Saturday, May 31, 2014

BILALI AZINDUA MFUKO WA ELIMU ACHANGIA MILIONI 10



Na John Gagarini, Kibaha
MAKAMU wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mohamed Gharib Bilali ameuchangia mfuko wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kiasi cha shilingi milioni 10.
Alichangia fedha hizo jana wakati wa uzinduzi wa mfuko wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani hapa.
Alisema kuwa katika kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwenye sekta ya elimu lazima kuwe mikakati maalumu ya kuweza kufikia malengo kwa kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.
“Nawapongeza kwa kuanzisha mfuko huu na serikali itawaunga mkono kwa hali na mali na mimi nawachangia milioni 10 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto kwenye sekta ya elimu katika mji wa Kibaha wilaya na mkoa mzima wa Pwani.
“Ningependa suala la choo kuwa historia kwani hii ni aibu na si changamoto ya kudumu na inapaswa kufanyiwa kazi mara moja na kuiondoa kabisa kwani ni jambo lisilo pendeza na changamoto nyingine zilizopo kama vile za upungufu wa madawati kwa shule za msingi, ukosefu wa maabara kwa shule za sekondari, upungufu wa nyumba za walimu, matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa na maktaba kupitia mfuko huo utasaidia kukabiliana na hali hiyo,” alisema Dk Bilali.
Aidha alisema kuwa amefurahi kusikia kuwa fedha hizo zitatumika kujenga maabara tatu katika sekondari za Pangani, Visiga na Miembe Saba na kununua madawati 1,500 kwa ajili ya shule za msingi za Tandau, Lulanzi, Misugusugu, Zogowale, Msangani, Viziwaziwa, Vikawe, Mwanalugali, Mkuza na Kidimu.
Alizitaka halmahauri hapa nchini kuiga mfano wa Halmashauri hiyo ya Mji wa Kibaha kwa kuanzisha mifuko kama hii kwa ajili ya kutatua changamoto za elimu badala ya kuisubiri serikali kwani ni mgao inaoutoa ni mdogo na elimu na mafunzo bora ni mkakati wa kipaumbele katika kufikia malengo ya mipango ya maendeleo ya Taifa ya 2025 na kutumia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza umaskini MKUKUTA na malengo ya milenia.
Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Kasimu Majaliwa alisema kuwa ubunifu wa kupata fedha kwa ajili ya Halmashauri 167 hapa nchini ni mzuri kwnai utasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu.
Majaliwa alisema kuwa uboreshaji wa elimu unapaswa kusimamiwa na watu wote wakiongozwa na madiwani na wananchi wote wanapaswa kujitokeza kuuchangia na wizara yake itachangia kiasi cha shilingi milioni tano.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa amefurahishwa na uzinduzi huo ambapo alisema kuwa moja ya ndoto zake za kukabiliana na changamoto za elimu.
“Ili kuwa na elimu bora ni pamoja na kuwa na miundombinu mizuri na watu wa kuiboresha ni wazazi pamoja na wadau wote ndani ya Halmashauri licha ya kuwa wananchi wanachangamoto kubwa ya kuchangia hata hivyo wameonyesha nia ya kuchangia kwa kujitolea na mimi nawaunga mkono kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 16,” alisema Koka.
Awali mwenyekiti wa mfuko huo Anna Bayi alisema kuwa lengo la kuanzishwa mfuko huo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo hadi sasa mfuko huo una kiasi cha shilingi milioni 210 na ahadi ni shilingi milioni 34 huku malengo yakiwa ni kukusanya kiasi cha shilingi milioni 300.
“Tunatarajia kati ya fedha hizo zitajenga maabara tatu katika shule ya sekondari Nyumbu, Miembe Saba na shule ya wasichana Kibaha ambapo tumejiwekea mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiunga na mfuko wa elimu nchini kwa lengo la kupata ruzuku ya miundombinu, samani, vifaa vya kufundishia na kujifunzia,” alisema Bayi.
Mwisho. 

   

No comments:

Post a Comment