Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani umeingia umeingia
mkataba na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wenyeviti wa
halmashauri juu ya utekelezaji wa mpango wa kupunguza vifo vya mama wajawazito
watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano.
Pia mkoa umeingia na viongozi hao
kwenye mkataba kwa ajili ya makusanyo ya mapato ambayo waliyapitisha kuwa wana
uwezo wa kuyakusanya kwenye halmashauri
za wilaya saba za mkoa huo katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2014-2015.
Tukio hilo la kihistoria la
kusaini mikataba hiyo ya kazi kwa viongozi hao ndani ya mkoa wa Pwani
lilifanyika juzi mjini Kibaha na lilisimamiwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu
Mahiza na mwanasheria wa mkoa Mohamed
Magati ambapo viongozi hao endapo watashindwa kufikia malengo yaliyowekwa
itawabidi kujieleza.
Wakuu wa wilaya ambao waliingia
mikataba hiyo na wilaya zao ni pamoja na Mercy Silla wilaya ya Mkuranga, Fatuma
Kimariyo Kisarawe, Nurdin Babu Rufiji, Sauda Mtondoo wilaya ya Mafia, Ahmed
Kipozi wilaya ya Bagamoyo na Halima
Kihemba wilaya ya Kibaha.
Akizungumza na watendaji hao
kuhusiana na mikata hiyo walioingia na mkoa Mahiza alisema kuwa mikataba hiyo
itasaidia uwajibikaji kwa watendaji hao ambao wanawatumikia wananchi katika
kuwaletea maendeleo.
“Mikataba hii ni changamoto kwa
watendaji wetu hawa na endapo watashindwa kutekeleza majukumu yao kama mkataba
unavyoonyesha itabidi wajieleze kwani hata mimi nishaingia mikataba na mamlaka
za juu hivyo kila mtu lazima atimize wajibu wake,” alisema Mahiza.
Mahiza alisema kuwa kwa upande wa
vifo vya mama wajawazito, watoto wa changa na wale wenye umri chini ya miaka
mitano ni tatizo kubwa hivyo mkataba huo utasaidia kupunguza vifo hivyo visivyo
vya lazima.
“Kwa upande wa makusanyo kila
halmashauri ilileta makadirio yake ya kukusanya mapato kwenye bajeti ya mwaka
2014- 2015 hivyo ni lazima watimize kusudio lao na hakuna sababu ya kusema
wameshindwa kuyafikia malengo hayo ya ukusanyaji wa mapato,” alisema Mahiza.
Halmashauri hizo kila moja
imejiwekea kiwango chake cha kukusanya kutegemeana na vyanzo vyake vya mapato
ambapo Bagamoyo watakusanya bilioni2.6, Kibaha Mjini, bilioni 4.2, Kibaha
Vijijini bilioni 2.6, Kisarawe bilioni 3.8, Mafia bilioni 1, Mkuranga bilioni
2.1 na Rufiji bilioni 2.7 ambapo jumla ya makusanyo hayo kwa wilaya zote za
mkoa huo itakuwa ni bilioni 8.7
Naye mganga mkuu wa mkoa wa
Singida ambaye alishinda tuzo ya Rais ya kupunguza vifo vya makundi hayo Dk
Doroth Gwajima alisema kuwa vifo vingi vinatokana na uzembe wa baadhi ya
watumishi wasio na maadili ya kazi.
Dk Gwajima aliwataka wahudumu wa afya kwenye
mkoa huo wa Pwani kumtanguliza Mungu wakati wa utendaji wao wa kazi pia
kuzingatia maadili ya kazi zao kwani baadhi ya vifo vinatokana na uzembe na si
mapenzi ya Mungu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment