Na John Gagarini, Kibaha
MFUKO wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani
utazinduliwa Mei 31 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gharib Bilali.
Kwenye uzinduzi huo ambao utafanyika mjini Kibaha mgeni rasmi
ataongoza matembezi ya hisani kwa ajili ya kuhamasisha uchangiaji wa mfuko huo
ambao una lengo la kupata kiasi cha shilingi milioni 300.
Akielezea juu ya tukio hilo mwenyekiti wa mfuko huo Anna Bayi
alisema kuwa katika
uzinduzi huo kutatanguliwa na matembezi ya hisani yatakayoanzia maeneo ya
Mkoani hadi viwanja vya Maili Moja ambapo ndipo halfa itafanyika.
Bayi alisema kuwa hadi sasa tayari wameshapata kiasi cha
shilingi milioni 180 zitakazosaidia kuiwezesha halmashauri hiyo kukabiliana na
changamoto za sekta ya elimu hususan madawati na maabara.
"Mara
zitakapopatikana fedha hizo tutaanzia kununulia madawati 1,500 yenye thamani ya
shilingi milioni 90 na kujenga maabara tatu kwa shilingi Milion 210,” alisema
Bayi.
Alisema uchangiaji
huo utakuwa ni zoezi endelevu ili kuhakikisha wanapunguza ama kumaliza kabisa changamoto
za kielimu katika halmashauri ya Mji wa Kibaha.
“Kila mwananchi anatakiwa
kuchangia kiasi cha shilingi 2,000 wakiwemo ,wafanyabiashara, wamiliki wa makampuni na
wadau wa elimu na hadi sasa mwamko unaonekana kwa wananchi hivyo kuwa na imani
ya kuwa mfuko utafanikiwa,” alisema Bayi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo, Jeniffer Omolo
alisema mfuko huo umeundwa chini ya sheria namba 288 kifungu kidogo namba 80
katika tangazo la serikali namba 218 la tarehe 18 Juni 2010.
“Shule za msingi na
sekondari za serikali bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo
zinafanya lengo la utoaji elimu bora kushindwa kufikiwa kikamilifu,” alisema
Omolo.
Alibainisha kuwa Shule za msingi zilizopo wilayani Kibaha Mji
zinakabiliwa na uhaba wa madawati 3,488 hali inayopelekea baadhi ya shule
hizo wanafunzi kutumia kukaa zaidi ya watatu kwenye dawati moja.
Aidha alisema katika upande wa shule za sekondari kuna upungufu wa
maabara 24 ambapo kwa sasa kuna maabara 9 pekee, Halmashauri ya mji wa Kibaha ina
jumla ya shule za msingi 47 na shule za sekondari za serikali na binafsi 34 .
Mwisho.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment