Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani
Asumter Mshama amesikitishwa na mapato yanayokusanywa kama ushuru ya shilingi
milioni 1.5 kwa mwezi kwenye soko kuu la Maili Moja kuwa ni madogo sana
ikilinganishwa na idadi ya wafanyabiashara sokoni hapo.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
mjini Kibaha wakati alipofanya mkutano na wafanyabiashara wa soko hilo kujua
changamoto zinazowakabili na kusema kuwa mapato hayo ni madogo sana na
Halmashauri hiyo inapaswa kuangalia namna ya ukusanyaji mapato hayo ili
yaendanena na hali halisi.
Mshama alisema kuwa soko hilo ni
chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri lakini ukusanyaji huo unakatisha tamaa
kwani inaonekana kuna fedha hazifiki hivyo kuna haja ya suala hilo kufanyiwa
kazi ili mapato halali yaweze kuonekana.
“Kiasi kilichotajwa cha shilingi
milioni 1.5 kwa mwezi hakikubaliki vinginevyo tutafanya uhakiki wa
wafanyabiashara wote kwa kupitia kibanda kwa kibanda ili tuweze kujiridhisha
juu ya usahihi wa mapato sokoni hapo ambapo ushuru ni shilingi 300 kwa siku kwa
kila mfanyabiashara ambapo kuna wafanyabiashara zaidi ya 500,” alisema Mshama.
Alisema kuwa kama ni mgodi soko hilo
ndiyo mgodi wa kuchimbwa hivyo lazima makusanyo yake yafanywe kwa usahihi ili
kutopoteza fedha kwenda kwenye mifuko ya watu binafsi.
“Makusanyo kama haya haiwezekani kwa
soko hili hapa kuna tatizo lazima tupate ukweli kwani hili halikubaliki au
mmeshindwa kukusanya kama tunakuja hapa kudaili milioni moja nadhani hata hichi
kikao hakina maana ni bora tuondoke tukaendelee na shughuli nyingine,” alisema
Mshama.
Akizungumzia juu ya Halmashauri
kujitoa kuweka ulinzi alisema kuwa hilo ni kosa lazima ulinzi uwe chini ya
Halmashauri na si kuwatwika mzigo wafanyabiashara mzigo huo kwani huduma hiyo
ni faida kwa Halamshauri hivyo hakuna sababu ya wao kulinda wenyewe.
“Inashangaza kuona kuwa eti sehemu
inayotuingizia mapato hatuiwekei ulinzi mbona pale ofisini mmeweka walinzi tena
wa kampuni na hapa lazima mlinde hamna hoja katika hili ninachotaka jukumu hili
mlichukue kama mlivyokuwa mkifanya zamani kama hamna fedha chukueni hizo
mnazokusanya hapo za ushuru mlipe walinzi hili halina mjadala,” alisema Mshama.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi Lucy
Kimoi alisema kuwa juu ya ulinzi ni utaratibu uliowekwa na Halmashauri
kuwaondoa vibarua wote hali iliyosababisha na walinzi ambao walikuwa vibarua
kuondolewa hivyo kukodisha kampuni ya ulinzi kulinda ofisi ya Halmashauri na
sokoni jukumu hilo likaudi kwa wafanyabiashara.
Kimoi alisema kuwa hiyo ni sheria ya
kuwaondoa vibarua ikiwa ni utaratibu wa serikali ndiyo sababu ya kulirudisha
suala hilo kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambao walikuwa wakichanga fedha kwa
ajili ya ulinzi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment