Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist
Ndikilo Ndikilo amesema kuwa kuanzia sasa hataki kusikia Halmashauri za Miji au
wilaya za mkoa huo kuwa zimepata hati chafu.
Sambamba na hilo amezitaka
Halmashauri hizo kuwatumia wakaguzi wa hesabu wa ndani ili kuweka mambo yao
katika mpangilio mzuri ili kuondokana na hati chafu ambazo zimekuwa
zikiziandama baadhi ya Halmashauri hizo.
Ndikilo aliyasema hayo wakati wa
kikao na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji za Mikoa hiyo ambao
waliapishwa hivi karibuni baada ya kuteuliwa na Rais Dk John Magufuli.
Alisema kuwa taarifa za hesabu za
kila Halmashauri zinapaswa kupelekwa kwa wakati kulingana na utartibu uliowekwa
na serikali pia hoja za mkaguzi mkuu wa serikali (CAG) zijibiwe mapema.
“Kuanzia sasa sitaki kusikia
Halmashauri imepata hati chafu kutokana na uzembe kwani wakati mwingine
inatokana na kushindwa kuonyesha risiti ambazo ni za manunuzi jambo ambalo liko
ndani ya uwezo wenu hakuna sababu ya kuharibu sifa za utendaji kazi wenu kwa
mambo madogomadogo,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa jambo jingine
ambalo wakurugenzi wa halmashauri tisa za mkoa huo wanapaswa kulizingatia ni
kutekeleza miradi kwa thamani halisi ya fedha na si kutekeleza miradi hiyo
chini ya kiwango.
“Mnapaswa kutekeleza miradi ya
maendeleo ya wananchi kwa wakati na kama mnaona kuna mtendaji ambaye anafanya
vibaya hakuna sababu ya kumuonea haya dawa ni kumwondoa,” alisema Ndikilo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani alisema
kuwa wakurugenzi hao wanapaswa kukuisanya mapato kwa nguvu kwani makusanyo
makubwa ndiyo yatakayoifanya Halmashauri kuweza kuendesha shughuli zake ikiwa
ni pamoja na kuchangia uchumi wa wananchi na Taifa.
“Watu wanaohusika na vyanzo vya
mapato wanapaswa kuwa wabunifu wa kuanzisha vyanzo vipya na siyo kuwa na vyanzo
vilevile miaka yote pia wavifanyie uchambuzi ili kutokusanya mapato chini
kutokana na taarifa za wazabuni ambao wamekuwa wakiidanganya Halmashauri juu ya
mapato huku mengine yakiingia mifukoni mwao,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake mkurugenziwa
Halmashauri ya Mji wa Kibaha Jenifa Omolo alisema kuwa amejipanga vyema
kutekeleza majukumu ya serikali kama walivyokula kiapo ili kuboresha utoaji
huduma kwa wananchi pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Naye Tatu Seleman mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha alisema kuwa atahakikisha
anashirikiana na wananchi katika kutekeleza majukumu ya Halmashauri kwani
ushirikishwaji utasaidia kupatikana kwa maendeleo hasa kupitia kwenye huduma za
kiajamii.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment