Tuesday, July 26, 2016

WATAKA SOKO LIJENGWE JIRANI NA STENDI

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABISHARA wa soko la Maili Moja wilayani Kibaha wamesema kuwa endapo soko lao litahamishwa kutokana na kuwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara na kuhamishiwa eneo la Kitovu cha Mji endapo halitajengwa jirani na stendi hawatakuwa tayari kwenda huko.
Waliyasema hayo wakati wa mkutano wao na mkuu wa Wilaya ya Kibaha Asumter Mshama ambaye alikwenda sokoni hapo kusikiliza changamoto zinazowakabiliwa wafanyabiashara hao ambao wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo ifikapo Septemba mwaka huu.
Aliyekuwa mwenyekiti wa soko hilo Ally Gonzi alisema kuwa tayari wameshaambiwa waondoke hapo lakini wanashindwa kuhama kutokana na Halmashauri kushindwa kujenga soko tangu mwaka 2013 ambapo walidai kuonyeshwa hadi michoro.
“Sisi hatutakuwa tayari kuhamia huko wanakotaka endapo hatawajenga soko letu jirani na stendi kwani vitu hivi vinakwenda kwa pamoja awali ramani ilionyesha kuwa tungekuwa jirani na stendi lakini baadaye tukasikia wanataka kutupeleka eneo la Mnarani maarufu kama Loliondo au Sagulasagula huko stendi ikiwa kitovu cha Mji,” alisema Gonzi.
Alisema kuwa kuwatenganisha kutawafanya wasipate wateja kwani wanunuzi wengi ni wale ambao wanasafiri pamoja na wateja kupata urahisi wa usafiri mara wanaponunua bidhaa ambapo kwa sasa soko lilipo ni jirani na stendi hivyo wanataka viende kwa pamoja.
“Awali Halmashauri walitushirikisha vizuri lakini walipobadili jinsi tutakavyokaa huko hawakutushirikisha lakini sisi tunasema tukitenganishwa hatutakuwa tayari kuhamia huko hivyo katika mipango yao wahakikishe wanatuweka pamoja na stendi ili huduma ziwe bora na sisi tupate wateja,” alisema Gonzi.
Akijibu suala hilo kaimu mkurugenzi Lucy Kimoi alisema kuwa ujenzi wa soko la kisasa unatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka huu ya 2016-2017 na taratibu za ujenzi zitafuatwa ili wafanyabiashara wawe kwenye mpangilio mzuri na wasiwe na wasiwasi.
Kimoi alisema kuwa waliomba mkopo kutoka benki ya uwezeshaji ya TIB kwa ajili ujenzi wa soko na stendi ambapo kwa sasa wanakamilisha kupata vibali toka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kupata fedha za kuanza ujenzi huo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Asumter Mshama aliitaka Halmashauri kuhakikisha inafanya ujenzi huo kwa muda uliopangwa na haitawahamisha wafanyabiashara hao hadi pale soko hilo litakapokuwa limejengwa ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara hao mara zoezi la bomobomoa litakapofanyika.
Mshama alisema kuwa stendi na soko vitakuwa pamoja hivyo wasiwe na wasiwasi kwani taratibu zote zitawekwa vizuri ili waweze kufanya biashara vizuri na kwa utaratibu na wafanyabiashara wote watapata nafasi kwenye soko jipya kwa kuzingatia aina ya biashara.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment