Tuesday, July 26, 2016

TFS KANDA YA MASHARIKI YAKUSANYA MABILIONI

Na John Gagarini, Kibaha
WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki imefanikiwa kukusanya mapato yenye tahamani ya shilingi bilioni 13 kwa mwaka jana kutokana na tozo mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha meneja wa TFS Kanda ya Mashariki Dk Abel Masota alisema kuwa tozo hizo ni pamoja na faini zinazotokana na ukiukwaji wa taratibu za matumizi ya rasilimali za misitu ya hifadhi.
Dk Abel alisema kuwa mapato hayo ni pamoja na ukataji wa vibali kwa ajili ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu 17 kwenye misitu iliyo chini ya wakala hiyo kwenye kanda yake.
“Mapato hayo ni kwa kipindi cha mwaka uliopita wa 2015 ambapo ni pamoja na leseni za biashara za mazao ya misitu, faini na vibali mbalimbali vya biashara hizo za misitu na tunawataka wafanyabiashara hao wafuate taratibu ili kuinusuru misitu yetu kwa kuvuna kufuatatana na taratibu zilizowekwa,” alisema Dk Abel.
Alisema kuwa katika kuhakikisha misitu inakuwa salama uvunaji wa mazao ya misitu umepangwa kwenye mashamba ya miti ambayo si misitu ya hifadhi bali ni mistu ya wazi ambapo asilimia tano ya mapato hurudi kwenye maeneo ya vijiji kwa ajili ya upandaji miti.
“Tunashirikiana na serikali za vijiji kuhakikisha tano ya mapato zirudi kwa ajili ya upandaji miti kwa lengo la kuwa na sehemu ya uvunaji wa miti kwani kama hakutakuwa na mashamba ya miti ni dhahiri watu wafanyabiashara watakuwa wakivuna kwenye misitu ya hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema Dk Abel.
Alisema kuwa changamoto zinazoikabili wakala ni pamoja na uvamizi wa watu kwenye hifadhi ya misitu, vitendea kazi, kilimo na ufugaji kwenye hifadhi, uchomaji moto na uharibifu mwingine unaofanywa na watu kwenye misitu hiyo ambayo iko kisheria na kuingia humo ni kinyume cha sheria.
Aidha alisema wamekuwa wakifanya doria alkini kutokana na misitu hiyo kuwa mikubwa ni vigumu kuweza kuwadhibiti wahalifu wa misitu ambao wamekuwa wakivizia na kuingia na kufanya uharibifu na Kanda ya Mashariki inaundwa na mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment