hao ambao asili yao ni kutoka Japan wanatumika mashuleni kwa ajili ya mafunzo kwa wanafunzi mashuleni kwa somo la Bailojia.

"Panya hawa ni rahisi kuwafuga na hawana usumbufu na hata kuwahudumia ni rahisi kwani ni rafiki na siyo wakorofi na hawakufanyi kushindwa kufanya shughuli nyingine,"amesema Mwasha.

Amesema kuwa mradi huo ni mzuri na hautumii gharama kubwa za uzalishaji ambapo panya mmoja anauwezo wa kuzaa watoto nane hadi 10 kwa wakati mmoja na huzaa kila mwezi.

"Mimi nafuga kuku wa kienyeji, bata bukini, bata mzinga, nyuki na upande wa kilimo nalima mbogamboga na kuzalisha uyoga hivyo ufugaji wa panya nao ni sehemu ya kuongeza kipato,"amesema Mwasha.

Aidha amesema kuwa mahitaji ya panya kwa mashule ni kubwa sana hivyo vijana watumie fursa hiyo ili waweze kuongeza kipato chao na familia zao.

"Changamoto ya hawa panya ni nyoka ambao hupenda sana kula panya hivyo endapo hujaimarisha banda wanaweza kuliwa na changamoto nyingine ni maradhi,"amesema Mwasha.

Aliongeza kuwa panya hao chakula chao ni pumba, nafaka kama vile mahindi mtama na dagaa ambapo panya 300 gharama za kuwalisha ni kama 100,000 na faida ni kama milioni 1.5.

"Panya hawa wana uwezo wa kuishi miaka miwili na yeye alianza kwa kufuga panya wanne na sasa ana panya 300 hadi 400 ambapo soko lake huwa kipindi cha katikati ya mwaka,"amesema Mwasha.

No comments:

Post a Comment