Saturday, June 15, 2024

WAZIRI JAFO ATUA KWA DC MAGOTI KUWEKA MIPANGO YA MAENDELEO

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi Makamu wa Rais Muungano na  Mazingira na Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Seleman Jafo amefika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kwenda kumsalimia Mkuu mpya wa Wilaya hiyo Petro Magoti.

Waziri Jafo alikwenda kumtembelea mkuu huyo mpya wa Wilaya ikiwa imepita  siku moja tu baada ya kuapishwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge.

Waziri Jafo amesema kwamba ameamua kwenda kumtembelea mkuu huyo kwa lengo la kuweza kumpongeza kwa dhati baada ya kuteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenda kuwaongoza wananchi wa Kisarawe.

 Jafo amesema kwamba ana mfahamu Magoti kwa muda mrefu kutoka na kuwa mchapakazi hodari na anatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa maslahi ya wananchi.

 "Kitu kikubwa nimekuja katika ofisi za Mkuu wa Wilaya lakini lengo kubwa ni kubadilisha mawazo katika Wilaya yetu ya Kisarawe na mimi nampongeza sana Magoti kwa kuletwa hapa,"amesema Waziri Jafo.

Pia Waziri Jafo alimshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kumteua Magoti nakumleta Kisarawe kwa lengo la kuwatumikia wananchi.

Sambamba na hilo Jaffo hakusita kumpa pongezi mkuu huyo wa Wilaya kwa kuchapa kazi kwa bidii zaidi kwani wanafahamiana tangu alipokuwa Waziri wa TAMISEMI waliweza i kufanya kazi kwa ushirikiano wa hali na mali.

Kwa upande wake Mkuu huyo wa Wilaya Petro Magoti amemwahidi waziri Jafo kumpa ushirikiano wa karibu zaidi lengo ikiwa ni kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.


  

Friday, June 14, 2024

HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI YA MAFUTA KINGA KWA WATU WENYE UALBINO

 

SERIKALI imezitaka Halmashauri nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kununua mafuta kinga ya kujipaka watu wenye ualbino ili kuepukana na mionzi ya jua ambayo inawasababishia kansa ya ngozi.

Hayo yalisemwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi ambapo hotuba yake ilisomwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya kuongeza uelewa juu ya Ualbino Duniani (IAAD) ambapo kitaifa ilifanyika Kibaha.

Ndejembi alisema kuwa serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye ualbino wanawekewa mazingira mazuri ili kupata huduma muhimu zikiwemo za kiafya.

"Tunaziagiza Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kununulia mafuta hayo (sun screen lotion) ili ziweze kuwasaidia kukabiliana na mionzi ya jua ambayo imekuwa ikiwasababishia kansa ya ngozi,"alisema Ndejembi.

Alisema kuwa huduma za afya ni sehemu ya jukumu la serikali kama inavyotoa huduma nyingine na hiyo ni huduma mojawapo kwa wananchi.

"Pia ni vema kuwapatia vifaa zaidi kuliko fedha pale wanapokuwa wanahitaji vifaa kama vile vyerehani ili waweze kushonea kofia ambazo zinawasaidia kukabiliana na mwanga mkali na jua,"alisema Ndejembi.

Aidha alisema kuwa serikali iko makini katika kuangalia ustawi wa watu wenye ulemavu ambapo inawndelea na utaratibu wa kuboresha sheria ya watu wenye ulemavu na inalaani matukio ya kuwafanyia vitendo vya ujatili watu wenye ualbino.

"Jamii inapaswa kuthamini utu wa mtu na ni jukumu la kila mwananchi na kamati za usalama za mikoa zihakikishe vitendo hivyo vinakomeshwa na wao kwa wao waache migongano na washiriki uchaguzi kwa kuchagua na kuchaguliwa kwani ni haki yao,"alisema Ndejembi.

Aliwataka maofisa watendaji kuhakikisha wanafanya utambuzi wa watu wenye ualbino na kuhusu asilimia mbili ya mikopo ya Halmashauri kwa watu wenye ukemavu kwa mtu mmoja mmoja badala ya kukopa kwa vikundi serikali inalifanyia kazi suala hilo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, SACP Ralph Meela  alisema kuwa wataendelea kusimamia ulinzi na usalama hivyo watu wenye ualbino wasiwe na wasiwasi.

Meela alisema kuwa wanafanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na wakaguzi wa polisi ngazi ya kata zaidi ya 3,000 nchini na kuna makamishna wa polisi jamii kwenye mikoa hivyo kutakuwa na usalama wa kutosha.

Kwa upande waka katibu wa Chama Cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) Batha Totei amesema kuwa wanaomba ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu na kuondoa gharama za matibabu ya kansa kwa watu wenye ualbino na kuwa na mpango wa bima ya afya.

Totei alisema kuwa serikali iweke mpango wa kuwa na kliniki kwenye hospitali za wilaya na kliniki tembezi na kuwashirikisha kwenye mikutano ya kampeni ili waweze kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa watu wenye ualbino.



MAGOTI KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI KUWATUMIKIA WANAKISARAWE

MKUU mpya wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amesema kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na viongozi waliopo ili kuleta maendeleo kwa wabanchi wa wilaya hiyo. 

Magoti ameyasema hayo Mjini Kibaha alipokula kiapo cha kuwa Mkuu wa Wilaya ambapo aliapishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge 

Amesema kuwa anamshukuru Rais kwa kumpa nafasi hiyo na hilo ni kama deni atalilipa deni hilo alilonalo kwa kuwatumikia wananchi wa Kisarawe katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Kunenge amewataka wakuu wa Wilaya zote kuhakikisha wanasimamia mapato kwenye Halmashauri zao ili ziweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

 Amewataka kutatua changamoto za wananchi kwa wakati na usimamizi kwenye utoaji huduma za afya na maji na usimamizi wa miradi ya elimu, barabara ili fedha zinazotolewa na serikali ziwe na tija.

Wednesday, June 12, 2024

WATU WENYE ULEMAVU WATAKA KUTEULIWA NAFASI NGAZI ZA MAAMUZI

CHAMA Cha Watu Wenye UalbinoTanzania (TAS) kimeiomba serikali iwateue kwenye nafasi za ngazi za maamuzi.

Aidha ametaja nafasi hizo za maamuzi kama vile Uwaziri, Ukuu wa Mikoa na Ukuu wa Wilaya kwani nao wanauwezo kama walivyo watu wengine.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Bodi ya chama hicho Thomas Diwani wakati akitoa salama za chama kwenye kongamano la kuongeza uelewa juu ya Ualbino lililofanyika kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwa Mfipa Kibaha.

Naye Mkurugenzi kitengo cha huduma kwa watu wenye ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Rasheed Maftah amesema kuwa serikali inaanda sera na miongozo mbalumbali kwa watu wenye ulemavu za kuweka usawa na haki.

Awali mwenyekiti wa Tas Godson Mollel amesema kuwa wanampongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Hospitali Rufaa ya KCMC kwa kuwapatia kiasi cha shilingi milioni 124 kwa ajili ya kuzalisha losheni zinazotumiwa na watu wenye ualbino.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa mkoa wa Pwani Nickson John amesema kuwa watu wenye ualbino wapatao 368 wanapatiwa misaada mbalimbali na zimeundwa kamati za watu wenye ualbino.


MAHAKAMA YATAKIWA KUTOA ADHABU KALI WANAOWAFANYIA VITENDO VYA UKATILI WATU WENYE UALBINO



CHAMA cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimeiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa watu wanaokutwa na hatia ya kuwakata viungo au kuwaua watu wenye Ualbino.

Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Taifa wa TAS Godson Mollel alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya siku kuongeza uelewa juu ya Ualbino (IAAD) duniani.

Mollel amesema kuwa Mahakama ikotoa hukumu kali kwa wahusika hao itakuwa fundisho kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha kuwadhuru watu wenye Ualbino.

Naye ofisa ustawi mkuu toka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye ulemavu Joy Maongezi amesema kuwa sheria namba 9 ya mwaka 2010 inataka kuwa na haki kwa watu wenye ulemavu ambapo watu wenye Ualbino ni sehemu yao.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala amesema kuwa wakati wa maadhimisho hayo huduma mbalimbali zinatolewa ikiwa ni pamoja na upimaji saratani ya ngozi, utoaji miwani, kofia na losheni ya kuzuia ngozi kuathirika, upimaji wa tezi dume na kansa ya kizazi.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka duniani ambapo kilele huwa tarehe 13 Juni kila mwaka na kwa mwaka huu kitaifa yanafanyika Kibaha Mkoani Pwani.


Monday, June 10, 2024

KAMPUNI YA REFUELLING TANZANIA LIMITED YATOA MABATI 72 KWA KIKUNDI CHA KUKAYA MIONO

KAMPUNI ya Refuelling Tanzania Ltd imekipatia mabati 72 kikundi cha KUKAYA-Miono Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya shule ya msingi Miono.

Akipokea mabati hayo kwa niaba ya kikundi cha KUKAYA MIONO ,Mwenyekiti Omary Mtiga ameishukuru kampuni ya Refuelling kwa msaada huo.

Alieleza ujenzi una miezi sita kwa nguvu zao wananchi ,wameshapokea milioni 13.5 kutoka kwa wadau, lengo lilikuwa kujenga kuongeza darasa moja lakini wamefanikiwa kujenga madarasa mawili.

Mtiga alifafanua, kwasasa bado kuna mahitaji ya mabati 34 ,malori sita ya mchanga ,maroli manne ya kokoto na mifuko ya saruji 60 ili kukamilisha ujenzi huo.

"Tunashukuru uongozi wa kampuni hii, chini ya Mkurugenzi Mohsin Bharwani ambae ameguswa na jambo hili, Mohsin amekuwa akijitoa katika masuala ya kijamii kwenye maeneo mengi ndio na sisi tuliamua kumuomba msaada na tunashukuru kutusaidia "

Aidha Mtiga alitoa wito kwa makampuni na wadau wengine kuendelea kujitolea kwani bado kuna uhitaji.

Aliiomba jamii Miono kuendelea kushirikiana katika masuala ya maendeleo ili kujiinua kimaendeleo ikiwemo kuboresha sekta ya elimu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya Refuelling Tanzania limited, Mohsin Bharwani, Meneja wa kampuni hiyo Renatus Kabeyo alisema wamekabidhi mabati 72 na kusafirisha jumla milioni mbili (mil.2).

Alifafanua kuwa, kampuni hiyo inashirikiana na jamii kwa kila jambo kulingana na uwezo wao.

"Nimeona kuna madarasa tunaona mnajenga ,vyoo ,niweze kuahidi tutajenga hoja ,pamoja na misaada inayokuja nikuombe ofisa elimu kata andika andiko ,ili mpate misaada mikubwa kutoka kwa wadau mbalimbali" alieleza Kabeyo.

Kabeyo alisema wanafunzi wanasoma ila wanatakiwa kusoma kwenye mazingira bora.

Sunday, June 9, 2024

375 WAFAULU BUNDIKANI SEC YAFUTA ZIRO

SHULE ya Sekondari ya Kata ya Maili Moja Bundikani Halmashauri ya Mji Kibaha imefanikiwa kufaulisha wanafunzi wote wa kidato cha nne 375 kufaulu na kuondoa daraja sifuri.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bernard Muyenjwa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Muyenjwa alisema kuwa ufaulu huo ni asilimia 100 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne waliofanya mitihani yao mwaka jana.

"Wanafunzi 234 wamefaulu kwenda kidato cha tano na vyuo mbalimbali vya kati ambapi ufaulu huo ni sawa na asilimia 65 huku wengine wakisubiri uteuzi wa awamu ya pili,"alisema Muyenjwa.

Alisema kuwa jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 375 wasichana wakiwa 218 wavulana 157 ambapo daraja la kwanza walikuwa 22 wasichana tisa wavulana 13.

"Daraja la pili 79 wasichana 53 wavulana 26 daraja la tatu 144 wasichana 73 wavulana 71 na daraja la nne ni 130 wasichana 83 wavulana 47 huku daraja sifuri kukiwa hakuna hata mmoja,"alisema Muyenjwa.

Aidha alisema kuwa mafanikio hayo yalitokana na mshikamano walionao walimu na kujitolea, kusimamia vizuri mipango iliyowekwa ya kufikia ufaulu.

"Ushirikiano kati ya shule, wazazi na bodi, kusimamia nidhamu kwa wanafunzi na kuhimiza walimu kufundisha kwa kasi na mazoezi ya mara kwa mara na ufuatiliaji, ufanyaji wa mitihani kila Jumamosi,"alisema Muyenjwa.

Aliongeza kuwa upande wa nidhamu ni kuweka uzio na walinzi ili kudhiti wanafunzi kutoka bila ya sababu zisizokuwa na msingi bali iwe ya msingi ndipo atoke au muda wa kuingia shuleni.

"Malengo ni kuhakikisha tunapunguza wanafunzi wanaopata daraja la nne na kuongeza ufaulu wa daraja la kwanza wafikie angala 60 au 70 na hilo linawezekana,"alisema Muyenjwa.

Alibainisha kuwa shule yao ambayo ni kinara kwa shule za Kata kwa kufaulisha kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha ikiwa inazidiwa na shule ya Tumbi na Kibaha wasichana ambazo ziko chini ya Shirika la Elimu Kibaha.

"Tunaishukuru Serikali kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa vinne na changamoto zilizopo ni ndogondogo ambazo ziko ndani ya uwezo wetu walimu wapo wa kutosha zaidi ya 100,"alisema Muyenjwa.

Aliwaomba wazazi na wadau kuendelea kutoa ushirikiano ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne na kufikia malengo ya kuwa na kidato cha tano na sita.