Sunday, August 6, 2017

WATOTO WAFA MTO RUVU MMOJA WA MIEZI MINNE













Na John Gagarini, Chalinze

WATU watatu wakiwemo mtoto wa miezi minne na wa mwaka mmoja wamekufa huku watu wawili wakinusurika kifo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Ruvu.

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa licha ya watu hao kubainika kufa dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 5 majira ya saa 4:00 asubuhi wakati watu hao walipokuwa wakijaribu kuvuka mto kutoka Vigwaza kwenda Mlandizi kwenye mto Ruvu wilaya ya kipolisi Chalinze.

“Ajali hiyo imepoteza maisha ya watoto wawili ambao ni Nusrat Haji miezi minne na Feisal Hamza mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu pamoja na Sikuzani Musa (41) ambaye mwili wake bado haujapatikana,” alisema Shana.

Alisema kuwa walionusurika ni Zuwena Ramadhan (29) na Tero Mziray (20) ambapo dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo na inaaminika hakufa maji.

“Chanzo cha mtumbwi huo kuzama bado kinachunguzwa na miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi,” alisema Shana.

Aliwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuhakikisha vinakuwa kwenye hali nzuri ili kuepukana na ajali kama hizo ambazo zinapoteza uhai wa watu kutokana na ubovu.

Mwisho.   


WAETHIOPIA 72 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUINGIA NCHINI BILA YA KIBALI

Moja ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni wahamiaji haramu kutoka nchi ya Ethiopia akiwahudumia wenzake kwa kuwapa mikate kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Kipolisi ya Chalinze baada ya kukamatwa huko Ruvu Vigwaza wilayani Bagamoyo mkoani Pwani

 Moja ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni mhamiaji haramu toka nchi ya Ethiopia akiwekewa uji pembeni ni askari akisubiri kupewa uji kwa ajili ya kuwapa watuhumiwa hao.

 Baadhi ya waethiopia wanaotuhumiwa kuingia nchini bila ya kibali wakipata kifungua kinywa cha uji.

 Askari akiwapatia mikate watu wanaotuhumiwa kuingia nchini bila ya kibali raia wa Ethiopia wakipata uji.

 Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shana akiwa mbele ya watu ambao wanatuhumiwa kuwa ni wahamiaji haramu  kutoka nchi ya Ethiopia ambao walikamatwa mkoani humo.
Na John Gagarini, Chalinze

HUKU Serikali ikiwa inaweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu hapa nchini Jeshi la polisi mkoa wa Pwani limewakamata wahamiaji haramu 72 kutoka nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo cha wilaya ya Kipolisi ya Chalinze kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa wahamiaji hao walikuwa safarini kwenda Afrika ya Kusini.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 5 majira ya saa 3:30 asubuhi kwenye Pori la Ranchi ya Taifa (NARCO) kata ya Vigwaza wilaya ya Kipolisi ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.

“Mbali ya wahamiaji hao haramu pia tunamshikilia Rajabu Hitaji (30) mkazi na mfanyabiashara wa Vigwaza baada ya msako mkali uliofanywa na makchero wa jeshi la polisi baada ya kupata taarifa kuwa kuna wahamiaji haramu wameingia bila ya kibali,” alisema Shana.

Alisema kuwa wahamiaji hao haramu baada ya kugundua kuwa kuna gari la polisi linawafuatilia waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kujificha lakini msako mkali uliofanywa uliweza kuwabaini na kukamata kundi la kwanza la watu 63 ambao walikaa sehemu ambayo gari haliwezi kufika.

“Baada ya kuwakamata wahamiaji hao haramu kundi la kwanza askari waliendelea na msako ambapo waliwakamata wahamiaji wengine tisa waliokuwa wakijaribu kutaka kutoka kwenye pori hilo,” alisema Shana.

Alisema kuwa wahamiaji hao haramu wanatarajiwa kukabidhiwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya hatua za kisheria pamoja na mfanyabiashara aliyekamatwa ambaye anatuhumiwa kuwasafirisha.


Mwisho.

Friday, August 4, 2017

AUWAWA NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI KWA TUHUMA ZA WIZI


Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi limesema kuwa bado linaendelea kumshikilia kijana wa kiume mkazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambaye alivalia mavazi ya kike ikiwemo dera hijabu na kuficha sura yake kwa kuva nikabu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa kijana huyo alikamatwa Agosti 2 maeneo ya Picha ya Ndege barabara ya kuelekea Magereza huku akiwa amevaa mavazi hayo.

Shana alisema kuwa kwa sasa jeshi hilo bado linamshikilia kijana huyo kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao anaoshirikiana nao kwenye matukio ya uhalifu.

“Kijana huyu tulimkamata baada ya kumwekea mtego uliowekwa na makachero wetu waliokuwa wamepata taarifa kutoka kwa wasiri waliokuwa wanamtilia mashaka na walifanikiwa kumkamata akiwa kwenye bodaboda akielekea maeneo ya Magereza,” alisema Shana.

Alisema kuwa hadi sasa bado hawajajua kijana huyo alikuwa na lengo gani la kuvaa nguo hizo za kike hali ambayo hadi sasa bado haijafahamika hasa alidhamiria nini.

“Hadi sasa tunaendelea kumhoji kujua ni kwanini avae mavazi ya kike na tunawashukuru wananchi na wasiri wetu kwa kuendelea kutupa ushirikiano wa kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu,” alisema Shana.


Mwisho.

KIJANA WA KIUME MVAA DERA BADO ASHIKILIWA NA POLISI


Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi limesema kuwa bado linaendelea kumshikilia kijana wa kiume mkazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambaye alivalia mavazi ya kike ikiwemo dera hijabu na kuficha sura yake kwa kuva nikabu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa kijana huyo alikamatwa Agosti 2 maeneo ya Picha ya Ndege barabara ya kuelekea Magereza huku akiwa amevaa mavazi hayo.

Shana alisema kuwa kwa sasa jeshi hilo bado linamshikilia kijana huyo kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao anaoshirikiana nao kwenye matukio ya uhalifu.

“Kijana huyu tulimkamata baada ya kumwekea mtego uliowekwa na makachero wetu waliokuwa wamepata taarifa kutoka kwa wasiri waliokuwa wanamtilia mashaka na walifanikiwa kumkamata akiwa kwenye bodaboda akielekea maeneo ya Magereza,” alisema Shana.

Alisema kuwa hadi sasa bado hawajajua kijana huyo alikuwa na lengo gani la kuvaa nguo hizo za kike hali ambayo hadi sasa bado haijafahamika hasa alidhamiria nini.

“Hadi sasa tunaendelea kumhoji kujua ni kwanini avae mavazi ya kike na tunawashukuru wananchi na wasiri wetu kwa kuendelea kutupa ushirikiano wa kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu,” alisema Shana.


Mwisho.

Thursday, August 3, 2017

WAZIRI NCHEMBA ALIA NA WANAOWASIDIA WAHAMIAJI HARAMU





                                    Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imesema imefika wakati kuwakamata watu wanaowasaidia kuwalipia faini wanazopigwa wahamiaji haramu mara wanapohukumiwa mahakamani.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alipotembelea ofisi za Uhamiaji mkoa wa Pwani na kusema kuwa watu hao ndiyo wanaosababisha kuendelea kuingia kinyume cha sheria wahamiaji haramu.

Nchemba alisema kuwa nchi imekuwa ikiingia gharama kubwa kuwatunza wahamiaji haramu wanapoingia nchini na nchi kutumia muda mwingi kuhangaika na wahamiaji hao.

“Hii ni mipango kwani wameshafanya biashara hii kama halali na kuona kuwa hata wakiwalipia adhabu za fedha zinazotolewa na mahakama na kufanya wahamiaji hawa kuingia mara kwa mara hivyo wanaokuja kuwalipia nao kamateni, magari wanayosafirishia wahamiaji haramu taifisheni na boti wanazotumia kamateni,” alisema Nchemba.

Alisema inashangaza kuona Watanzania eti wanawalipia faini wanazopigwa kama adhabu baada ya kubainika kuingia nchini bila ya kibali jambo hilo halikubaliki.

“Hii ni biashara ambayo kuna baadhi ya wenzetu wanajihusisha nayo ndiyo maana tatizo hili haliishi na pia kuna baadhi ya watumishi wa serikali nao wanahusika na tutawachukulia hatua kali watakaobainika kushiriki kwenye mtandao huu wa kuwaingiza wahamiaji haramu,” alisema Nchemba.

Aidha alisema kuwa nchi haiwezi kutumia fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya kununulia dawa za wagonjwa mahospitalini, kujenga barabara, kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu na fedha hizo kuzipeleka kuwahudumia wahamiaji haramu jambo hilo hatutakubali liendelee.

Awali Ofisa Uhamiaji mkoa Plasid Mazengo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja usafiri na boti kwa ajili ya kudhibiti wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakitumia bandari ya Bagamoyo ambayo ina vipenyo vingi vya kuingilia nchini.

Mazengo alisema kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa wakalimani kwa ajili ya kutafsiri lugha za Kihabeshi na upungufu wa watumishi kwenye baadhi ya wilaya.

Mwisho.

PICHA YA NDEGE WAPATA ENEO UJENZI SHULE YA SEKONDARI

Na John Gagarini,Kibaha

KATA ya Picha ya Ndege imepata eneo lenye ukubwa wa hekari 11 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Kata ambapo kwa sasa wanafunzi wanaotoka kata hiyo wanasoma shule ya sekondari ya kata kwenye mtaa wa Mkuza.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata hiyo Robert Machumbe wakati wa mkutano wa kata uliofanyika kwenye shule ya Msingi ya Lulanzi na kusema kuwa eneo hilo limepatikana kutokana na jitihada zake na wananchi.

Machumbe alisema kuwa licha wanafunzi wanaotoka kwenye kata yake wanasoma kwenye mazingira magumu kwani darasa moja linawanafunzi 450 hali ambayo inafanya usomaji kuwa mgumu.

“Watoto wetu wanapata shida kwanza kule ni mbali na pia madarasa yao yamejaa wanafunzi hivyo hupunguza ari ya usomaji na ufaulu kuwa mdogo,” alisema Machumbe.

Naye Thomas Raymond alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo itakuwa mkombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye kata hiyo ambayo ni mpya ikiwa haina shule yake ya sekondari.
Raymond alisema kuwa wao wako tayari kuchangia ujenzi wa shule hiyo mara wakati utakapofika ili kuhakikisha shule hiyo inajengwa haraka kwenye kata yao.

Mwisho.


HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAOMBWA KUTENGA FEDHA KWA WATU WENYE ULEMAVU

Na John Gagarini, Kibaha

WADAU wa watu wenye ulemavu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wameiomba Halmashauri hiyo kutenga asilimia moja ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukabili changamoto za ulemavu.

Hayo yalisemwa na Methew Chungu mwezeshaji wa  mafunzo yaliyoandliwa na Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Kibaha Mjini kwa wadau wa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu.

Chungu alisema kuwa mapato hayo yangesaidia kuwapatia huduma mbalimbali watu wenye ulemavu zikiwemo za kiafya, elimu, kiuchumi na huduma nyingine za kiutu.

Naye katibu wa SIVYAWATA Kibaha Mjini Happiness Matagi alisema kuwa kwa sasa changamoto za upataji huduma kwa watu wenye uelemavu zimepungua ambapo kumwona daktari kwa ni bure.

Matagi alisema kuwa kupitia kituo chao cha watu wenye ulemavu kilichopo Kwa Mfipa wanatoa huduma mbalimbali za kiafya hasa kwa wale walemavu wa viungo pamoja na shughuli za ujasiriamali.

“Pale watu wenye ulemavu wanafanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuma, kushona nguo na mradi wa matofali ambao uko mbioni kuanza lengo kuwakwamua watu wenye ulemavu ili wasijione wanyonge na kuachana na tabia ya kuomba ambayo itawafanya washindwe kujitegemea,” alisema Matagi.

Kwa upande wake mwakilishi wa mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dk Mariamu Mgaya alisema kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakisaidia ili kuhakikisha wanapata huduma za afya bila ya usumbufu kwa kuwapa kipaumbele.

Akijibu baadhi ya hoja ofisa mipango wa Halmashauri ya Mji Kibaha Amkauane Ngilangwa alisema kuwa katika bajeti iliyopitishwa watu wenye ulemavu wametengewa kiasi cha shilingi milioni 10.


Ngilangwa alisema kuwa pia wanapatiwa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuta ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi albino ili ngozi zao zisiharibike na fimbo kwa ajili ya wasioona.