Tuesday, January 27, 2026

WANASIASA WANAWAKE WATAKIWA KUJIKITA KWENYE UCHUMI

WANAWAKE wanasiasa Wilayani Kibaha wametakiwa kupambana kukuza uchumi wao ili kukabiliana na changamoto ukatili wa kijinsia wanazozipata kipindi cha kuwania uongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha mgombea Udiwani Kata ya Kibaha kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Hamo Machapula amesema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakikumbana na changamoto hiyo kutokana na kuwa na uchumi duni.

Machapula amesema kuwa ili kupata uongozi kwa mwanamke ni changamoto kubwa sana kutokana na baadhi ya viongozi wanaume kuwakwamisha kutokana na kuwawekea vikwazo.

"Ili tuweze kufanikiwa kupata uongozi lazima tuwe na uchumi imara ili tuweze kufanikiwa lakini uchumi wetu ukiwa chini ni changamoto kuwa viongozi,"amesema Machapula.

Alisema kuwa wanawake wanauwezo mzuri wa kuwa viongozi lakini wanakumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoka kwa viongozi wanaume pale wanapotaka kuwania nafasi za uongozi.

"Ninachowasihi wanawake wenye ndoto za kuwa viongozi ili kukabiliana na vitendo vya ukatili pale wanapowania nafasi za uongozi ni kuwa na uchumi imara ili kukabili vitendo hivyo,"amesema Machapula.

Aidha amesema kuwa uongozi wa vyama unapaswa kuchukua hatua kwa viongozi wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

"Kwanza tunapaswa kutoa taarifa pale tunapokumbana na kadhia hizo badala ya kukaa kimya kwani ukimya wetu utatusababishia madhara makubwa na kufifisha ndoto zetu,"amesema Machapula.

Alibainisha kuwa wanawake ndani ya vyama wajishughulishe na shughuli mbalimbali ili kujiongezea kipato kwani siasa inaendana na uchumi.








No comments:

Post a Comment