CHAMA cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimeiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa watu wanaokutwa na hatia ya kuwakata viungo au kuwaua watu wenye Ualbino.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Taifa wa TAS Godson Mollel alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya siku kuongeza uelewa juu ya Ualbino (IAAD) duniani.
Mollel amesema kuwa Mahakama ikotoa hukumu kali kwa wahusika hao itakuwa fundisho kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha kuwadhuru watu wenye Ualbino.
Naye ofisa ustawi mkuu toka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye ulemavu Joy Maongezi amesema kuwa sheria namba 9 ya mwaka 2010 inataka kuwa na haki kwa watu wenye ulemavu ambapo watu wenye Ualbino ni sehemu yao.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala amesema kuwa wakati wa maadhimisho hayo huduma mbalimbali zinatolewa ikiwa ni pamoja na upimaji saratani ya ngozi, utoaji miwani, kofia na losheni ya kuzuia ngozi kuathirika, upimaji wa tezi dume na kansa ya kizazi.
Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka duniani ambapo kilele huwa tarehe 13 Juni kila mwaka na kwa mwaka huu kitaifa yanafanyika Kibaha Mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment