Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Msaada wa Kisheria wilayani Kibaha mkoani Pwani kimeiomba serikali kuwatambua wasaidizi wa kisheria ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Kutokana na changamoto nyingi za kisheria kuikabili jamii na watu wengi kukosa haki zao kwa kushindwa kujua sheria ambazo ndo msingi wa haki za binadamu wasaidizi hao.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria wa wilaya ya Kibaha ambayo yalitolewa na kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake (WLAC), mwenyekiti wa kituo hicho Israel Sazia alisema kuwa wasaidizi hao bado hawajatambuliwa rasmi na serikali.
Sazia alisema kuwa endapo wasimamizi wa msaada wa kisheria watatambuliwa wataweza kuisaidia jamii kutambua sheria mbalimbali ambazo zitawafanya wapate haki zao mara inapotokea migogoro kwenye jamii.
"Endapo watatambuliwa itasaidia hata kuwapatiwa misaada na fursa mbalimbali kutoka serikalini kupitia kwenye halmashauri kwa ajili ya kuiwezesha jamii katika masuala yanayohusu sheria," alisema Sazia.
Alisema kuwa wananchi wengi hawajui taratibu za kutafuta haki ikiwa ni pamoja na wanawake kwenye masuala mbalimbali endapo watashindwa kuendelea kuishi na mume wake pamoja hivyo kudai talaka.
"Kumekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na masuala ya mirathi, haki za watoto, migogoro ya ardhi na masuala ya ndoa ambazo zimekuwa zikileta migogoro mingi kwenye jamii," alisema Sazia.
Aidha alisema kuwa kituo chao kilichoanzishwa mwaka 2001 kimekuwa na changamoto kubwa ya wasaidizi hao kulegalega katika utendaji kazi kutokana na wengi wao kushindwa kujitolea hivyo kushindwa kufanya kazi kikamilifu.
Aliwataka wasaidizi hao wa kisheria kufanya kazi kwa kuzingatia weledi wa kazi zao ili kuweza kuisaidia jamii ambayo ina mahitaji makubwa ya kujua sheria mbalimbali katika maeneo yao ili waweze kupata haki zao za msingi.
Baadhi ya masomo waliyofundishwa ni pamoja na uelewa kuhusu dhana ya ya msaidizi wa kisheria, misingi na vyanzo vya sheria, sheria ya ndoa, sheria ya mirathi na taratibu za ufunguaji wa mirathi, sheria ya ardhi sura namba 113, sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya mwaka 2002, haki ya mtoto ya mwaka 1999 na ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za wateja na uandishi wa ripoti ya mwezi. Mafunzo hayo yaliwahusisha wasaidizi zaidi ya 30.
mwisho.
No comments:
Post a Comment