Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na
Watoto Dk Hamis Kigangwala ametoa saa 24 kwa Mkurugenzi wa Shirika la Elimu
Kibaha (KEC) Dk Cyprian Mpemba kuandika barua ya kwa nini asiondolewe kwenye nafasi
hiyo kwa kushindwa kuendesha Hospitali Teule ya Rufaa ya Tumbi iliyopo wilayani
Kibaha mkoani Pwani.
Waziri Dk Simbachawene alitoa agizo hilo huku mkurugenzi huyo
akiwa hayupo na kumwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo Anase Nko
kumfikishia ujumbe huo Dk Mpemba kwa ajili ya kutoa maelezo hayo.
Dk Kigangwala aliyasema hayo jana mara baada ya kutembelea
hospitali hiyo kutokana na kuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kushindwa
kusimamia maslahi ya watumishi ambao wamekosa morali ya kufanya kazi.
Alisema kuwa hali iliyopo kwenye hospitali hiyo ni mbaya sana
na inasikitisha sana huku ofisi ya mkurugenzi ikiwa inatumia fedha ambazo
zingesaidia kuboresha huduma kwenye hospitali hiyo.
“Shirika limeshindwa kuendesha natoa saa 24 hadi leo saa nane
mchana awe ameandika barua ya kujieleza kwanini asiondolewe kwenye nafasi hiyo kwani
ameshindwa kusimamia hospitali hiyo kwani vitu vingi haviko sawa kuanzia
mochwari ambapo imekuwa ikitoa harufu mbaya kutokana na baadhi ya vifaa vya
majokofu kuharibika,” alisema Dk Kigwangala.
“Nataka atoe maelezo yanayojitosheleza kwani inaonekana
hakuna jambo ambalo linaweza kufanyika kwenye hospitali bila ya mkurugenzi
ambapo fedha za hospitali zimekuwa zikitumika kwenye matumizi mengine,” alisema
Dk Kigangwala.
Aidha alisema kuwa mbali ya hivyo pia kuanzia sasa shirika
hilo lisisimamie masuala ya fedha za Hospitali hiyo bali ijisimamie yenyewe ili
kuangalia vipaumbele vinavyohusu hospitali kwani huduma hazisubiri utaratibu.
“Tumeona kuwa tatizo ni utawala ambao unaonekana umeshindwa
kusimamia hospitali nilipokuja nilifikiri tatizo ni meneja wa Huduma za afya Dk
Peter Datani lakini una bahati nilikuja kwa ajili ya kukutimua wewe kumbe wewe
huusiki,” alisema Dk Kigwangwala.
Alibainisha kuwa kuna changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na
chumba cha upasuaji kutokuwa na hadhi kwani ni sawa na stoo, viyoyozi havifanyi
kazi, chumba cha wagonjwa mahututi nacho hakiko sawa na vifaa vinaharibika hakuna
matengenezo hivyo huduma kuwa mbaya.
“Inashangaza kuona kuwa hospitali inakosa vifaa tiba pamoja
na madawa licha ya kuwa inaingiza fedha nyingi kati ya shilingi milioni 120
hadi 150 kwa mwezi lakini inashindwa kujiendesha inashindwa hata kutoa milioni
sita kwa ajili ya kununulia mifuko ya kuhifadhia damu inasikitisha sana
hospitali hii inaendeshwa kiujanja ujanja tu lazima mjiendeshe kwa mikakati
siyo kwenda tu,” alisema Kigwangwala.
Kutokana na hali hiyo ameagiza chumba cha kuhifadhia maiti
cha hospitali hiyo ifungwe na iwe imefanyiwa matengenezo ndani ya siku tatu na
watajua maiti watazipeleka wapi kwani haiwezekani chumba hicho kuwa kwenye hali
hiyo pia miezi mitatu wanatakiwa wawe wamehakikisha maji yanapatikana kwa
kujenga matenki ya kuhifadhia maji.
Alimtaka mkuu wa mkoa kupata ushauri kwa wataalamu ili kuangalia mahusiano baina ya
hospitali hiyo na sekretarieti ya mkoa pia inaonekana ni vema hospitali hiyo
ikasimamiwa na mkoa badala ya shirika.
Alisisitiza kuwa endapo watashindwa kukarabati chumba hicho
cha maiti ndani ya siku tatu atawaondoa kwenye nafasi zao kwani watakuwa
wameshindwa kutekeleza agizo la serikali kwani haiwezekani huduma kutolewa
kwenye mazingira magumu wakati fedha zinapatikana.
Kwa upande wake msajili wa hospitali nchini Dk Pamela Sawa
alisema kuwa walifanya ukaguzi kwenye hospitali mwaka 2010 hadi 2011 ambapo
walikuta hospitali nyingi zina mapungufu mengi mafano hospitali ya Mawenzi
mkoani Kilimanjaro ilikuwa ikitumia chumba cha upasuaji kilichokuwa kikitumika
enzi za mkoloni lakini walibadilisha baada ya kuifunga pia hospitali ya Mbeya
nayo ilikuwa na matatizo ya maji.
Naye Dk Datani alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo
hospitalini hapo ni ukosefu wa fedha kwani waliomba kiasi cha shilingi milioni
600 lakini walipewa kiasi cha milioni sita tu hivyo kujikuta wakiwa kwenye
wakati mgumu wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na kununua vifaa tiba
pamoja na madawa.
Mwisho.