Na John Gagarini, Kibaha
ASASI isiyo ya Kiserikali ya Amani Development Organization (ADEO) la Kibaha mkoani Pwani limetenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuwakopesha wasichana waliokuwa wakifanyabiashara ya ngono na matumizi ya dawa za kulevya zaidi ya 20.
Mbali ya kuwakopesha fedha hizo pia shirika hilo linawapatia elimu ya kuepukana na mambo hayo ambayo yamekuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Akizungumza jana mjini Kibaha kwenye mkutano shirikishi wa utekelezaji wa programu ya vijana kupambana na UKIMWI inayofadhiliwa na Sat Tanzania, mratibu wa shirika hilo Jane Apollo alisema kuwa lengo la kuwakopesha fedha hizo ni kuwapatia njia mbadala ili wajiepushe na vitendo hivyo.
Apollo alisema kuwa kupitia mpango huo umeweza kuwafikia vijana wa ndani na nje ya shule 3,817 ambapo kati yao wasichana wanaofanya biashara ya ngono 41 wanaume 11 wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, vijana 63 wanaotumia dawa za kulevya na machimbo sita ya mchanga.
"Lengo ni kuwafanya vijana kuachana na vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya na biashara ya ngono na kuwafundisha shughuli za ujasiriamali ili kuinua kipato chao na kupunguza umaskini katika maisha yao," alisema Apollo.
Moja ya waischana waliokuwa wakifanya biashaya ya ngono (Subira Hatibu) Jasmini siyo jina halisi alisema kuwa alikuwa akiishi Jijini Dar es Salaam na kujiuza kwa wanaume ambapo kwa siku alikuwa akitembea na wanaume watatu au wanne.
"Nilikuwa nikifanya biashara ya kujiuza kuanzia shilingi 50,000 hadi 30,000 kwa mtu mmoja ambapo nilifanya biashara hii kwa muda mrefu lakini sikuona faida yake zaidi ya kupata matatizo," alisema Jasmini.
Naye kijana aliyejitambulisha kwa jina la Omary Mkumba alisema kuwa alikuwa akijihusisha na uvutaji wa bangi pamoja na dawa za kulevya ambazo zilimsababisha kupata ugonjwa wa kifua kikuu lakini baada ya kupatiwa elimu aliamua kuachana na matumizi hayo.
Shirika hilo lilianzishwa mwaka 2010 na linajihusisha na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, UKIMWI, biashara ya ngono, mimba za utotoni, ndoa kwenye umri mdogo na afya ya uzazi.
mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Msalaba Mwekundu mkoani Pwani kimtoa misaada ya viatu na vifaa vya shule kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Nyumbu na vituo vya kulelea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Chama hicho kilitoa misaada hiyo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi hao waweze kusoma kwa kuwa na mahitaji muhimu ili kufanikisha masomo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya sherehe ya siku ya chama hicho inayoadhimishwa kila mwaka ambapo bkitaifa ilifanyika mkoani Mbeya, katibu msaidizi wa msalaba mwekundu mkoani humo, Felisiana Mmasi alisema kuwa waliamua kuadhimisha siku hiyo kwa kuwasaidia wanafunzi.
Mmasi alisema kuwa lengo la chama hicho ni kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali kwenye jamii ikiwa ni pamoja na kutoa msaada kwenye majanga na maafa yanoyojitokeza ikiwa ni pamoja na ajali, mafuriko na kwenye vita.
"Mbali ya kutoa viatu pia tumetoa madaftari na kalamu ambapo vituo vya watoto waishio kwenye mazingira magumu vya THADEI na Buloma wamenufaika na misaada hiyo," alisema Mmasi.
Naye mratibu wa mradi wa Life kupitia chama hicho Kibaha Mjini Agnes Lubogo alisema kuwa mbali ya kusaidia kutoa misaada mbalimbali pia wanasaidia kuwahudumia wagonjwa wa UKIMWI walio majumbani.
Lubogo alisema kuwa wanahudumia wagonjwa ambao watoro ambao hawapati huduma mahospitalini hivyo kuwafuata huko waliko ambapo wana wahudumu wa nyumbani wapatao 73.
Aliwataka watu kujiunga na chama hicho ili waweze kuisaidia jamii ambayo inahitaji misaada mbalimbali ya kiutu ikiwa ni pamoja na kujitolea damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa.
mwisho.
No comments:
Post a Comment