Tuesday, June 25, 2024

GRACE JUNGULU ATOA TOFALI 300

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Picha ya Ndege Grace Jungulu ametoa tofali 300 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kibaha Mjini.

Hayo yamesemwa na Katibu wa UWT Kibaha Mjini Cecilia Ndalu wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Jumuiya hiyo kilichofanyika mjini Kibaha ambapo aliwashukuru wote waliochangia tofali ili kufanikisha ujenzi huo.

Ndalu amesema anawashukuru wanaccm waliojitolea kuchangia tofali ili ujenzi huo usichelewe na kukamilika kwa wakati kama malengo yaliyowekwa.

Ndalu amesema kuwa katika harambee hiyo jumla ya tofali 1,500 zilipatikana kwa ajili ya ujenzi huo ambapo mlezi wa UWT Selina Koka alitoa tofali 500 huku Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akitoa mifuko ya simenti 100.

"Malengo yetu ni kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu ujenzi huo uwe umekamilika ili kuepusha katibu kuishi kwenye nyumba ya kupanga ambapo pia itapunguza gharama,"amesema Ndalu. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Eline Mgonja amesema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha mipango yote waliyojiwekea ikiwemo ujenzi huo na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mgonja amesema kuwa juu ya uchaguzi wamejipanga kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Naye Mgeni rasmi kwenye Baraza hilo Mbunge Koka amesema kuwa ataendelea kushirikiana na umoja huo katika kuhakikisha chama kinapiga hatua na kuwaletea wananchi maendeleo.

Koka amesema kuwa ili kufanikisha ushindi wa chama wanawake lazima waungane washirikiane na kuacha kugawanyika kwani wasiposhirikiana watakigawanya chama.

No comments:

Post a Comment