Monday, October 9, 2017
ATAKA WATHAMINI RAIS KUREJESHA RASILIMALI ZA NCHI
MKUU wa wilaya ya Kibaha Asumter
Mshama amesema anasikitishwa na watu wanaomsema vibaya Rais Dk John Magufuli
kwa kutothamini kile anachokifanya katika kurejesha rasilimali za umma.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha alisema kuwa kazi inayofanywa na Rais
inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania yoyote anayeitakia mema nchi yake.
Mshama alisema kuwa kutokana na
jitihada anazozifanya wananchi wanapaswa kumuunga mkono kwa kubainisha wale
ambao hawana uzalendo na nchi yao.
“Rais kasikia kero nyingi na
sasa ameanza kutekeleza kwa vitendo mfano masuala ya usafiri, upatikanaji wa
dawa, suala la madini, reli na masuala ya viwanda iweje watu waanze kumsemea
vibaya na kumwita majina yasiyofaa jambo hili halikubaliki,” alisema Mashama.
Alisema kuwa kuna njia nzuri za
kumfikishia ujumbe hata kama unaona anakosea lakini siyo kumwambia maneno
mabaya yasiyofaa ni vema kutumia njia nzuri.
“Hata vitabu vya dini
vinatuelekeza kutii mamlaka iliyopo na mamlaka yoyote imewekwa na Mungu hivyo
lazima watu wanapaswa kuheshimu mamlaka,” alisema Mshama.
Aidha alisema anatoa pole kwa
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu kwa kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na
watu wasiojulikana hivi karibuni mkoani Dodoma.
“Tunampa pole Tundu Lisu kwa
kujeruhiwa na tunaamini watu waliohusika na tukio hilo watakamatwa tu na
wananchi ndiyo watakaojua wafanywe nini watu hao,” alisema Mshama.
Alibainisha kuwa kwa sasa nchi
imeingia kwenye matukio ambayo si ya kawaida ikiwa ni pamoja na watoto kutekwa
watu kujeruhiwa kwa silaha utamaduni ambao si Wawatanzania na haupswi kuungwa
mkono.
“Matukio kama haya na mengine ya
ukatili kama yaliyokuwa yakitokea wilaya ya Kibiti ya kuwaua watu wasio na
hatia ni mambyo mabaya na serikali imedhamiria kupambana nayo kwa nguvu zote,”
alisema Mshama.
Aliwataka Watanzania kuendelea
kuiombea nchi imani ili iendelee kuwa Kisiwa cha amani na kuachana na watu
wanaotaka kuichafua nchi ili ionekane ina matatizo.
Mwisho.
John Gagarini, Kibaha
WATUMISHI wa Umma ambao
wanaotumia vyeti vya kughushi wametakiwa kujiondoa wenyewe kwani endapo
watabainika watapelekwa kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na kurudisha
fedha wanazojipatia kupitia mishahara.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angela
Kairuki wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, watumishi wa
Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kairuki alisema kuwa watumishi
wa umma nchini wanaotumia vyeti vya kughushi au visivyo vyao wajiondoe wenyewe mara
moja katika utumishi wa umma kwani wakiendelea kukaa itawagharimu na endapo
watabainika watatakiwa kurejesha mishahara ya miezi yote waliyoiibia serikali.
“Hata kwa upande wa watumishi
ambao hawajahakikiwa kwenye zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi nao
wanatakiwa wajiondoe kwani wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na
fedha wanazolipwa kupitia mshahara watazirudisha,” alisema Kairuki.
Alisema kuwa makatibu tawala wa
mikoa wanapaswa kuangalia na kujiridhisha na majina ya watumishi kwenye orodha
ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na ya kwenye zoezi la uhakiki kama
yanafanana.
“Majina yalioonekana kwenye
zoezi la uhakiki ndiyo yanayopaswa kuonekana kwenye orodha ya ya malipo ya
mishahara na kama kuna mtumishi hajahakikiwa anatakiwa aondolewe kwenye malipo
ya mshahara,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa serikali
itaendelea na zoezi kuhakikiwa watumishi hadi itakapojiridhisha kuwa hakuna
watumishi ambao hawana sifa kwenye utumishi wa umma.
Mwisho.
Sunday, October 8, 2017
UJENZI WA BANDARI KAVU KWALA KIBAHA KUPUNGUMZA MSONGAMANO
Na John
Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA
kuwa ukamilikaji wa Bandari Kavu ya Kwala wilayani Kibaha mkoani Pwani
itasaidia kupunguza msongamao wa malori Jijini Dar es Salaam kwani makontena
yote yanayoingia nchini hayatashushwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam badala
yake yatashushwa kwenye bandari mpya ya Kwala.
Kutokana na
ujenzi huo wa Bandari Kavu ya Kwala mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist
Ndikilo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kupanga mipango mji kwenye
Kijiji hicho cha Kwala kwani sasa inaenda kuwa Mji.
Ndikilo
aliyasema hayo alipotembelea mradi huo ambao ulianza mwezi Machi mwaka huu
ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 7.2 ukijengwa na kampuni ya kizalendo ya
Suma JKT chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
“Halmashauri
mnapaswa kuhakikisha mnaweka mipango miji kwenye eneo hilo ili kusiwe na ujenzi
holela pia kuwe na huduma zote kuanzia mahoteli sehemu ya magari kusubiria siyo
zije kujengwa na watu binafsi, polisi, mabenki na huduma nyingine muhimu,”
alisema Ndikilo.
Alisema kuwa
Hlmashauri isisubiri hadi mradi uishe ndiyo ianze kuweka mipangomiji kwani wanatakiwa
kwenda sambamba na ujenzi wa mradi ili kuwe na mpangilio mzuri.
“Hichi
kitakuwa kitovu cha biashara na kutakuwa na shughuli nyingi hivyo lazima kuwe
na mpangilio mzuri wa ujenzi kwani hata barabara ya kuja huku ni mbaya lazima
mamlaka zinazohusika zianze kuboresha mazingira na mara kazi zitakapoanza
mwakani serikali ijipatie mapato,” alisema Ndikilo.
Naye Meneja
mradi Mhandisi Raymond Kweka alisema kuwa wanatarajia kukamilisha Novemba 30
mwaka huu kwa awamu ya kwanza ujenzi huo ambao unaendelea vizuri ukiwa umefikia
asilimia 85 kwenye eneo la mradi lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 150.
Kweka alisema
kuwa baadhi ya changamoto kubwa ni mvua baada ya barabara ya Vigwaza Kwala
kukatika na maji kujaa kwenye eneo la mradi, maji yanatoka mbali ambapo mwanzo
walitegemea bwawa jirani na mradi ambao limeendelea kukauka na kukosa maji.
Kwa upande
wake kaimu mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya ya Kibaha Beda Mbaga alisema kuwa
wanatarajia kuanza kupitia maeneo yanayozunguka mradi huo ili kuweka
mipangomiji kuanzia wiki hii kwa
Mwisho.
WAANDISHI WA HABARI NCHINI WAASWA
Na John
Gagarini, Kibaha
WAANDISHI wa
Habari mkoani Pwani na hapa nchini wametakiwa kutotumia vibaya kalamu zao ili
kulinda amani ya nchi kwani maneno yao endapo yatatumika vibaya ni hatari zaidi
ya bunduki.
Hayo
yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama wakati
akifungua kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani mafunzo juu ya Haki za Binaadamu
Utawala Bora na Amani nchini kwa Viongozi na watumishi wa serikali za mitaa
mkoa wa Pwani yaliyoandaliwa na Alpha And Omega Reconciliation And Peace
Building (AREPEB).
Mshama
alisema kuwa waandishi wana nafasi kubwa ya kudumisha amani iliyopo kwa kutumia
vyema kalamu zao katika kuleta mshikamano na kuepusha utengano.
“Nyie ndiyo
mnanafasi kubwa ya kuifanya nchi iendelee kuwa na amani au mnaweza kuifanya
nchi ikaingia kwenye machafuko hivyo mnatakiwa kutumia vizuri kalamu zenu kwa
kutotumia vibaya kalamu zenu,” alisema Mshama.
Alisema kuwa
mafunzo hayo yatawasaidia viongozi hao kuwahamasisha wananchi kulinda amani ya
nchi na kutokubali kuingia kwenye migogoro ambayo itasababisha amani kuvunjika.
“Tanzania
bado tuna amani kubwa na ya kutosha hatuna sababu ya kuleta vurugu kwani nchi
inatawaliwa kwa utawala wa sheria lakini kuna baadhi ya watu wanataka
kutuingiza kwenye matatizo,” alisema Mshama.
Naye
mkurugenzi wa (AREPEB) Francis Luziga
alisema kuwa lengo lao kubwa ni kujenga amani hapa nchini kwa kubadilishana
uzoefu na viongozi na watendaji wa serikali za mitaa na wasimamizi wa
watekelezaji wa sheria katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora.
Luziga
alisema kuwa pia mafunzo hayo yameambatana na uzinduzi wa mfumo wa kieletroniki
wa kupokea maoni na malalamiko dhidi ya masuala mazima ya haki za binadamu.
Mwisho.
MKUU WA WILAYA KIBAHA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WATENDAJI
Na John
Gagarini, Kibaha
MKUU wa
wilaya ya Kibaha Asumter Mshama amesema kuwa serikali inawafanyia tathmini
watendaji wa mitaa vijiji na vitongoji na wale ambao watashindwa kufikia vigezo
wataondolewa ili kupisha wale wenye weledi wafanyekazi ili kuwaletea maendeleo
wananchi.
Ameyasema
hayo mjini Kibaha wakati wa mkutano na viongozi hapo pamoja na wenyeviti kwenye
Halmashauri za Mji na wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na kusema baadhi ya
watendaji wamekuwa hawawajibiki ipasavyo.
Nao baadhi ya
wenyeviti walielezea changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili kwenye maeneo
yao.
Kwa upande
wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Marco Njau alikiri kuwepo
kwa baadhi ya changamoto.
Naye kaimu
mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Beda Mbaga amesema kuwa
watakabili changamoto zilizo kwenye eneo lao ili kuleta maenedeleo kwa wananchi.
Naye Ernest
Shalua ambaye ni mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wilaya ya Kibaha amesema kuwa
ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa watuhumiwa lazima viongozi na wananchi watoe
tushahidi kwenye matukio mbalimbali.
mwisho.
Saturday, October 7, 2017
CCM WILAYA YA BAGAMOYO YAPATA MWENYEKITI MPYA
ABDUL Zahoro Sharifu
amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo
mkoani Pwani baada ya kumshinda aliyekuwa mwenyekiti Alimasi Masukuzi.
Uchaguzi huo
ambao ulifanyika Msata wilayani humo Sharifu alimshinda mpinzani wake kwa
kupata kura 711 dhidi ya kura 383 za Masukuzi huku Tariq Kafuku akipata kura
185 na nafasi ya Katibu Mwenezi ilikwenda kwa John Francis maarufu kama
Bolizozo aliyepata kura 112 akimshinda Hassan Sharifu aliyepata kura 4.
Kutokana na
ushindi huo Sharifu amesema kuwa chama ndiyo kilichoshinda na siyo yeye na
kuwataka wagombe na wanachama kuwa kitu kimoja ili kukijenga chama kwa ajili ya
kuendelea kushika dola.
“Kuanzia sasa
hakuna makundi makundi yamekwisha baada ya uchaguzi na kila mtu anahaki ya kuwa
na mgombea anayempenda lakini kwa kuwa mshindi kashapatikana hakuna sababu ya
kuwa na makundi,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa
baada ya uchaguzi kwisha malengo yake ni kujenga chama kwa kuanzisha vitega
uchumi na kuachana na tabia ya kutegemea kuomba fedha kwa ajili ya kuendesha
shughuli za chama.
“Furaha yangu
ni kuona chama kinajitegemea chenyewe kwa kujiendesha kwani kina miradi mingi
na endapo itasimamiwa vizuri itakiletea manufaa chama,” alisema Sharifu.
Kwa upande
wake Bolizozo alisema kuwa kwa kutumia nafasi yake atahakikisha anashirikiana
na viongozi na wanachama kuleta maenedeleo ya chama ili kiweze kwenye chaguzi
kuanzia ya serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.
Mwisho.
CCM KIBAHA MJINI WACHAGUA VIONGOZI WAKE
Na John Gagarini, Kibaha
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mkoani Pwani Maulid
Bundala amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa
chama hicho.
Bundala alifanikiwa kutetea nafasi yake hiyo kwa kipindi cha awamu
tatu sasa baada ya kushinda kwenye uchaguzi ambao ulifanyika kwenye shule ya
sekondari ya Filbert Bayi mjini Kibaha na kuwashinda wenzake wawili.
Wajumbe wa mkutano huo mkuu wa CCM Kibaha Mjini walimpa ushindi wa
kishindo Bundala kwa kumpigia kura 288 kati ya kura 489 za wajumbe wote huku
kukiwa hakuna kura iliyoharibika.
Aliyemfuatia mshindi alikuwa ni Batholomew Nyalusi ambaye alipata
jumla ya kura 164 akifutaiwa na Joseph Masenga ambaye alipata kura 37.
Kwa upande wa uwakilishi wa mkutano mkuu wa mkoa washindi wawili
walikuwa ni Rugemalila Rutatina kura 392 na Happines Mgalula kura 201 kwa
upande wa uwakilishi Halmashauri Kuu wilaya wajumbe wawili ni Kabunda Bekari
kura 238 na Philemon Mabuga kura 209.
Nafasi nne za uwakilishi toka Umoja wa Vijana (UVCCM) nafasi nne
ni Makwiro selaman kura 289, magreth Mbawala kura 283, Herman Kagaruki kura 269
na Jagala Salum kura 233.
Kwa upande wa uwakilishi Jumuiya ya Wanawake (UWT) nafasi nne
washindi walikuwa ni Zamda Komba kura 276, Dk Alice Karungi kura 255, Joyce
Mushi 230 na Joyce Shauri kura 185.
Washindi wa nafasi tatu za uwakilishi mkutano mkuu wa Taifa ni
Abdulaziz Jaad kura 355, Catherine Katere kura 336, Dk Alice Kaijage 332 ambapo
katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri
na hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa wagombea.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)