Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amezuia bajeti ya fedha
iliyokuwa inatengwa kwa ajili ya wenyeviti wa halmashauri za wilaya badala yake
fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.
Fedha hizo ambazo zimekuwa zikitengwa kwenye bajeti za kila
mwaka za halmashauri bado hazijaonyeshwa kuwa zinatengwa kwa kanuni gani
tofauti na fedha nyingine ndani ya halmashauri.
Akizungumza na wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri,
maofisa mipango na waweka hazina wa halmashauri za mkoa huo Mahiza alisema kuwa
fedha hizo ni nyingi kwani baadhi ya wenyeviti wamekuwa wakitengewa hadi
milioni 11 kw akila bajeti.
Mahiza alifikia kutoa agizo hilo baada ya baadhi ya
halmashauri kusema kuwa zimetenga fedha hizo kwa ajili ya wenyeviti wa
halmashauri kwa ajili ya matumizi ambayo hayakuwekwa bayana.
“Natoa agizo kuwa mfuko huo wa fedha kwa ajili ya mwenyekiti
uondolewe hadi mtakapotoa mwongozo wa mfuko kwani mifuko yote ikiwemo ile ya
Jimbo ya Mbunge ipo kisheria na inatambulika je huu umewekwa kwa kufuata sheria
ipi,” alisema Mahiza.
Alisema kuwa hana nia mbaya juu ya kuzuia mfuko huo lakini
anachotaka ni mwongozo ambao unaelekeza kuwepo kwa fedha hizo ambapo
wakurugenzi walishindwa kuonyesha ni sheria gani wanayoitumia kutenga fedha hizo.
“Hadi sasa hakuna anayejua fedha hizi zinatengwa kwa kufuata
utaratibu au mwongozo upi hivyo naomba ofisa wa serikali za Mitaa anipatie
mwongozo ili mfuko uo uendelee na kama hakuna mwongozo wowote basi fedha ziende
kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Mahiza.
Aidha alisema hata wakuu wa wilaya hawana fedha kama hizo
ambapo wao fedha zao hazizidi zaidi ya milioni tano jambo ambalo liliwashitua
watu wengi waliposikia kuhusu mfuko huo wa wenyeviti wa halmashauri.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
ILI kuleta ufanisi wa utendaji kazi kwa wauguzi mkoa wa Pwani
utawapatia kiasi cha shilingi 1,000 kwa muuguzi atakayezailisha mama wajawazito
kwa usalama.
Pia vituo vya afya na zahanati zinatakiwa kufanya kazi kwa
saa 24 ili kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa muda wote tofauti na ili
sasa ambapo wahudumu wa afya wanafunga muda wa kazi saa 9:30.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu
Mahiza wakati wa kikao cha kazi ambacho kiliambatana na uingiwaji wa mikataba
baina ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo juu ya
utendaji kazi kwenye sekta ya afya na makusanyo kwenye bajeti ya mwaka 2014-
2015.
Mahiza alisema kuwa mpango wa kuwapa fedha wauguzi
wanaowazalisha mama wajawazito salama ni kuwapa hamasa ili waweze kufanya vizuri
katika kuwahudumia akinamama hao.
“Kwa kuwa tayari tumeshaingia mkataba na wakuu wa wilaya na
wakurugenzi wa halmashauri kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama wajawazito,
watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano lazima tuwape
motisha watendaji wa sekta ya afya ili wafanye kazi kwa moyo,” alisema Mahiza.
Aidha Mahiza alisema kuwa kuanzia sasa vituo vya afya na
zahanati vifanye kazi kwa saa 24 ili kuweza kufikia malengo ya kupunguza vifo
hivyo pamoja na utoaji huduma kwa muda wote kwani ugonjwa hauna saa.
No comments:
Post a Comment