Na John Gagarini, Kibaha
MSICHANA Theresia Matai (19) ambaye ni mfanyakazi wa ndani
mkazi wa Kwa Mathias wilayani Kibaha mkoani Pwani anashaikiliwa na Jeshi la
polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumtupa mtoto wake aliyejifungua.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani
Pwani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa
tukio hilo lilitokea Mei 27 mwaka huu majira ya saa 3 usiku.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea eneo la
Mwembe tayari nyuma ya nyumba ya Dalaida Samwel (54) ambaye ni bosi wake ambapo
alikuwa akifanya kazi za ndani.
“Baada ya kufanya tukio hilo alirudi ndani na kulala na aliweza
kufahamika baada ya wasiri kutoa taarifa kuwa mtuhumiwa alionekana kuwa na
mimba na baada ya kujifungua alimwacha mtoto huyo nyuma ya nyumba hiyo,”
alisema Kamanda Matei.
Alibainisha kuwa jirani yake na mwenye nyumba Filbert
Sekeleno (31) alipata taarifa kutoka kwa jirani mwenzake aliyefahamika kwa jina
la Mama Frank kuwa kuna sauti ya mtoto nyuma ya nyumba alipokutwa mtoto huyo.
“Majirani waliongozana hadi kwenye eneo la tukio na kumkuta
mtoto mchanga wa kiume akiwa ametelekezwa na kutoa taarifa polisi ambao
walianza uchunguzi juu ya tukio hilo,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa mtuhumiwa alipelekwa hospitali ya Tumbi
kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na daktari kujua chanzo kilichosababisha
kufanya tukio hilo ambapo mtoto huyo anaendelea vizuri.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment