Tuesday, July 5, 2016

WATENDAJI WATAKAOSHINDWA KUKAMILISHA ZOEZI LA UPATIKANAJI MADAWATI KUJIFUKUZISHA KAZI

Na John Gagarini, Kibaha

MKUU mpya wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Asumter Mshama ametoa siku 24 kwa watendaji wa kata na maofisa tarafa kuhakikisha wanakamilisha zoezi la upatikanaji wa madawati na atakayeshindwa kukamilisha zoezi hilo kwenye sehemu yake atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Mshama ametoa agizo hilo mjini Kibaha kwenye mkutano alioundaa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na watendaji hao na baadhi ya wakuu wa Idara za Elimu, Ardhi na Mazingira na kusema kuwa watendaji hao wanapaswa kukamilisha zoezi hilo ifikapo Julai 29 mwaka huu.

Amesema kuwa agizo la Rais Dk John Magufuli ilikuwa ni Juni 30 mwaka huu hivyo hakuna sababu ya watedaji hao kushindwa kutekeleza agizo hilo kwani muda uliotolewa ulishapita.

Aidha amesema kuwa Baadhi ya watendaji wamefanikiwa kukamilisha zoezi nawapongeza lakini wengine wameshindwa kukamilisha hivyo anatoa muda hadi Julai 29 wawe wamekamilisha na atakayeshindwa atakuwa kajifukuzisha kazi mwenyewe kwa kushindwa kuwajibika.

Akielezea juu ya uwezekano wa kukamilisha hilo amesema kuwa yeye kule alikotoka wilaya ya Wangingombe mkoani Njombe alipambana na kufanikiwa kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa ambapo madawati yalipatikana na kuwa na ziada ya madawati 2,000 hivyo hata Kibaha hakuna sababu ya kushindwa kufanya hivyo kwani hakuna jambo ambalo linashindikana.

Amesisitiza kuwa Maagizo waliyopewa wao wakuu wa wilaya na Rais ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini kwani haiwezekani nyumbani watoto wakae kwenye makochi au sofa lakini wakifika shule wanakaa chini lazima watendaji hao wahamasishe wananchi kuchangia miundombinu ya elimu.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha amesema kuwa watendaji hao wanapaswa kuwahamasisha wananchi kuchangia unpatikanaji wa madawati hakuna haja ya kusema kuwa eti watu wagumu kuchangia.

Amesisitiza kuwa Kama mtendaji ameshindwa kukamilisha zoei hilo ni kwamba ameshindwa kazi kwani sheria zipo na wanapaswa kuzitumia ili kufanikisha zoezi hilo la upatikaaji wa madawati.

Naye mtendaji wa kata ya Kongowe Said Kayangu alikiri kuwa baadhi ya maeneo zoezi hilo limeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.

Kayangu amesema kuwa watahakikisha muda uliosalia wanakamilisha zoezi hilo na kusema kuwa watajipanga vizuri ili kufanikisha zoezi hilo ili kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli ili kila mtoto aweze kukaa kwenye dawati.

mwisho.



No comments:

Post a Comment