Tuesday, July 5, 2016

CHAURU YAWATAKA WAFUGAJI KUONDOA NGOMBE KWENYE SHAMBA LAO

Na John Gagarini, Bagamoyo

UONGOZI Chama Cha Ushirika wa Wakulima wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) wamewataka wafugaji walioko kwenye shamba hilo kuhamisha mifugo yao ambayo imekuwa ikifanya uharibifu wa mazao pamoja na miundombinu ya umwagiliaji.

Akizungumza kwenye kikao cha wakulima na wafugaji waliopo kwenye shamba hilo ambalo liko kwenye kitongoji cha Msigala Kijiji cha Visezi kata ya Ruvu wilayani Bagamoyo mwenyekiti wa chama hicho Sadala Chacha amesema kuwa uharibifu uliofanywa ni mkubwa sana.

Chacha amesema kuwa kutokana na baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye shamba hilo la umwagiliaji la mpunga kumewasababishia hasara kubwa wanachama wake na uharibifu wa miundombinu.

Amesema kuwa serikali ilishawatengea eneo lao liitwalo Mnyanama lakini hawataki kwenda wakidai kuwa hakuna huduma za kijamii jambo ambalo limewafanya waendelee kukaa hapo na huku mifugo hiyo hasa ngombe wakiendelea kufanya uharibu wa miundombinu na kula mazao ya wakulima.

Aidha amesema kuwa wamekuwa wakikaa vikao vya mara kwa mara ili kujaribu kuangalia utaratibu wa namna ya kufuga na wao kulima lakini wao wamekuwa wakilishia mifugo kwenye mashamba hayo ya wakulima na kusababisha ugomvi mara kwa mara.

Ameongeza kuwa wamechoshwa na vitendo hivyo vya wafugaji vya kuingiza ngombe kwenye shamba hilo huku sheria aikikataza mifugo kuingia kwenye eneo hilo lakini utekelezaji wa suala hilo umekuwa mgumu kwani mifugo bado inaingizwa shambani hapo.

Kwa upande wake mmoja wa wafugaji Lupina Kirayo amesema kuwa tatizo kubwa linatokana na baadhi ya wafugaji wanaoleta mifugo toka maeneo ya mbali kwa ajili ya kwenda kuuza ngombe kwenye mnada wa Ruvu ndiyo wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye shamba hilo la ushirika wakitafuta maji.

Lupina amesema kuwa wao kama wenyeji wa Kitongoji hicho wako makini na mifugo yao ambapo wakati mwingine wachungaji wao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti ngombe na kuingia kwenye shamba hilo ambapo wamekuwa wakiwafukuza wachungaji wazembe ili kuondoa migongano na kuomba radhi na kutaka kuwe na maridhiano na kuangalia njia nzuri ya kudhibiti mifugo isiingie kwenye shamba hilo lakini siyo kuwaondoa hapo.

Naye mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Msigala Otiniel Mbura amekiri kutokea changamoto ya ngombe kuingizwa kwenye shamba hilo na kusema kuwa ili kuondoa tatizo hilo ni wafugaji hao kuondoa mifugo hiyo na kuipeleka kule walikopangiwa.

Mbura amesema kuwa wafugaji hao hawataki kwenda huko kwa madai kuwa hakuna huduma za kijamii kama zahanati, shule na malambo ya maji kwa ajili ya mifugo yao hali ambayo imefanya ugomvi kwenye shamba hilo kutokwisha kwa muda mrefu sasa.

Shamba hilo la umwagiliaji mpunga lilianzishwa miaka ya 60 na lina wanachama wapatao 894 na lina ukubwa wa hekta 3,209 huku za makazi zikiwa hekta 720 ambapo baada ya mavuno ya mpunga wanachama hulima mazao mengine kama vile mahindi,ufuta na mtama pamoja na kilimo cha mbogamboga.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment