Monday, October 9, 2017

SIMBA WAKIWA WAMEPOZI

ATAKA WATHAMINI RAIS KUREJESHA RASILIMALI ZA NCHI




Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama amesema anasikitishwa na watu wanaomsema vibaya Rais Dk John Magufuli kwa kutothamini kile anachokifanya katika kurejesha rasilimali za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha alisema kuwa kazi inayofanywa na Rais inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania yoyote anayeitakia mema nchi yake.
Mshama alisema kuwa kutokana na jitihada anazozifanya wananchi wanapaswa kumuunga mkono kwa kubainisha wale ambao hawana uzalendo na nchi yao.
“Rais kasikia kero nyingi na sasa ameanza kutekeleza kwa vitendo mfano masuala ya usafiri, upatikanaji wa dawa, suala la madini, reli na masuala ya viwanda iweje watu waanze kumsemea vibaya na kumwita majina yasiyofaa jambo hili halikubaliki,” alisema Mashama.
Alisema kuwa kuna njia nzuri za kumfikishia ujumbe hata kama unaona anakosea lakini siyo kumwambia maneno mabaya yasiyofaa ni vema kutumia njia nzuri.
“Hata vitabu vya dini vinatuelekeza kutii mamlaka iliyopo na mamlaka yoyote imewekwa na Mungu hivyo lazima watu wanapaswa kuheshimu mamlaka,” alisema Mshama.
Aidha alisema anatoa pole kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu kwa kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana hivi karibuni mkoani Dodoma.
“Tunampa pole Tundu Lisu kwa kujeruhiwa na tunaamini watu waliohusika na tukio hilo watakamatwa tu na wananchi ndiyo watakaojua wafanywe nini watu hao,” alisema Mshama.
Alibainisha kuwa kwa sasa nchi imeingia kwenye matukio ambayo si ya kawaida ikiwa ni pamoja na watoto kutekwa watu kujeruhiwa kwa silaha utamaduni ambao si Wawatanzania na haupswi kuungwa mkono.
“Matukio kama haya na mengine ya ukatili kama yaliyokuwa yakitokea wilaya ya Kibiti ya kuwaua watu wasio na hatia ni mambyo mabaya na serikali imedhamiria kupambana nayo kwa nguvu zote,” alisema Mshama.
Aliwataka Watanzania kuendelea kuiombea nchi imani ili iendelee kuwa Kisiwa cha amani na kuachana na watu wanaotaka kuichafua nchi ili ionekane ina matatizo.
Mwisho.
John Gagarini, Kibaha
WATUMISHI wa Umma ambao wanaotumia vyeti vya kughushi wametakiwa kujiondoa wenyewe kwani endapo watabainika watapelekwa kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na kurudisha fedha wanazojipatia kupitia mishahara.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angela Kairuki wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kairuki alisema kuwa watumishi wa umma nchini wanaotumia vyeti vya kughushi au visivyo vyao wajiondoe wenyewe mara moja katika utumishi wa umma kwani wakiendelea kukaa itawagharimu na endapo watabainika watatakiwa kurejesha mishahara ya miezi yote waliyoiibia serikali.
“Hata kwa upande wa watumishi ambao hawajahakikiwa kwenye zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi nao wanatakiwa wajiondoe kwani wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na fedha wanazolipwa kupitia mshahara watazirudisha,” alisema Kairuki.
Alisema kuwa makatibu tawala wa mikoa wanapaswa kuangalia na kujiridhisha na majina ya watumishi kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na ya kwenye zoezi la uhakiki kama yanafanana.
“Majina yalioonekana kwenye zoezi la uhakiki ndiyo yanayopaswa kuonekana kwenye orodha ya ya malipo ya mishahara na kama kuna mtumishi hajahakikiwa anatakiwa aondolewe kwenye malipo ya mshahara,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa serikali itaendelea na zoezi kuhakikiwa watumishi hadi itakapojiridhisha kuwa hakuna watumishi ambao hawana sifa kwenye utumishi wa umma.

Mwisho.

Sunday, October 8, 2017

UJENZI WA BANDARI KAVU KWALA KIBAHA KUPUNGUMZA MSONGAMANO



Na John Gagarini, Kibaha

IMEELEZWA kuwa ukamilikaji wa Bandari Kavu ya Kwala wilayani Kibaha mkoani Pwani itasaidia kupunguza msongamao wa malori Jijini Dar es Salaam kwani makontena yote yanayoingia nchini hayatashushwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam badala yake yatashushwa kwenye bandari mpya ya Kwala.

Kutokana na ujenzi huo wa Bandari Kavu ya Kwala mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kupanga mipango mji kwenye Kijiji hicho cha Kwala kwani sasa inaenda kuwa Mji.

Ndikilo aliyasema hayo alipotembelea mradi huo ambao ulianza mwezi Machi mwaka huu ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 7.2 ukijengwa na kampuni ya kizalendo ya Suma JKT chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

“Halmashauri mnapaswa kuhakikisha mnaweka mipango miji kwenye eneo hilo ili kusiwe na ujenzi holela pia kuwe na huduma zote kuanzia mahoteli sehemu ya magari kusubiria siyo zije kujengwa na watu binafsi, polisi, mabenki na huduma nyingine muhimu,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa Hlmashauri isisubiri hadi mradi uishe ndiyo ianze kuweka mipangomiji kwani wanatakiwa kwenda sambamba na ujenzi wa mradi ili kuwe na mpangilio mzuri.

“Hichi kitakuwa kitovu cha biashara na kutakuwa na shughuli nyingi hivyo lazima kuwe na mpangilio mzuri wa ujenzi kwani hata barabara ya kuja huku ni mbaya lazima mamlaka zinazohusika zianze kuboresha mazingira na mara kazi zitakapoanza mwakani serikali ijipatie mapato,” alisema Ndikilo.

Naye Meneja mradi Mhandisi Raymond Kweka alisema kuwa wanatarajia kukamilisha Novemba 30 mwaka huu kwa awamu ya kwanza ujenzi huo ambao unaendelea vizuri ukiwa umefikia asilimia 85 kwenye eneo la mradi lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 150.

Kweka alisema kuwa baadhi ya changamoto kubwa ni mvua baada ya barabara ya Vigwaza Kwala kukatika na maji kujaa kwenye eneo la mradi, maji yanatoka mbali ambapo mwanzo walitegemea bwawa jirani na mradi ambao limeendelea kukauka na kukosa maji.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya ya Kibaha Beda Mbaga alisema kuwa wanatarajia kuanza kupitia maeneo yanayozunguka mradi huo ili kuweka mipangomiji kuanzia wiki hii kwa 


Mwisho.

WAANDISHI WA HABARI NCHINI WAASWA










Na John Gagarini, Kibaha

WAANDISHI wa Habari mkoani Pwani na hapa nchini wametakiwa kutotumia vibaya kalamu zao ili kulinda amani ya nchi kwani maneno yao endapo yatatumika vibaya ni hatari zaidi ya bunduki.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama wakati akifungua kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani mafunzo juu ya Haki za Binaadamu Utawala Bora na Amani nchini kwa Viongozi na watumishi wa serikali za mitaa mkoa wa Pwani yaliyoandaliwa na Alpha And Omega Reconciliation And Peace Building (AREPEB).

Mshama alisema kuwa waandishi wana nafasi kubwa ya kudumisha amani iliyopo kwa kutumia vyema kalamu zao katika kuleta mshikamano na kuepusha utengano.

“Nyie ndiyo mnanafasi kubwa ya kuifanya nchi iendelee kuwa na amani au mnaweza kuifanya nchi ikaingia kwenye machafuko hivyo mnatakiwa kutumia vizuri kalamu zenu kwa kutotumia vibaya kalamu zenu,” alisema Mshama.

Alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia viongozi hao kuwahamasisha wananchi kulinda amani ya nchi na kutokubali kuingia kwenye migogoro ambayo itasababisha amani kuvunjika.

“Tanzania bado tuna amani kubwa na ya kutosha hatuna sababu ya kuleta vurugu kwani nchi inatawaliwa kwa utawala wa sheria lakini kuna baadhi ya watu wanataka kutuingiza kwenye matatizo,” alisema Mshama.

Naye mkurugenzi wa  (AREPEB) Francis Luziga alisema kuwa lengo lao kubwa ni kujenga amani hapa nchini kwa kubadilishana uzoefu na viongozi na watendaji wa serikali za mitaa na wasimamizi wa watekelezaji wa sheria katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

Luziga alisema kuwa pia mafunzo hayo yameambatana na uzinduzi wa mfumo wa kieletroniki wa kupokea maoni na malalamiko dhidi ya masuala mazima ya haki za binadamu.


Mwisho. 

MKUU WA WILAYA KIBAHA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WATENDAJI




Na John Gagarini, Kibaha

MKUU wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama amesema kuwa serikali inawafanyia tathmini watendaji wa mitaa vijiji na vitongoji na wale ambao watashindwa kufikia vigezo wataondolewa ili kupisha wale wenye weledi wafanyekazi ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Ameyasema hayo mjini Kibaha wakati wa mkutano na viongozi hapo pamoja na wenyeviti kwenye Halmashauri za Mji na wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na kusema baadhi ya watendaji wamekuwa hawawajibiki ipasavyo.

Nao baadhi ya wenyeviti walielezea changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Marco Njau alikiri kuwepo kwa baadhi ya changamoto.

Naye kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Beda Mbaga amesema kuwa watakabili changamoto zilizo kwenye eneo lao ili kuleta maenedeleo kwa wananchi.

Naye Ernest Shalua ambaye ni mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wilaya ya Kibaha amesema kuwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa watuhumiwa lazima viongozi na wananchi watoe tushahidi kwenye matukio mbalimbali.

mwisho.  



Saturday, October 7, 2017

CCM WILAYA YA BAGAMOYO YAPATA MWENYEKITI MPYA










Na John Gagarini, Bagamoyo

ABDUL Zahoro Sharifu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kumshinda aliyekuwa mwenyekiti Alimasi Masukuzi.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika Msata wilayani humo Sharifu alimshinda mpinzani wake kwa kupata kura 711 dhidi ya kura 383 za Masukuzi huku Tariq Kafuku akipata kura 185 na nafasi ya Katibu Mwenezi ilikwenda kwa John Francis maarufu kama Bolizozo aliyepata kura 112 akimshinda Hassan Sharifu aliyepata kura 4.

Kutokana na ushindi huo Sharifu amesema kuwa chama ndiyo kilichoshinda na siyo yeye na kuwataka wagombe na wanachama kuwa kitu kimoja ili kukijenga chama kwa ajili ya kuendelea kushika dola.

“Kuanzia sasa hakuna makundi makundi yamekwisha baada ya uchaguzi na kila mtu anahaki ya kuwa na mgombea anayempenda lakini kwa kuwa mshindi kashapatikana hakuna sababu ya kuwa na makundi,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa baada ya uchaguzi kwisha malengo yake ni kujenga chama kwa kuanzisha vitega uchumi na kuachana na tabia ya kutegemea kuomba fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama.

“Furaha yangu ni kuona chama kinajitegemea chenyewe kwa kujiendesha kwani kina miradi mingi na endapo itasimamiwa vizuri itakiletea manufaa chama,” alisema Sharifu.

Kwa upande wake Bolizozo alisema kuwa kwa kutumia nafasi yake atahakikisha anashirikiana na viongozi na wanachama kuleta maenedeleo ya chama ili kiweze kwenye chaguzi kuanzia ya serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Mwisho.


CCM KIBAHA MJINI WACHAGUA VIONGOZI WAKE








Na John Gagarini, Kibaha

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mkoani Pwani Maulid Bundala amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa chama hicho.

Bundala alifanikiwa kutetea nafasi yake hiyo kwa kipindi cha awamu tatu sasa baada ya kushinda kwenye uchaguzi ambao ulifanyika kwenye shule ya sekondari ya Filbert Bayi mjini Kibaha na kuwashinda wenzake wawili.

Wajumbe wa mkutano huo mkuu wa CCM Kibaha Mjini walimpa ushindi wa kishindo Bundala kwa kumpigia kura 288 kati ya kura 489 za wajumbe wote huku kukiwa hakuna kura iliyoharibika.

Aliyemfuatia mshindi alikuwa ni Batholomew Nyalusi ambaye alipata jumla ya kura 164 akifutaiwa na Joseph Masenga ambaye alipata kura 37.

Kwa upande wa uwakilishi wa mkutano mkuu wa mkoa washindi wawili walikuwa ni Rugemalila Rutatina kura 392 na Happines Mgalula kura 201 kwa upande wa uwakilishi Halmashauri Kuu wilaya wajumbe wawili ni Kabunda Bekari kura 238 na Philemon Mabuga  kura 209.

Nafasi nne za uwakilishi toka Umoja wa Vijana (UVCCM) nafasi nne ni Makwiro selaman kura 289, magreth Mbawala kura 283, Herman Kagaruki kura 269 na Jagala Salum kura 233.

Kwa upande wa uwakilishi Jumuiya ya Wanawake (UWT) nafasi nne washindi walikuwa ni Zamda Komba kura 276, Dk Alice Karungi kura 255, Joyce Mushi 230 na Joyce Shauri kura 185.

Washindi wa nafasi tatu za uwakilishi mkutano mkuu wa Taifa ni Abdulaziz Jaad kura 355, Catherine Katere kura 336, Dk Alice Kaijage 332 ambapo katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri na hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa wagombea.


Mwisho.