Na John Gagarini, Bagamoyo
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Kikwete
amesema kuwa hakuna kitu kilichokuwa kikimpa wakati mgumu kama kushindwa katika
uongozi wake wa miaka 10 iliyopita.
Aliyasema hayo juzi mjini Bagamoyo wakati wa
sherehe iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA) ya kumkaribisha nyumbani baada ya kukabidhi uongozi kwa mwenyekiti mpya
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli mjini Dodoma hivi karibuni.
Dk Kikwete alisema kuwa hali ya kushindwa ilikuwa
ikimpa wakati mgumu na kujiona kuwa kama endapo angeshindwa basi ange waangusha
Wanabagamoyo na Pwani nzima.
“Kila nilipokuwa nikifikiria kushindwa kwenye jambo
lolote la uongozi wangu kwa nchi au kwenye Chama lakini namshukuru Mungu kwani
tulifanikiwa sana katika suala la maendeleo kwa nchi nzima kwani huwezi
ukapendelea sehemu uliyotoka au ukawanyima maendeleo ni kitu ambacho
hakiwezekani,” alisema Dk Kikwete.
Alisema kuwa wakati fulani alikuwa akilalamikiwa na
baadhi ya wabunge kuwa anapendelea Bagamoyo jambo ambalo si la kweli ambapo
walidai kuwa amehamisha fedha za ujenzi wa barabara na kuzihamishia kwenye
ujenzi wa barabara ya Msata Bagamoyo.
“Hali kama hiyo Ilikuwa inanipa wakati mgumu kwnai
kila sehemu inataka maendeleo na nisingeweza kutofanya maendeleo kwa watu wa
Bagamoyo kwani hata wao wanahitaji maendeleo kama sehemu nyingine,” alisema Dk
Kikwete.
Aidha alisema kuna wakati ilibidi ahamishe fedha
kutoka Bagamoyo na kufanya ujenzi kwenye maeneo ya Geita-Sengerema hadi Usagara
wakati huo waziri wa Ujenzi alikuwa Basil Mramba lakini hawakuliona lakini
anasema alishukuru Mungu kwani ujenzi kwenye barabara hizo ulifanyika vizuri.
“Namshukuru Mungu katika uongozi wangu tulifanya
kazi na kuleta maendeleo makubwa na tumeiacha nchi mahali pazuri na salama
kwnai imetulia licha ya mwaka 2015 wakati wa uchaguzi ambapo baadhi ya watu
walisema kuwa Rais gani hata hafanyi mpango wa kubadilisha katiba ili aendelee
kukaa madarakani kwani watu walishindana lakini hawakupigana wala kumwaga damu
na uchaguzi ulipokwisha maisha yaliendelea salama kabisa,” alisema Dk Kikwete.
Alibainisha kuwa Watanzania wanapaswa kumuombea
Rais Dk John Magufuli ili aweze kuleta maendeleo kwani ni mpenda maendeleo
hivyo lazima asaidiwe aweze kuleta maendeleo ya watu.
Akizungumzia kuhusu Chama alisema kuwa kiko vizuri
na hakuna kinachoiweza CCM kwani anajua hakuna chama cha kuweza kukishinda
kwani havina uwezo ikizingatiwa ni chama kikubwa na viongozi wake ni imara.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya
Bagamoyo Maskuzi alisema kuwa katika uongozi wake alifanikiwa kuleta maendeleo
makubwa kuanzia kwenye elimu na mpango wa shule za kata sasa umeonyesha
mafanikio ambapo shule hizo kwa mwaka huu zimeongoza kwenye matokeo.
Maskuzi alisema kuwa umeme ni moja ya mafanikio
ambapo kwa sasa umefika hadi vijijini kupitia mpango wa Umeme Vijijini REA,
ujenzi wa barabara na masuala mengine ya kimaendeleo kwenye nchi ambayo ni ya
kujivunia.
Katika sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na familia
ya Dk Kikwete alipewa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mifugo kama vile
ngombe, mbuzi, kuku, bata, mavazi ya jadi na vitu mbalimbali ambavyo vilitolewa
na wananchi wa mkoa wa Pwani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment