MITI 6,379 itapandwa Mkoani Pwani katika kuadhimisha siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu Abubakar Kunenge amesema zoezi hilo litafanyika kesho huko Wilayani Rufiji.
Kunenge amesema kuwa zoezi la upandaji wa miti hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais katika kulinda na kutunza mazingira hapa nchini ili kukabili mabadiliko ya Tabianchi.
"Zoezi hilo litahusisha upandaji wa miti ya matunda 671 pamoja na miti 5,708 ya mbao na vivuli, ambayo itapandwa katika maeneo ya shule ili kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutunza mazingira,"amesema Kunenge.
Amesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa Mkoa wa Pwani wa kupanda jumla ya miti milioni 13.5 wakati wa mvua za masika pamoja na ugawaji wa miche ya mikorosho milioni 1.5 kwa wakulima wa Wilaya ya Rufiji chini ya kauli mbiu “Uzalendo ni Kutunza Mazingira – Shiriki Kupanda Miti.”

No comments:
Post a Comment