Na John Gagarini, Kibaha
WATU wawili wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya
magari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani
Pwani, kamishna Msaidizi mwandamizi wa polisi (SACP) Ulrich Matei amesema kuwa
ajali hiyo ilihusisha lori na gari dogo.
Kamanda Matei alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Juni 16 mwaka
huu majira saa 1:15 usiku eneo la Chamakweza kata ya Pera tarafa ya Chalinze
wilayani Bagamoyo.
Alisema ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba
za usajili T 164 AUS na tela namba T 498 AZ likiendeshwa na Hassan Shaban mkazi
wa Dar es Salaam ambaye aligongana na gari aina ya Isuzu Carry lenye namba za
usajili Z 190 DR likitokea mkoani Morogoro.
“Waliokufa ni dereva
wa gari dogo Meja Edward Mosi ambaye ni ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) kikosi cha Kinonko na mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa wilaya ya Korogwe
mkoani Tanga Johnson Zakaria,” alisema Matei.
Aidha alisema katika ajali hiyo mtu mmoja alijeruhiwa na
kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kwa ajili ya matibabu huku
miili hiyo nayo ikiwa hospitalini hapo kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.
“Kutokana na ajali hiyo jeshi la polisi linamtafuta dereva wa
lori ambaye alikimbia mara baada ya tukio hilo, ili aweze kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria,” alisema Matei.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment