Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wamefariki
dunia na wengine 11 wamejeruhiwa kutokana na ajali mbili tofauti zilizotokea mkoani
Pwani.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kamanda wa Polisi mkoani Pwani
Jonathan Shana imesema kuwa matukio hayo yalitokea wilaya za Kisarawe na Bagamoyo.
Kamanda Shana
amesema kuwa tukio la kwanza lilitokea Agosti 10 majira ya saa 11:15 jioni eneo
la Mwambisi wilaya ya Kisarawe basi dogo aina ya Eicher lenye namba za usajili
T192 DDD likitokea Masanga kwenda Buguruni Jijini Dar es Salaam liliacha njia
na kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku 11 wakijeruhiwa.
Amesema kuwa
chanzo cha ajali hiyo ni breki kushindwa kufanya kazi na kusababisha gari hilo
kupoteza mwelekeo na kupinduka na kusababisha kifo cha mwanamke mmoja anayekadiriwa
kuwa na umri wa miaka (60) ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Amebainisha kuwa
majeruhi wawili Fatma Hamis (35) aliyeumia kifuani na John Clement aliyevunjika
mguu wa kulia wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Aidha amesema
kuwa baada ya gari hilo kupinduka liligonga mzinga wa nyuki ambao waliingia kwenye
basi na kujeruhi watu tisa ambao wamelazwa kwenye hospitali ya Kisarawe na dereva
wa gari hilo alikimbia baada ya tukio hilo ambapo jeshi hilo linamtafuta.
Katika tukio
la pili dereva wa pikipiki na abiria wake wamefariki dunia baada ya kugongwa na
gari.
Shana amesema
kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 13 majira ya saa 11:40 jioni ambapo pikipiki
hiyo aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 315 BLM iliyokuwa ikiendeshwa na
Ally Seif (19) mkazi wa Kerege iligongana na gari aina ya Mitsubishi Fuso likitokea
Dar es Salaam kwenda Bagamoyo likiendeshwa na dereva ambaye hakufahamika.
Amebainisha kuwa
chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bodaboda kulipita gari lililokuwa mbele yake
kwa kasi bila ya kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo
hivyo vya dereva na abiria wake Mohamed Rajabu (18) mkazi wa Kerege
Amewataka wamiliki
wa magari kufanya matengenezo ya magari yao pindi yanapokuwa na hitilafu na
madereva wasikubali kuendesha magari mabovu pia wafanye ukaguzi wa kina katika
magari yao kabla ya kuanza safari kwani ubovu wa magari huchangia ajali kwa
kiasi kikubwa.
Mwisho.