Na John Gagarini, Bagamoyo
WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani imebaini uwepo wa
watumishi hewa 83 na kuifanya wilaya hiyo kwa sasa kuwa na watumishi hewa 91 ambapo
wakati zoezi hilo linaanza lilibaini watumishi hewa nane tu.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuzindua madawati
300 yaliyotengenezwa na wadau mbalimbali na kuzinduliwa na mkuu wa mkoa wa
Pwani Injinia Evarist Ndikilo, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema
kuwa watumishi hao wamebainika baada ya kuundwa kikosi kazi kuchunguza
watumishi hao.
Mwanga alisema kuwa awali baada ya agizo
lililotolewa na Rais Dk John Magufuli kulibainika watumishi hewa nane lakini
sasa idadi hiyo imeongezeka baada ya kufanywa kwa kina.
Alisema kuwa kikosi kazi kilichoundwa na watu sita
wanaoundwa na kamati ya ulinzi na usalama na kugundua watumishi hewa wengi ni
kutoka idara ya elimu hasa kwenye shule za msingi na sekondari.
“Watumishi wengi ni walimu ambao wengi wamekwenda
masomoni bila ya kuaga na hawana ruhusa na baadhi walishaacha kazi lakini cha
kushingaza mishahara yao ilikuwa inaingizwa kama kawaida jambo ambalo ni kinyume
cha taratibu,” alisema Mwanga.
Aidha alisema kuwa tatizo kubwa linaonyesha ni
idara ya elimu kushindwa kutoa maamuzi ya haraka mara walimu wanapoomba kwenda
masomoni hivyo huamua kuondoka kienyeji.
“Watumishi wengine walibainika kuwa hawana vielelezo
vyo vyote vya vya juu ya ajira zao na tunaomba hatua kali zichukuliwe kwa
watumishi hao ambao ni hewa na wamekuwa wakilipwa mishahara huku hawafanyi kazi
wanachukua mishahara ya bure,” alisema Mwanga.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia
Evarist Ndikilo alisema kuwa kutokana na kubainika watumishi hao 83 hewa
wilayani Bagamoyo kwa sasa mkoa wamefikia watumishi hewa 272.
Ndikilo alisema kuwa zoezi hilo bado linaendelea na
kukipongeza kikosi kazi cha wilaya hiyo kuweza kuwabaini watumishi hao hewa na
itaendelea kuchunguza hadi kuondoa kabisa suala hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment