WAKAZI wa wilaya za Bagamoyo mkoani Pwani na Pangani mkoani
Tanga wametakiwa kulinda misitu ikiwemo ile ya Mikoko iliyopo kandokando mwa
Bahari ya Hindi ili kuinusuru wilaya hiyo na athari zitokanazo na mabadiliko ya
Tabia Nchi.
Hayo yalisemwa na mkuu
wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi alipokuwa akifungua mafunzo ya juu ya namna
ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi kwa wajumbe wa kamati za mazingira
kutoka wilaya za Bagamoyo na Pangani mkoani Tanga.
Kipozi amesema kuwa watu wengi waliathirika na mvua kubwa
zilizonyesha ambazo zilileta mafuriko na kusababisha madhara yakiwemo ya watu
kufa, mazao yao kusombwa na maji, miundombinu ikiwemo ya barabara na madaraja
zilitokana na mabadiliko hayo ya Tabia Nchi.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mratibu wa mafunzo hayo Dk
Beno Mnembuka ambaye ni mtafiti kiongozi kwenye mradi huo unaosimamiwa na Chuo
Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Ardhi,
Mamlaka ya hali ya Hewa na mtafiti mmoja toka nchini Norway amesema kuwa
mabadiliko ya Tabia Nchi pia yameathiri viumbe hai kama vile samaki.
Dk Mnembuka amesema kuwa viashiria vya mabadiliko ya Tabia
Nchi ni pamoja na mabadiliko ya misimu ya mvua, joto, upepo mkali wa Kasi na
Kusi, ukame, mafuriko ambapo hutokana na uharibifu wa mazingira ambapo ili
kukabiliana na madhara hayo lazima kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti na
kutoharibu vyanzo vya maji.
Naye meneja wakala wa
misitu Tanzania (TFS) wilaya ya wilaya Bagamoyo Charles Mwafute amesema kuwa
katika kutekeleza kwa vitendo washiriki wa mafunzo hayo walipanda miti ya
Mikoko eneo la ukubwa wa hekari mbili na nusu kwenye kijiji cha Kiharaka.
Mradi huo ambao utaisha mwezi Desemba mwaka huu unatekelezwa
kwenye vijiji vya Bumbwini, Kisakasaka Zanzibar, Magomeni, Kiharaka na Kondo
wilayani Bagamoyo, Matakani, Kipumbwi na Pangani Mjini wilaya ya Pangani.
No comments:
Post a Comment