Tuesday, July 26, 2016

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WATAKIWA KUANDAA DAFTARI LA CHANGAMOTO ZA WANANCHI

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuanzisha daftari maalumu la wakuu wa Idara kwenda kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi Vijijini kila mwezi.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kikao baina yake na wakurugenzi walioteuliwa hivi karibuni na Rais Dk John Magufuli juu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi.
Ndikilo alisema kuwa umefika wakati sasa wa watendaji kwenda kuwatumikia wananchi na si kukaa ofisini wakati wananchi wakiwa na matatizo mengi huku wao wakiwa wamekaa ofisini tu.
“Nataka nione wakurugenzi mkiwa mmetengeneza dafatari hilo ambalo litamwonyesha mkuu wa idara kazi aliyoifanya kwa ajili ya kutatua kero na kule wanako kwenda lazima kuwe na sahihi zao kuwa walifika kwenye vijiji husika ili iwe ushahidi wa utendaji kazi wao na si kukaa tu ofisini,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa sambamba na hilo wakurugenzi lazima watenge siku maalumu ya kusikiliza kero za wananchi na mfumo wa kupata taarifa za matatizo kwa kila kata ili iwe rahisi kufuatilia ikiwa ni pamoja na kuweka sanduku la kero za wananchi ili zishughulikiwe mapema.
“Mnapaswa kushughulikia kero za wananchi kwa wakati kwani ucheleweshaji wa kutatua kero kwa muda muafaka husababisha matatizo kuongezeka na kufanya malalamiko kutoisha ambapo wananchi wamekuwa wakikimbilia kwa wakuu wa wilaya na mkoa huku kukiwa hakuna utatuzi ngazi ya Halmashauri,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa wakurugenzi wanapaswa kusimamia suala la ulinzi na usalama na wasiliache kwa serikali kuu ili wananchi waweze kufanya shughuli zao wakiwa na amani kwani kukiwa na uvunjifu wa amani itakuwa ni vigumu watu kufanya shughuli za maendeleo.
“Changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, migogoro kutoshughulikiwa kwa wakati na mipaka pamoja na changamoto nyingine nyingi ambapo wajibu wa wakurugenzi ni kuwasimamia watendaji mbalimbali na hawapaswi kuwa na urafiki usiokuwa wa maendeleo kwa watendaji,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wakurugenzi hao kuwasimamia watendaji wao ili wasikae ofisini kusubiri maelekezo toka ngazi za juu bali waende kwa wananchi kwani muda huu si wa kukaa bali wanapaswa kuwa wabunifu na si kukaa tu kwani lazima wawe wawajibikaji.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment