Na John Gagarini, Kibaha
UONGOZI wa zamani wa soko la mkoa la
Maili Moja wamegoma kuwakabidhi ofisi uongozi mpya uliochaguliwa mbele ya mkuu
wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama wakidai kuwa taratibu za uchaguzi huo
zilikiukwa.
Makabidhiano ya ofisi ambayo yalikuwa
yakisimamiwa na diwani wa kata ya Maili Moja Theodory Joseph, ofisa mtendaji wa
mtaa wa Maili Moja John Dotto, mwenyekiti mpya wa soko Ramadhan Maulid na
katibu Elias Kisandu yalishindikana kutokana na uongozi wa zamani kutoridhia
jinsi walivyoondolewa madarakani
Akizungumza baada ya makabidhiano ya
soko hilo kushindikana katibu wa zamani wa soko hilo Muhsin Yusuph alisema kuwa
hawawezi kukabidhi mali za soko hilo bila ya taratibu kwani soko hilo lilikuwa
liko kwenye mfumo wa ushirika.
Yusuph alisema kuwa taratibu za
ushirika zinafahamika hivyo sisi hatuwezi kuwakabidhi uongozi mpya bila ya
taratibu ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi chini ya mrajisi wa vyama vya
ushirika.
“Huu ni ushirika na ushirika una
taratibu zake sasa sisi hatuwezi kuukabidhi uongozi mpya bila ya kufuata
utaratibu kwani uchaguzi haukufanyika kwa kufuata katiba ya ushirika ambapo
mrajisi ndiye aliyetakiwa kuwa msimamizi,” alisema Yusuph.
Alisema kuwa siku walipochaguliwa
viongozi wapya ilikuwa ni mkutano na mkuu wa wilaya kujua changamoto
zinazotukabili lakini haukuwa mkutano wa uchaguzi ambao unakuwa ni maalumu na
unasimamiwa na mrajisi wa vyama vya ushirika.
Mwenyekiti wa kamati ya makabidhiano
diwani Theodory Joseph alisema kuwa wao walikuwa wakikamilisha taratibu kwani
uchaguzi ulifanyika na uongozi huo wa zamani kushindwa na kutakiwa kuwakabidhi
ofisi viongozi wapya.
Joseph alisema kwa kuwa wamekataa
watawasiliana na ngazi zinazohusiaka kwa taratibu zaidi lakini wao hawana la
zaidi kwani kila kitu kilikuwa kinajulikana hivyo watasubiri taratibu zingine.
Kwa upande wake mwenyekiti mpya
Ramadhan Maulid alisema kuwa kwa kuwa uongozi uliopita umegoma kukabidhi ofisi
watawasiliana na mkuu wa wilaya ili kujua nini cha kufanya juu ya hatua hiyo.
Soko hilo lilikuwa likiendeshwa kwa
taratibu za ushirika ambapo kuna zaidi ya wafanyabiashara zaidi ya 500 ambapo
baadhi ni wanachama wa ushirika na wengine si wanachama wa ushirika ambapo mkuu
wa wilaya alishauri ni vema uongozi ukawa tofauti kati ya ule wa ushirika na
soko ili kuondoa muingiliano wa majukumu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment