Tuesday, July 26, 2016

ZOEZI LA UBOMOAJI LAZUA TAFRANI

     
Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la ubomoaji kwa amri ya Mahakama vibanda vya biashara vilivyopo eneo la mtaa wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani umeingia kwenye mgogoro baada ya familia ya iliyodaiwa kujenga kwenye eneo ambalo si lao wamedai vimebomolewa kimakosa.
Ubomoaji huoa ambao ulifanywa Julai 15 na kampuni ya udalali ya Coast Auction Mart baada ya kesi hiyo ambayo imedumu kwa kipindi cha miaka 35 familia hiyo ya iliyoongozwa na Eva Pwele ambaye alikuwa mlalamikaji bada ya baba yake mzazi Pwele Showe ailiyefungua kesi hiyo kufariki dunia kumlalamikia Tonga Fueta kudai eneo hilo ni mali yake ambapo mahakama ilimpa ushindi.
Akizungumza na mwandishi wa habari mdai Eva Pwele alisema kuwa maamuzi ya mahakama yalikuwa ni  mlalamikiwa kupewa eneo lenye ukubwa wa mita 3 na nchi 7 kwa mita 3 na nchi 5 na si mita 352.92 ikiwa ni maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya Mwanzo Kibaha mwaka 1980.
Pwele alisema kuwa baada ya maamuzi ya mahakama hayo miezi mitatu iliyopita alifuatwa na dalali na kutakiwa avunje mwenyewe lakini yeye hakufanya hivyo na kusema kuwa yeye anachojua ni kumkabidhi eneo lenye ukubwa wa mita 3 na nchi 7 tu na si hadi kwenye eneo walilojenga mabanda hayo ya biashara.
“Cha kushangaza siku ya tukio nililiona watu wakija wakiwa Dalali na kuanza kubomoa mabanda yetu ambayo yalijengwa hivi karibuni baada ya kutokuwa na wasiwasi juu ya eneo hilo kwani mapitio ya hukumu yalisema kuwa katika maamuzi ya mwanzo hayakuonyesha ukubwa wa eneo lakini mapitio hayo ya mwaka 2005 ndiyo yaliyosema kuwa mlalamikiwa alipaswa kurudishiwa sehemu iliyotajwa hapo juu,” alisema Pwele.
Alisema kuwa mbali ya maamuzi kukiukwa pia alishangaa wahusika wa bomoa hiyo kutokuwa na barua yoyote ambayo inawaruhusu kufanya ubomoaji huo ambao umewatia hasara kubwa kutokana na mabanda hayo kuvunjwa kwa madai ya kujengwa kwenye eneo la mlalamikiwa.
Kwa upande wake Tonga Fueta alisema kuwa kwanza anamshukuru Mungu kwani baada ya kuhangaika kwa miaka 35 hatimaye haki yake imepatikana kwani tangu mwanzo wa kesi hiyo ilipofunguliwa na mlalamikaji alikuwa akishinda kuanzia mahakama ya mwanzo hadi mahakama kuu kabla ya kukatiwa rufaa na mlalamikaji baada ya hukumu ya kwanza iliyotolewa na hakimu Chungulu mwaka 1981.
Fueta alisema kuwa alinunua eneo hilo mwaka 1969 kwa kiasi cha shilingi 400 toka kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Ramadhan na mwaka huo huo alimpa sehemu ya eneo hilo Pwele Showe ambaye kwa sasa ni marehemu lakini aliongeza na eneo lake.
“Mwaka 1971 nyumba zetu na mdai wangu zilivunjwa kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro ndipo naye akamfuata Ramadhan ili amuuzie eneo na kumuuzia kwa shilingi 500 na ndipo aliponimbia nivunje banda langu kwakuwa yeye ameshanunua ndipo tatizo hilo lilipoanzia,” alisema Fueta.
Kufuatia bomoabomoa hiyo familia ya Pwele imesema kuwa itatafuta haki yao kwenye vyombo vya kisheria kwani ubomoaji huo umekiuka amri ya mahakama kwa kuvunja sehemu ambayo haihusiki kwani wao walikuwa wakijiandaa kumkabidhi eneo kama ilivyoagizwa na mahakama.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment