Na John
Gagarini,Bagamoyo
WAFUGAJI
wanaoishi kwenye Kitongoji cha Msigala Kijiji cha Visezi kata ya Ruvu wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani wamepinga kupelekwa Kitongoji cha Mnanyama kutokana na
kutokuwa na huduma za kijamii.
Wakizungumza
na waandishi wa habari Kijijini hapo wamesema kuwa eneo walilopangiwa halina
huduma hizo ndiyo sababu ya wao kuendelea kukaa hapo walipo sasa.
Akizungumzia
juu ya hali hiyo Lupina Kirayo alisema kuwa chanzo cha wao kutakiwa kuondoka ni
kutokana na madai ya wakulima wa shamba la Chama Cha Ushirika wa Umwagiliaji
Ruvu (CHAURU) kuwa ngombe wao wamekuwa wakiingia kwenye mashamba na kuharibu
mazao.
Kirayo alisema
kuwa wao wako hapo kwa muda mrefu lakini wanashangaa kutakiwa kuondoka na
kwenda Mnanyama ambako hakuna huduma hyoyote ya Kijamii.
“Zamani
kijiji hicho kiliweka njia kwa ajili ya ngombe kupita kwenda kunywa maji mtoni
lakini wakulima walifunga njia ya kupita ngombe na ndiyo chanzo cha migogoro ya
wakulima na wafugaji ilipoanza,” alisema Kirayo.
Alisema kuwa
tatizo kubwa linatokana na baadhi ya wafugaji wanaoleta mifugo toka maeneo ya
mbali kwa ajili ya kwenda kuuza ngombe kwenye mnada wa Ruvu ndiyo wamekuwa
wakiingiza mifugo kwenye shamba hilo la ushirika wakitafuta maji.
Aidha alisema
kuwa wao kama wenyeji wa Kitongoji hicho wako makini na mifugo yao ambapo
wakati mwingine wachungaji wao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti ngombe na
kuingia kwenye shamba hilo ambapo wamekuwa wakiwafukuza wachungaji wazembe ili
kuondoa migongano na kuomba radhi na kutaka kuwe na maridhiano na kuangalia
njia nzuri ya kudhibiti mifugo isiingie kwenye shamba hilo lakini siyo
kuwaondoa hapo.
Naye
Elizabeth Meja amesema kuwa yeye alizaliwa hapo na kipindi cha nyuma wamekuwa
wakiishi vizuri lakini kwa sasa wanaambiwa waondoke ambako kule huduma ya afya
hakuna ambapo kwa akinamama hasa pale wanapokuwa wajawazito huhitaji kupata
huduma za mara kwa mara.
Meja alisema
kuwa sehemu wanayotaka kuhamishiwa kuna umbali wa km 20 hadi kufika kwenye
huduma za afya na hata watoto wanapozaliwa hupaswa kupelekwa kliniki lakini
kutokana na umbali huo itakuwa ni matatizo pia watoto wao kwa sasa licha ya
kutumia masaa zaidi ya mawili kwenda shule ni karibu tofauti na wakienda kule
hatapata fursa ya kusoma kutokana na umbali huo.
“Hata suala
la maji ni tatizo kwani hapa tunatumia maji ya shilingi 20,000 kwa siku lakini
kule tunakotakiwa twende maji hakuna kabisa hivyo ni vema wakaweka miundombinu
kwanza ili huduma kama hizo zipatikane,” alisema Meja.
Naye
mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Msigala Otiniel Mbura alisema kuwa tayari
serikali iliamua wafugaji hao kwenda huko ili kuondoa migogoro inayojitokeza
kila wakati.
Mbura alisema
kuwa ni vema wafugaji hao wakenda kwanza na serikali itawapelekea huduma kuliko
hivi sasa wanavyokataa kwenda huko walikopangiwa.
No comments:
Post a Comment