Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist
Ndikilo amesema kuwa mkoa wake unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa magari
hali ambayo inawafanya kuazima magari kwenye wilaya katika shughuli za kikazi
katika mkoa huo.
Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha
wakati wa mkutano wake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na watumishi wa
ofisi ya mkuu wa mkoa na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji za mkoa
huo.
Ndikilo alisema kuwa changamoto hiyo
kwa wataalamu wa mkoa ni kubwa hali ambayo inawafanya wafanye kazi kwenye
mazingira magumu hasa kwenye maeneo ya mbali ikiwa ni pamoja na kwenye
Halmashauri za mkoa huo.
“Waziri mkoa una changamoto kubwa ya
ukosefu wa magari ikiwemo ofisi yangu na wataalamu wangu inapofika hatua ya
kwenda kwenye maeneo ya mbali inakuwa mtihani mkubwa kwani inatubidi tuazime
magari ya kwenye wilaya kwa ajili ya kufika baadhi ya maeneo,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa hata mkuu wa wilaya ya
Kibaha gari alilonalo ni bovu ambapo hivi karibuni alipata ajali ya kuligonga
gari jingine kutokana na breki kugoma naye mkuu wa wilaya ya Mkuranga naye gari
lake siyo zuri sana, wilaya Mpya ya Kibiti yenyewe haina gari kabisa.
“Usafiri kwa mkoa wetu ni changamoto
kubwa hivyo tunaomba mtusaidie ili katika bajeti ijayo mtufikirie kwa kutupatia
usafiri ili tuweze kutekeleza majukumu yetu vizuri ili kukabiliana na
changamoto hii ambayo inatupa wakati mgumu inapofikia suala la usafiri,”
alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine
ni ukomo wa bajeti ambayo kwa mwaka 2014-2015 ulishuka kwa asilimia 40
ikilinganishwa na bajeti iliyopita, fedha za maendeleo kuchelewa, madeni ambayo
yamefikia milioni 152, watumishi kuhama kutafuta maslahi mazuri, vitendea kazi
na upandishwaji wa madaraja.
Akijibu baadhi ya hoja Waziri Kairuki
alisema kuwa Wizara inazifanyia kazi changamoto hizo na pale fedha
zitakapopatikana itaboresha mazingira ya watumishi ili wafanye kazi vizuri
kwani serikali inawathamini wafanyakazi na haitaki wafanye kazi katika
mazingira magumu.
Kairuki alisema kuwa juu ya maofisa
utumishi waliokuwa wakilipa mshahara watumishi hewa itabidi wawajibike ambapo
kwa sasa inawsafuatilia kwani inaonekana nao walichangia kulipa mishahara kwa
watumishi ambao hawakustahili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment