Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametaka
kupitiwa upya mkataba wa kuuziwa mwekezaji eneo la Magofu ya Chole wilaya ya
Mafia mkoani Pwani ambapo kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development
Ltd imemilikishwa ambapo eneo hilo kuna gereza walilokuwa wanafungwa watumwa
enzi za ukoloni wakati wa Utawala wa Wajerumani.
Aidha ameunda tume ya kufuatilia undani wa mkataba huo na
amezuia marekebisho yaliyokuwa yanafanywa na kampuni hiyo kwa kipindi cha mwezi
mmoja hadi pale ufumbuzi wa kujua namna mkataba huo ulivyoingiwa baina ya Kijiji
cha Chole na mwekezaji huyo kama umezingatia taratibu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chole Mjini kata ya
Jibondo kwenye mkutano wa hadhara Ndikilo alisema kuwa mkoa hauna nia mbaya na
mwekezaji huyo ambaye amepewa hati miliki ya eneo hilo kwa kipindi cha miaka 33.
Ndikilo alisema kuwa eneo hilo ambalo lina kumbukumbu
mbalimbali ambalo liko jirani na Bahari ya Hindi lilikuwa likitumika kwa ajili
ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na soko la Watumwa pamoja na gereza lina
ukubwa wa hekta 3.7 ambapo eneo hilo liko chini ya Wizara ya maliasili na
Utalii Idara ya Malikale.
“Mkataba huo ambao ulisainiwa mwaka 2007 shamba namba 2031 baina
ya mwekezaji Dk Jean de Villiers na Kijiji
hicho ambapo mwenyekiti wa Kijiji hicho Maburuki Sadiki alisaini kwa niaba ya
Kijiji na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya wakati ule Manzie Mangochi pasipo
kuishirikisha Halmashauri ya wilaya ambayo haipati mapato yoyote kutokana na
uwekezaji huo licha ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi wa Kijiji cha Chole”
alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo amemtaka mwekezaji huyo
kusimamisha ukarabati na kuunda tume ya kufanya uchunguzi na itatoa majibu
baada ya mwezi mmoja ili kujiridhisha na kumilikishwa eneo hilo mtu binafsi
eneo la serikali la kihistoria na kujengwa hoteli ya kitalii kwa kukarabati
jengo la zamani.
Alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ilituma barua
ambayo iliyosainiwa na John Kimaro kwa niaba ya katibu mkuu kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Mafia kuhirikiana na mwekezaji na kusema kuwa sheria ya Mambo ya Kale
ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979 na sera ya Malikale ya mwaka
2008 inasema Malikale au Magofu yanaweza kumilikiwa na mtu binafs, taasisi na
serikali.
Barua hiyo inaendelea kusema kuwa jukumu la serikali (Idara
ya Mambo ya Kale) ni kuhakikisha kuwa mmiliki hatabomoa au kufanya chochote
katika magofu hayo kinyume cha sheria.
Akitoa maelezo juu ya umiliki wake mkurugenzi wa Chole Mjini
Conservation and Development Company Ltd Anne De Villiers amesema kuwa kampuni
hiyo iliingia Mafia na kukuta hali ya majengo hayo ya kale yakiwa kwenye hali
mbaya ndipo walianza mchakato wa kuyakarabati.
Dk Villiers alisema kuwa lengo la kuchukua eneo hilo ni
kuhakikisha uasili wa mahali hapo haupotei kwa kuyafanyia ukarabati magofu hayo
ambapo moja lilibaki ukuta mmoja na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati
huo.
Naye mkuu wa wilaya ya Mafia Dk Nasoro Hamid alisema kuwa
serikali haishirikishwi jambo lolote wala haijui ni watalii wangapi wanaoingia
hapo wala mapato yanayopatikana kwenye eneo hilo.
Dk Hamid amesema kuwa Kijiji cha Chole ndicho kiliingia
mkataba na mwekezaji huyo ambapo hugawana asilimia kutokana na watalii
wanaoingia kwenye eneo hilo la makumbusho lakini tatizo haijulikani
kinachopatikana hapo ni kiasi gani katika mgawanyo huo wa mapato.
Awali baadhi ya wanakijiji wakizungumzia suala hilo wakiongozwa
na Ally Sikubali na Hemed Ally walisema kuwa moja ya changamoto iliyokuwepo ni
mkataba Kiswahili unasema kuwa endapo kutakuwa na kutoeleweka mkataba wa
Kiingereza ndiyo utakaotumika.
Waliomba mkataba huo uangaliwe upya na kufanya marekebisho
ili kila upande unufaike kwani kwa sasa inaonekana kuwa pande nyingine
hazinufaiki na mkataba huo.
Mwisho.