Diwani wa Kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mradi huo Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kwa Manispaa ya Kibaha.
Lutambi amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu sana kwani itaufungua Mji wa Maili Moja pia itafungua uchumi wa wakazi wa Kata hiyo kuondoa changamoto ya ubovu wa barabara.
"Ninachowaomba wananchi kutoa ushirikiano ili ujenzi usiwe na changamoto kwani kwa sasa hichi ndiyo kipaumbele cha Kata yetu kwa mwaka huu lazima lami ijengwe ikiwa ni awamu ya kwanza,"amesema Lutambi.
Amesema ni mradi muhimu sana kwani utafungua fursa nyingi za kiuchumi na kurahisisha usafiri kuwa wa haraka na usafirishaji na Mji utajengeka na kuleta maendeleo kwenye Mitaa ya Uyaoni, Maili Moja Shule na Muheza.
Naye Salum Mizoka Mthamini wa mradi kutoka Kampuni ya Botek ambaye ni Mkandarasi mshauri kwa kushirikiana na Kampuni ya Uress amesema zoezi hilo linakwenda vizuri.
Mizoka amesema kuwa uthamini unaofanyika ni kujua kila mlengwa anadai na atalipwa nini na baada ya hapo malipo yatafanyika kwa wahusika ambao wameshatambuliwa kwenye barabara hiyo kwa awamu ya kwanza ikianza na kilometa 4.
Amesema kuwa lengo la kufanya tathmini ni kuhakikisha kila mtu anayepitiwa na mradi huo ambapo sehemu za nyumba au baraza zinataguswa watalipwa fidia.
"Tunataka kusiwe na migogoro wakati wa utekelezaji wa mradi ili ujenzi ufanyike bila ya manunguniko kwani walengwa watalipwa stahiki zao bila ya tatizo lolote,"amesema Mizoka.
Aidha amesema kuwa malipo hayo yanafanywa kulingana na hali ya soko kwa sasa na hadi wakati huu hakuna changamoto na zilizopo ni ndogo ndogo.

No comments:
Post a Comment