Na John Gagarini, Kibaha
IDARA ya Afya ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani
imeanza uhakiki wa wafanyabiashara mbalimbali kama wamepima afya zao kwa mujibu
wa sheria ili watoe huduma hizo wakiwa na afya njema na endapo watashindwa
kufanya hivyo watafungiwa biashara zao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jana mjini Kibaha ofisa afya wa Halmashauri ya Mji
wa Kibaha David Vuo alisema kuwa wafanyabiashara hao pamoja na wamiliki wa
viwanda wanapaswa kuhakikisha watoa huduma wao wanapima afya zao.
“Utaratibu huu ni wa kisheria kwani hata wafanyakazi wa
serikali kabla ya kuanza kazi wanapaswa kupima afya zao na hii ni sheria ya
afya ya mwaka 2009 namba 169 kifungu namba 17ambapo kwa sasa maofisa afya wa
kata wanafanya uhakiki kuona zoezi hilo ili taratibu stahiki zichukuliwe kwa
wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo ,” alisema Vuo.
Alisema kuwa jambo hilo si geni kwani liko kisheria na
linawagusa wafanyabiashara wote na shughuli mbalimbali za wajasiriamali ambao
wanapaswa kufuata taratibu za kiafya.
“Lengo la kupima afya na kuhakikisha kuwa wahudumu hao
wanahudumia wateja wakiwa na afya njema na kama kuna atakayegundulika anapaswa
kutibiwa kwanza hadi atakapopona ndipo aendelee kutoa huduma na kutakuwa na
fomu maalumu itakayokuwa kwenye eneo la shughuli ili kuwatambua waliofanya
hivyo na wale watakaoshindwa hawataruhusiwa kuhudumiwa watu,” alisema Vuo.
Aidha alitaja magonjwa ambayo yanapimwa kuwa ni Taifodi,
Kuhara, Mkojo, magonjwa ya Kaswende, Gono, Kifua, magonjwa ya ngozi kama vile upele
na mengineyo.
“Suala la kupima virusi vya ugonjwa wa UKIMWI ni hiyari
ambapo upimaji wa magonjwa haya hayahusiani na kupima ugonjwa huo labda mhusika
atake mwenyewe ambapo upimaji huu utafanyika kwenye hospitali ya wilaya ya
Mkoani na kituo cha afya Kongowe,” alisema Vuo.
Ofisa afya huyo wa halmashauri ya Mji wa Kibaha alissema kuwa
kuhusiana na uchangiaji wa vipimo hivyo kila mhusika anapaswa kutoa kiasi cha
shilingi 5,000 kwenye ofisi ya kata kisha atapewa fomu kwa ajili ya kwenda
kupima ambapo alisema elimu ilishatolewa.
Alitaja biashara ambazo watumishi wake wanatakiwa kupima afya
zao kuwa ni mama na baba lishe, bekari, migahawa, hoteli, baa, nyumba za kulala
wageni, mashine za kusaga nafaka, maduka ya vyakula, mabucha, machinjio,
saluni, dobi, viwanda, wachoma chipsi, vilabu vya pombe za kienyeji,
wafanyakazi wa kampuni na vikundi vya ujasiriamali.
No comments:
Post a Comment