WABUNGE wa Bunge Maalumu la Katiba ambao walisusia vikao vya
bunge hilo Mjini Dodoma wametakiwa kurejea kwenye mjadala wa marekebisho ya
katiba kwani kuendelea kususia ni sawa na kufanya uasi na usaliti kwa wananchi.
Wanapaswa kuheshimu mamalaka iliyopo kwa kulimaliza tatizo
lililopo kwa kutumia busara kwa kukaa chini kwa pamoja na kukubaliana na si kwa
kulalamika kwa kupiga kelele nje ya Bunge hilo ili suluhu ipatikane.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha Nabii Jofrey
John wa Huduma ya HAKI Ministry ya Kongowe Kibaha mkoani Pwani amesema kuwa
endapo wabunge hao wataendelea kususia bunge lijalo kama walivyosusa ni kwamba
watakuwa wanaihujumu nchi.
Nabii John amesema kususa na kulalamika nje ya bunge hilo ni
sawa na kuasi hali ambayo inaweza kujenga chuki na matokeo yake ni kuleta
mafarakano ambayo mwisho wake ni mbaya kwani urithi walionao Watanzania ni
amani na si vurugu
Nabii John amesema kuwa kusiwe na kundi ambalo linasusia
mchakato wa kuunda katiba hiyo mpya kwani ni moja ya njia ambayo inaweza
kusababisha kuvurugika kwa amani na litajenga roho za kuona kuwa wanaonewa.
Amesema kuwa haitapendeza kuona kuwa kuna wabunge wamekwenda
kwenye bunge hilo kwa ajili ya kuhujumu mchakato huo kwani watasababisha
kuvunja amani iliyopo ambayo imedumu kwa maiaka 50 tangu tulipopata uhuru hivyo
haipaswi kuvunjwa na kundi la watu.
Amesema kiongozi yoyote awe wa chama au sehemu yoyote
amechaguliwa na Mungu hivyo hapaswi kudharau mamlaka iliyopo madarakani ambayo
hata Mungu anaitambua.
Aidha amesema kuwa anaamini kuwa wabunge waliochaguliwa
kwenye bunge hilo la katiba ni wasomi hivyo wasijishushie heshima ya usomi wao
kwani wako pale kwa niaba ya wananchi na si kwa maslahi yao binafsi bali kwa
maslahi ya wananchi.
Amewataka waumini wa dini zote kufunga na kuomba kwa ajili ya
amani ya nchi ili Mungu aepushe roho ya umauti katika nchi yetu ambayo
inanyemelea kutokana na sababu ambazo
zinaweza kuzuilika za kumaliza tofauti ndogo ndogo zilizopo.
Ameiomba serikali kuwatumia viongozi wa dini kama sehemu ya
kudumisha amani ya nchi kwa kuwafanyia maombi viongozi waliopo madarakani ili
waweze kuongoza kwa kutumia hekima za Mungu kwani bila ya kuwa na maombi hayo
shetani anaweza kuleta roho ya uchonganishi na kusababisha amani kutoweka.
Amebainisha kuwa kwa kipindi chote cha mwezi huu hadi ujao
watakuwa na kongamano kubwa la kuiombea amani ya nchi ambapo halitakuwa na
itikadi ya dini yoyote bali ni madhehebu yote hivyo kuwataka watu kujitokeza
kufanya maombi hayo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment