Thursday, January 29, 2026

SIKU 100 ZA RAIS DK SAMIA SULUHU HASSAN MIRADI YA MAENDELEO


KATA ya Visiga Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inaendelea na mchakato wa kuibadilisha Zahanati ya Visiga kuwa kituo cha afya ambapo imepokea kiasi cha shilingi milioni 57 kwa ajili hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha kawaida cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Visiga pia kuelezea yaliyofanyika kipindi cha siku 100 za Rais Dk Samia Suluhu Hassan Diwani wa Kata hiyo Mohamed Mpaki alisema kuwa baadhi ya kero za wananchi wa Kata hiyo zimetatuliwa.

Mpaki alisema kuwa fedha hizo zilizotolewa kwenye Zahanati hiyo ya Visiga zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ambayo yamekuwa na mchango mkubwa wa kuleta maendeleo kwenye Kata hiyo ambayo ina wakazi zaidi ya 17,000.

Alisema kuwa mbali ya Zahanati hiyo kupokea fedha hizo pia na ile ya Miwaleni zimepatiwa Ultra Sound ili kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa kukabili changamoto za vifaa hivyo kwenye Zahanati hizo.

"Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika kipindi cha siku 100 za Rais hakika Kata yetu inaenda kupiga hatua za kimaendeleo,"alisema Mpaki.

Aidha alisema kuwa pia zimetolewa kiasi cha shilingi milioni 110 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ambapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya vyumba vitano vya madarasa.

"Katika siku 100 za Rais pia tumeweza kuchonga barabara zote za mitaa ya Kata yetu ambapo fedha zilizotengwa ni kiasi cha shilingi milioni 30 na tumepokea makalavati 15 ambapo nane yatatumika kwenye eneo la Gaza ambako kuna changamoto kubwa,"alisema Mpaki.

Aliongeza kuwa pia wameweza kukusanya kiasi cha shilingi milioni 128 kutoka vyanzo mbalimbali kwenye Kata hiyo na inatokana na ufuatiliaji mzuri wa vyanzo hivyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Visiga Rashid Kibiriti alisema kuwa itekelezaji wa ilani unafanyika vizuri ikiwa ni pamoja na kupokea madawati 20 kwenye Shule ya Msingi Juhudi awamu ya kwanza.

Kibiriti alisema kuwa changamoto ya maji imeanza kutatuliwa kwenye Mitaa ya Saeni na Visiga Kati mabomba yamepelekwa hivyo baada ya muda maji yataanza kupatikana na wananchi kufurahia huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment