Wednesday, May 21, 2014

WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KULIMA BANGI HEKARI 2

 Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia wakazi wawili wa Kijiji
cha Mwetemo wilaya ya Bagamoyo mkoani humo kwa tuhuma za kulima shamba
la bangi hekari mbili kwenye shamba la mahindi.

Watuhumiwa hao walibainika baada ya askari wa jeshi hilo kufanya doria
ya kusaka makosa mbalimbali wilyani humo ili kukamata wahalifu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana mjini Kibaha kamanda wa
polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi (SACP)
Ulrich Matei alisema kuwa msako huo ni wa kawaida.

Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 19 mwaka huu
majira ya saa 9 alasiri huko kijiji cha Mwetemo- Kiwangwa Tarafa ya
Msata wilayani humo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Musa Zahoro (20) na Asher Mbuya (29)
ambapo watuhumiwa hao watafikishw amahakamani mara upelelezi
utakapokamilika.

Kwenye tukio lingine Jeshi hilo linamshikilia Omary Sultan (32)
mkulima wa mkazi wa Kijiji cha Kauzeni wilaya ya Kisarawe kwa tuhuma
za kupatikana na pombe ya Moshi lita 12 na mtambo wa kutengenezea
pombe hiyo.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 19 majira ya saa 6:00 Kijijini
hapo na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara uchunguzi wa
tukio hilo utakapokamilika.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment