WILAYA ya Kibaha imejiwekea lengo la kukusanya chupa za damu 700 hadi 800 kwa mwaka ili ziweze kusaidia wahitaji wakiwemo akinamama wanaojifungua watoto na majeruhi wa ajali.
Hayo yamesemwa na mratibu wa damu salama wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Nyaisawa Birore alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye zoezi la uchangiaji damu kwenye Kituo cha Afya Mlandizi.
Birore amesema kuwa wamejiwekea malengo ya kukusanya chupa 85 hadi 200 kwa kipindi cha robo mwaka ili ziweze kutumika kwa wagonjwa wenye mahitaji ya damu.
"Matumuzi ya damu kwa mwezi yalikuwa ni chupa 45 lakini yameongezeka na kufikia ni chupa 80 hadi 100 hivyo mahitaji ni makubwa sana na tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kujitolea,"amesema Birore.
Moja ya wachangiaji wa damu ambaye ni katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kibaha Vijijini Joel Kijuu amesema ameamua kujitolea ili kusaidia kuokoa maisha ya akinamama na wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
Kwa upande wake mhamasishaji uchangiaji damu Mariam Ngamila amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa na dhana kuwa damu inayochangwa inauzwa kitu ambacho siyo cha kweli.
Naye mhamasishaji uchangiaji damu Maria Ngamila amesema tone moja la damu linaweza kuokoa maisha ya watu wengi hivyo vijana wahamasike kuchangia damu.
Faudhi Kinanga ambaye yuko kwenye kambi ya uchangiaji damu amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa vijana kushiriki zoezi la uchangiaji damu ili kuisaidia jamii.
No comments:
Post a Comment