Tuesday, July 26, 2016

PWANI YATAKIWA KUMALIZA ZOEZI LA WATUMISHI HEWA


Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki ameutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kuhakikisha unamaliza kushughulikia tatizo la watumishi hewa haraka.
Mkoa huo una jumla ya watumishi hewa 272 ambao wamebainika na kuitia serikali hasara ya shilingi bilioni 1.4 kufuatia zoezi la uhakiki wa watumishi hewa kufanyika kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli.
Kairuki aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa mkutano wake na uongozi wa mkoa huo, wakurugenzi wa Halmashauri na Miji za mkoa huo pamoja na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa ili kujua changamoto zinazowakabili watumishi wa Umma.
Alisema kuwa kwa kuwa tayari agizo la Rais lilishatoka tangu mwezi Machi mwaka huu kinachotakiwa ni kuwachukulia hatua wahusika baada ya kuwabaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili na si kuwaacha tu.
“Rais alitoa maagizo kubainisha watumishi hewa na baada ya kubainika wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwani wamefanya makosa ya kuiibia serikali hivyo hakuna sababu ya kutowachukulia hatua stahiki,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa hatua stahiki zichukuliwe mapema ikiwa ni pamoja na kurekebisha taarifa za watumishi hao ikiwa ni pamoja na kusitisha mishahara yao kabla ya malipo yamwezi Agosti ili tatizo hilo lisije likaendelelea.
“Pia nataka kusiwe na data chafu ambazo Halmashauri ziliweka kwa watumishi hao ambazo ni pamoja na kutopandishwa madaraja, malipo kwa watu ambao wana umri zaidi ya miaka 60 na watumishi kutokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi huku wakiendelea kulipwa,” alisema Kairuki.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa mkoa huo una watumishi 16,156 huku ukiwa na upungufu wa watumishi 3,306 na watumishi hewa waliobainika ni 272 kwenye Halmashauri saba za mkoa huo ambazo ni Kibaha Mjini, Kibaha, Mafia, Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na Bagamoyo.
Ndikilo alisema kuwa mkoa unalishughulikia suala la watumishi hewa ambapo wanashirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kusema kuwa zoezi hilo ni gumu hivyo inabidi walifanye kwa umakini ili lisije likaleta matatizo na watalikamilisha mapema.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment