Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA kuungua bweni la shule ya
sekondari ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kuungua kwa moto baadhi ya
wadau wameanza kuichangia shule hiyo ili kusaidia wanafunzi ambao vifaa vyao
vyote viliungua.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi diwani wa kata ya Bwiringu Lucas Lufunga alisema kuwa kutokana na tukio
hilo waliitisha kikao cha kata kwa ajili ya kuangalia namna ya kuisaidia shule
hiyo.
Lufunga alisema kuwa katika kikao
hicho walifanikiwa kupata kiasi cha shilingi 449,000 na kunua vyakula kwa ajili
ya kusaidia kwani vyakula viliungua na moto huo ambao ulitokea usiku wakati
wanafunzi wakiwa wanjisomea masomo ya usiku.
“Tunaomba watu mbalimbali wajitokeze
kuwasaidia wanafunzi walikuwa wakiishi kwenye bweni hilo kwani kufuatia moto
huo hakuna kilichotoka kwani vyote viliteketea kabisa hivyo kuna haja ya
kulichukulia kwa uzito wake tatizo hilo,” alisema Lufunga.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi mwalimu mkuu wa Shule hiyo Emanuel Kahabi alisema kuwa moto huo ulitokea
wakati wanafunzi hao wakiwa wanajisomea madarasani usiku.
Kahabi alisema kuwa tukio hilo
lilitokea Julai 12 majira ya saa 2:50 usiku ambapo moto huo haukuweza
kufahamika ulitokea wapi na kusababisha hasara kubwa ya bweni hilo na vifaa
mbalimbali vikiwemo vya wanafunzi.
“Bweni hilo ambalo lilikuwa bwalo la
chakula baada ya wanafunzi hao zaidi ya 100 kuhamishiwa humo kutokana na bweni
lao kuungua kwa moto miezi michache iliyopita,” alisema Kahabi.
Alisema kuwa anawashukuru wadau ambao
wameanza kuisaidi shule yake kutokana na moto huo ambao hadi sasa haijafahamika
chanzo chake ni nini na kuwataka watu wakiwemo wakazi wa Chalinze, wilaya na
mkoa amzima kuwasaidia wanafunzi hao.
Mwisho.