Saturday, June 8, 2024

LAMI KUWEKWA SHELI MAILI MOJA






WANANCHI wanaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya BP Sheli-Maili Moja yenye urefu wa kilometa nne wametakiwa watoe ushirikiano ili kufanikisha ujenzi huo.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi alipokuwa akizungumza na wananchi wakati wa utoaji elimu juu ya mradi huo ambao kwa sasa uko kwenye hatua ya usanifu.

Lutambi amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na benki ya dunia umeanza kwa kufanya usanifu hivyo wananchi wasiweke vikwazo ili hatua hiyo ambayo ni ya miezi nane iweze kwenda vizuri bila ya kikwazo chochote.

"Tunawaomba wananchi muonyeshe ushirikiano kwani kujengwa lami kwa barabara hii ni mkombozi kwa Kata yetu na italeta maendeleo na kurahisisha shughuli mbalimbali hasa za usafirishaji,"amesema Lutambi.

Amesema kuwa katika kutekeleza mradi huo hakutakuwa na fidia kwa sehemu ambazo nyumba zimejengwa barabarani itakapopita barabara hiyo ambayo inaanzia barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro.

"Tusije tukakwamisha mradi ukikwama mradi utahamishiwa sehemu nyingine hivyo hii ni fursa kwetu tusiiache kwani kukwamisha ni kushindwa kujiletea maendekeo kwani barabara ni maendeleo na fursa zitajitokeza kwa wingi kupitia barabara,"amesema Lutambi. 

Kwa upande wake mwakilishi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA Mhandisi Fredrick Nzogela amesema kuwa hatua ya usanifu itakamilika mwezi wa tisa ambapo mkandarasi atakabidhi taarifa ambayo itaonyesha baadhi ya maeneo yatakayo athirika.

Nzogela amesema kuwa barabara hiyo itakuwa na upana wa mita 8.5 na itakuwa na mitaro pande zote pamoja na kuwekwa taa na alama mbalimbali na matuta sehemu ambazo ni hatarishi hususani kwenye eneo la shule.

Kaimu Mtendaji wa Kata ya Maili Moja  Mwanawetu Said amewataka wananchi wasiwe na hofu kwani athari hazitakuwa kubwa kama wanavyofikiri na sehemu zitakazo athirika ni kidogo sana.

Said amesema kuwa sehemu zitakazo athirika wahusika wasikwamishe kufanyika kwa ujenzi huo kwani kuukwamisha ni kuyakataa maendeleo ndani ya maeneo yao.

Naye Mhandisi Kiza Mwesigwa ambaye anasimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa ujenzi wa changarawe kabla ya kuwekwa lami amesema ujenzi wake utakuwa kuchonga na kuweka kifusi na kushindilia itakuwa na urrefu wa kilometa .

Mwesigwa amesema kuwa mradi huo utaanza mwezi huu kuanzia wiki ijayo na utakuwa wa miezi sita hadi mwezi Novemba itakuwa na urefu wa kilometa moja na mita 800.

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa elimu juu ya mradi huo waliitaka Halmashauri kutoa elimu ya kutosha juu ya utekelezaji mradi huo.

Wamesema wako tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo na kuwaweka wazi ili wajue maeneo ambayo yameonekana kuzidi ili waweze kuhamisha vitu vyao mapema.





No comments:

Post a Comment