Saturday, September 12, 2026

DIWANI LUTAMBI AWATAKA WANANCHI KURASIMISHA ARDHI WAMILIKI KISHERIA

WANANCHI wa Mtaa wa Muheza Kata ya Maili Moja wametakiwa kuchangamkia fursa ya urasimishaji ardhi baada ya serikali kupunguza gharama kutoka 150,000 hadi 130,000.

Akizungumza na wananchi wa Mtaa huo Diwani wa Kata ya hiyo Ramadhan Lutambi alisema kuwa hiyo ni fursa kwa wananchi kuelekea kupata umiliki wa ardhi kisheria.

Lutambi alisema kuwa kumiliki ardhi kisheria kuna faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuepukana na migogoro ya ardhi ambaye imeleta changamoto kubwa kwa wananchi.

"Tunaishukuru Serikali kwa kupunguza gharama za urasimishaji ardhi hivyo kuwafanya wananchi kumiliki ardhi kisheria hivyo kuwa na umiliki halali na kupunguza migogoro,"alisema Lutambi.

Akizungumzia suala la changamoto ya maji alisema kuwa kuna mradi wa maji ambao kwa sasa uko kwenye utekelezaji ambapo mitaa yote itapitiwa ambapo kwenye mtaa huo watu zaidi ya 8,000 hawapati huduma hiyo.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo alisema kuwa mikopo ya asilimia 10 ipo kwa makundi wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mawazo alisema kuwa fedha zimetengwa jambo kubwa ni walengwa kuunda vikundi ambavyo vitatimiza masharti ikiwa ni pamoja na usajili huku kwa watu wenye ulemavu hata kwa mtu mmoja anaruhusiwa.

Akizungumza kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa mradi wa maji wa Pangani utaondoa changamoto ya maji kwenye mtaa huo hivyo wananchi wawe na subira.

John alisema kuwa Serikali imekuwa ikipambana kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto hiyo ambayo imekuwa kero kubwa lakini inakwenda kupatiwa suluhu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alisema kuwa mipango iliyopo ni ujenzi wa Shule ya Sekondari na Zahanati.

Shemwelekwa alisema kuwa kuhusu urasimishaji vifaa vimenunuliwa kwa ajili ya urasimishaji hivyo wananchi wajiandae na watazichukua changamoto zilizotolewa na wananchi ili wazipatie ufumbuzi.

Wednesday, September 9, 2026

ULEGA ATAKA MIUNDOMBINU ITOE HUDUMA KIPINDI CHA MVUA ZA ELNINO.

WAZIRI wa Ujenzi Abdala Ulega ametaka hatua za haraka kuchukuliwa ili miundombinu ya barabara iendelea kutoa huduma hata wakati wa mvua kubwa za Elnino zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni kote nchini.

Ulega ametoa maelekezo hayo akiwa mkoani Pwani katika ziara yake aliyoianza ya ukaguzi wa maandalizi ya kimiundombinu kufuatia maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa watendaji wa Serikali kuhakikisha nchi inakingwa na athari za mvua zinazoweza kujitokeza wakati huo.

Amesema kuwa inapaswa kufanyika kwa ukaguzi wa barabara na madaraja kote nchini kama sehemu ya maandalizi dhidi ya mvua kubwa za Elnino zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha amesema kuwa ukaguzi huo ndiyo utakuwa msingi wa kufahamu ni wapi na wapi panahitaji kufanyiwa kazi ili mvua hizo zisiathiri mzunguko wa watu na biashara.

"Naagiza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha barabara na madaraja yote nchini yanakaguliwa na hatua za haraka kuchukuliwa ili miundombinu hiyo iendelea kutoa huduma hata wakati wa mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini",amesema Ulega.

Amesisitiza kuwa pamoja na uwepo wa vifaa ³na mitambo utayari wa wataalam na watendaji ndio msingi wa kuhakikisha nchi inapita salama katika kipindi cha mvua hizo.

"Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS kufanya tathmini ya kila wiki katika mikoa yote nchini ili kubaini maeneo yoyote yanayohitaji kuongezewa nguvu kwa wakati ili kuhakikisha huduma za dharura zinafika kila kona ya nchi,"amesema Ulega.

Aliingeza kuwa TANROADS mejipanga katika kanda mbalimbali na Mkoa wa Pwani ndiyo kitovu cha kanda zote kwa ajili maandalizi ya tahadhari ya mvua za Elnino.

Pia alikagua pia vifaa mbalimbali vitakavyotumika kufanya matengenezo ya dharura katika miundombinu ya barabara na madaraja nchini
kote.

Meneja wa TANROADS Mkoa waPwani Mhandisi Joel Mwambungu amesema kuwa wamejipanga kukabiliana na athari za mvua hizo kwa ununuzi na usambazaji wa vifaa vya dharura katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwambungu amesema kuwa TANROADS tayari ina kalavati za chuma zenye jumla ya urefu wa mita 5,638 zitakazotumika katika maeneo ambayo barabara au madaraja yanaweza kupata athari kutokana na mvua hizo.

mwisho.

Tuesday, September 8, 2026

MEYA DK NICAS MAWAZO AKABIDHI PHOTOCOPY MACHINE KWA SEKONDARI YA MWAMBISI




MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo amekabidhi mashine ya kudurusu karatasi kwa Shule ya Sekondari Mwambisi na kusema kuwa itapunguza gharama za uandaaji mitihani.

Mawazo alikabidhi mashine kwa uongozi wa shule hiyo kwa kushuhudiwa na Ofisa elimu Sekondari, bodi za Shule za Sekondari za Manispaa, baadhi ya wazazi na wanafunzi wa Shule hiyo.

Amesema kuwa Serika inaendelea kuwaka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu na kupunguza changamoto za Shule ndani ya Manispaa.

"Utoaji wa mashine hii ni kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa elimu kwani amejitahidi kujenga miundombinu ya elimu,"amesema Mawazo.

Aidha amesema kuwa miaka ya nyuma Shule zilijengwa na wananchi lakini kwa miaka ya sasa Serikali imejenga miundombinu mingi ya elimu hivyo wadau nao waunge mkono serikali.

"Kuhusu bweni wenyeviti wa bodi za Shule zielezee kwenye mipango yao juu ya mahitaji hayo na kama yapo tutaongea na wadau ili kushirikiana na serikali kuyajenga kama kuna mahitaji hayo,"amesema Mawazo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yahaya Mtonda amesema kuwa kuna haja ya kuipandisha hadhi Shule hiyo ili iwe na kidato cha tano.

Mtonda amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wanashindwa kwenda kusoma mbali pale wanapofaulu kutoka Shule za Msingi kwenye Manispaa ya Kibaha.

RC PWANI KUENDELEZA AGENDA YA UWEKEZAJI NA KUWAJENGA VIJANA KIUCHUMI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amesema ataendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili kukuza uwekezaji na uchumi wa Mkoa wa Pwani, huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kiuchumi.

Mhe. Nyongo amesema hayo leo, Septemba 8, 2026, wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Abubakar Mussa Kunenge, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Amesema Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa maeneo muhimu kwa uwekezaji nchini na kwamba atashirikiana na viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa rafiki kwa wawekezaji.

“Mkoa huu ni wa uwekezaji. Nimezunguka maeneo mbalimbali kutafuta wawekezaji, kwa hiyo niwakaribishe kwa kuweka mazingira wezeshi,” amesema Mhe. Nyongo.

Aidha, Mhe. Nyongo ameomba ushirikiano wa jamii katika kuwajenga na kuwawezesha vijana kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi yanayolenga kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.

Amesema atashirikiana na viongozi wa Mkoa katika kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, mifugo, uchumi wa buluu pamoja na sekta nyingine za uzalishaji.

“Ninaamini utendaji wetu wa pamoja utatumika kikamilifu katika kuendelea kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zao mbalimbali, pamoja na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nyongo ameomba viongozi na wananchi kutumia sheria, kanuni na taratibu katika kutatua migogoro ya ardhi, akisisitiza umuhimu wa kutumia busara na haki ili kupata suluhisho la kudumu.

Ameahidi kulisimamia kwa karibu suala hilo kwa lengo la kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua na wananchi wanapata haki na fursa ya kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

KONEKTI NA WAZIRI


Serikali inaendesha programu maalumu kwa vijana waliojikita kwenye kilimo.

Fursa hizi ziko kwenye mnyororo mzima wa Kilimo.

Kuanzia uzalishaji wa mbegu, mikopo ya vifaa vya kilimo...

Pembejeo za kilimo, kuongeza thamani mazao...

Usafirishaji mazao, uhifadhi mazao...

Karibu upate nafasi ya kupata taarifa kuhusu programu hizi pamoja na namna ya kupata mikopo ya masharti nafuu kwenye sekta ya kilimo.

Ili uweze kuzitumia ipasavyo fursa hizi zilizoandaliwa kwa ajili yako.

Kipindi ni kesho saa 11 jioni LIVE Instagram, Facebook na YouTube: @ Joel Nanauka & Waziri Wa Vijana.

Kama utahudhuria comment neno "NDIO".

Saturday, September 5, 2026

MJUMBE WA HALMASHAURI KUU MKOA WA PWANI ALHAJ MUSSA MANSOUR AJITOLEA KUJENGA OFISI YA CCM KATA YA MKUZA

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mussa Mansour ametoa vifaa vya ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Mkuza Wilaya ya Kibaha Mjini.

Akizindua ujenzi wa ofisi hiyo na kuhudhuria Mkutano Maalum wa Kata hiyo Mansour amesema kuwa alipewa ombi na Kata hiyo ambayo inatumia ofisi za tawi kwa ajili ya shughuli zake.

Mansour amesema kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo vya ujenzi ni kufanikisha Kata hiyo kuwa na ofisi ili kuwa na ofisi badala ya kutegemea ofisi ambazo siyo zao.

"Nimejitolea ili kuimarisha chama na ningetamani uchaguzi wa ndani ya chama mwakani ufanyike kwenye ofisi hizo kikubwa ni uongozi kufuata taratibu ili tuweze kufikia lengo la kuzikamilisha,"amesema Mansour.

Amesema kuwa aliahidi mchanga, simenti, kokoto nondo na matofali anashukuru kwani vyote amevitoa kilichobaki ni ujenzi tu kuanza na uzinduzi uliifanyika ndiyo ishara ya kazi kuanza.

Naye Mwenyekiti wa Kata ya Mkuza Matata Ngollo amesema kuwa wanamshukuru Mjumbe huyo wa Halmashauri ya Mkoa kwa kujitoa kwake kusaidia ujenzi huo.

Ngollo amesema kuwa wanamshukuru kwani vifaa hivyo vitafanya ujenzi kwa asilimia 80 na itabaki umaliziaji tu hivyo kuifanya Kata nayo kumiliki ofisi yake.

Mjumbe huyo alikuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano Maalum wa Kata ambapo alizungumza na viongozi mbalimbali wa ngazi za matawi, alizindua tawi la CCM la waendesha bodaboda tawi la Barckyard, alitembelea kijiwe cha draft na kutoa fedha kwa makundi maalum wakiwemo wajane, wazee, bodaboda  na watu wenye ulemavu na vijana na alitembelea soko la Mkuza.

Wednesday, September 2, 2026

WAMACHINGA WAISHUKURU SERIKALI KUWATENGEA ENEO LA BIASHARA

WAFANYABIASHARA wadogo Mkoani Pwani maarufu kama Wamachinga wameishukuru serikali kwa kuwatengea eneo maalum kwa ajili ya kufanyabiashara.

Hayo yemesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoani humo Filemon Maliga alipokuwa akizungumzia kuhusu zoezi la kusajili wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kwenye eneo la hifadhi ya barabara eneo la Maili Moja.

Maliga amesema kuwa wafanyabiashara hao wametengewa eneo lingine kwa ajili ya kufanya biashara mara utaratibu wa eneo jipya utakapokamilika watahamishiwa hapo ili kuendelea na biashara zao.

"Kama unavyoona zoezi linaloendelea na kuwasajili kutegemeana na biashara wanazofanya wakiwemo wauza mitumba, mama lishe, wauza matunda, chips na biashara nyingine,"amesema Maliga.

Amesema kuwa kutokana na uhaba wa ajira watu wengi wameingia kwenye mfumo wa kujiajiri kwa kufanya biashara hivyo hiyo ni ajira kwa kundi hilo kwani watu wanaendesha maisha yao kupitia biashara zao.

"Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutaka wafanyabiashara wadogo nao watengewe mazingira mazuri kwa ajili ya kufanya biashara zao wakiwa kwenye mazingira rafiki hivyo kufanya biashara zao kwa uhuru,"amesema Maliga.

Aidha amesema kuwa kupitia biashara hizo wafanyabiashara hao wanaendesha maisha yao kw kujenga nyumba kusomesha watoto na kuongeza kipato na kujiletea maendeleo.

Naye moja ya wafanyabiashara wa eneo hilo Wilielmina Lazaro amesema kuwa mpango huo ni mzuri kwani walikuwa hawana eneo maalum na hapo walikuwa wakifanya kwenye eneo la hifadhi ya barabara ambapo maandalizi ya ujenzi yataanza wakati wowote. 

Lazaro amesema kuwa wanatunza familia zao pia baadhi wanakopa fedha kupitia biashara zao hivyo kuweza kukuza biashara na kujiletea maendeleo wao na familia zao.